Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Bagamoyo

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, migongano baina ya binadamu na wanyamapori imekuwa ni tatizo kubwa na kumekuwa na ongezeko kubwa la uharibifu wa mali na kusababisha majeraha kutoka kwa wanyamnapori.

Kwa kulitambua hilo, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi ili kusaidia kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Akifungua mafunzo kwa wanahabari wa mazingira yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania(JET), ambapo mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Wizara ya Kiuchumi na MaendeleoSerikali ya Ujerumani (BMZ), Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele, wilayani Bagamoyo, juu ya Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika suala la utoaji elimu ya uhifadhi.

“Tunampongeza sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa namba moja katika suala la uhifadhi na kwa ubunifu wa kutangaza rasilimali zilizopo katika maeneo ya hifadhi na kuchangia kukuza uchumi utokanao na sekta ya utalii,” amesema Mapepele.

Tanzania imepiga hatua kubwa katika uhifadhi kwa zaidi ya asilimia 32 na hiyo imetokana na juhudi kubwa inayofanywa na Rais Samia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika uhifadhi mazingira nchini.

Amesema kuwa wizara ina falsafa mbili kubwa ikiwemo Uhifadhi na Utangazaji utalii na hivyo mafunzo hayo lengo lake kuu ni kusaidia katika kuimarisha uhifadhi ili usaidie katika utangazaji utalii suala mabalo ni muhimu kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“Tumeweka nguvu nyingi katika kutangaza rasilimali zetu na kwa mujibu wa bajeti iliyopita takwimu zinaonesha sekta ya utalii ilichangia asilimia 25 ya fedha za kigeni na asilimia 21 ya pato la taifa,” ameongeza.

Mapepele amesema bila uhifadhi hakuna uhai ndio maana wamekuwa wakiwahamasisha jamii kutunza maeneo ya hifadhi ili kusaidia kuepusha migongano kati yao na wanyama.

Amesema wanafanya hivyo kwa sababu wizara imepewa dhamana ya kusimamia, kulinda maeneo ya wanyamapori kukuza uchumi na kuendeleza utalii kwa lengo la kuzalisha ajira.

Aidha, amebainisha kuwa, Tanzania ni moja ya nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika eneo la uhifadhi ambapo asilimia 32 ya nchi imehifadhia jambo ambalo ni la kupongezwa.

Kwa upande wake, Mshauri wa Mradi wa kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyapori nchini unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Anna Kimambo, amesema mradi huo utatekelezwa katika wilaya tatu za Namtumbo,Tunduru mkoani Ruvuma na Liwale mkoani Lindi na kutekelezwa kwa vijiji 30 ambayo vimebainika kupata matukio makubwa ya wanyamapori.

“Kutatua migogoro baina ya binadamu na wanyamapori sio jukumu la wizara au serikali bali ni la Watanzania wote, hivyo mafunzo haya tunatarajia yatasaidia kujua vyanzo vya migogoro mbalimbal na kusaidia kupunguza migogoro itokanayo na binadamu na wanyama,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), John Chikomo, ameishukuru GIZ na Serikali ambapo amebainisha kuwa mafunzo yatawasaidia waandishi kutoa habariwa mazingira kuelimisha jamii na kusaidia kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

“Mafunzio haya ya siku mbili yatawasaidia kuelimisha jamii katika wilaya tatu yenye vijiji 30 katika mkoa wa Lindi na Ruvuma ambako kumekuwa na migongano ya mara kwa mara kati ya binadamu na wanyama na kusababisha madhara,” amesema.

Chikomo amesema kuwa mradi huo ni wa mwaka mmoja na umelenga kuboresha uwezo wa wadau muhimu nchini wanaohusika kudhibiti na kutatua migongano ya binadamu na wanyamapori.

“Mafunzo haya yatawawezesha wanahabari kupata elimu mbalimbali za kupunguza madhara kwa jamii zilizoathirika zaidi katika eneo la mradi hivyo na kutoa elimu iliyojitosheleza kwa jamii,” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa JET, Dk.Ellen Otaru amesema kuwa malengo ya mafunzo hayo ni kupata taarifa ya namna ya kutokomeza kwa usahihi migogoro kati ya binadamu na viumbe wengine na kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuidhibiti.

Katika kukabiliana na ongezeko la idadi ya wau, mahitaji ya ardhi kwa ajili ya maliasi, mifugo, kilimo na miundombinu imeongezeka.

Hii imesababisha watu na maisha yao kuathiriwa zaidi na uharibifu unaofanywa na wanyamapori, hasa katika maeneo jirani na hifadhi na katika shoroba za wanyamapori.

By Jamhuri