Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Madaba Songea.

Wananchi wa Kata ya Mtyangimbole, Kijiji cha IKalangiro kilichopo Wilaya ya Songea Vijijini wametakiwa kutofanya makosa katika marudio ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata hiyo utakaofanyika Septemba 19, mwaka huu na kuombwa kumchagua mgombea anayetokana na Chama cha Mapinduzi, Twahibu Diwani Ngonyani.

Kauli hiyo imetolewa na mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama wakati akizindua kampeni hizo katika Jimbo la Madaba mkoani Ruvuma ambapo alikutana na viongozi wa Chama pamoja wanachama wa CCM Kata.

Alisema kuwa, chama cha Mapinduzi kimewaletea mgombea sahihi ambaye atawatumikia wananchi na kushirikiana na Serikali kutatua kero zao ili kuwaletea maendeleo kulingana na kasi ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Wananchi mnawajibu wa kuhakikisha mnachagua mgombea anayetoka na CCM katika uchaguzi huu wa marudio ili kukamilisha mafiga matatu na kunufaika na chama chenu chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo,” alisema Mbunge Jenista Mhagama.

Aidha Mbunge huyo alisema, Ilani inayotekelezwa kwa sasa ni ya Chama cha Mapinduzi na kuwataka kumchagua Twahibu Diwani Ngonyani ili aweze kuisimamia Ilani hiyo kwa vitendo akisema kuwa, jukumu la chama cha Mapinduzi ni kuleta maendeleo na kuwataka kukikopesha imani chama hicho kwa kumchagua mgombea wake nacho kitawalipa maendeleo.

“Serikali imejipanga kutatua kero za maji na katika huduma za afya kuna mikakati ya ujenzi wa vituo vya afya kwa lengo la kuwapungiza adha wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma muhimu hali inayorudisha nyuma maendeleo,” Ameeleza Mbunge Jenista Mhagama.

Katika hatua nyingine Mbunge huyo aliwataka wakinamama kuhakikisha wanawahimiza vijana na kinababa kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kumchagua mgombea anayetokana na CCM akieleza kuwa ni nia njema ya Serikali kuhakikisha inaboresha miundo mbinu ya barabara, upatikanaji wa mbolea kwa wakulima kwa bei nafuu ili kulima kilimo chenye tija.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Songea Vijijini Bw. Thomas Masolwa amewahimiza kumchagua Twahibu kwa ajili ya maendeleo yao ni siyo wagombea wengine kutokana na uzoefu wake ndani ya Chama hivyo atakuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.

Naye Mgombea wa Udiwani katika Kata ya Mtyangimbole Bw. Twahibu Diwani Ngonyani akinadi sera zake ameahidi kushirikiana na wananchi wa Kata hiyo pindi watakapomchagua kwa kumpa ushindi wa kishindo.

By Jamhuri