Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Hadithi ya maendeleo ya taifa letu haiwezi kukwepa kuzungumzia ushirikiano wa taasisi za dini, hususan Kanisa Katoliki.

Tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1964, Kanisa Katoliki limefanya mambo mengi katika kuchagiza maendeleo ya wananchi.Katika maeneo mengi ya nchi yetu, taasisi hii imekuwa ikiendesha na kusimamia huduma muhimu za kijamii kama vile shule, hospitali na hata vyuo vikuu.

Kama hiyo haitoshi, miradi hii inayoendelezwa kupitia taasisi za dini hususan Kanisa Katoliki haiangalii watu wa imani zao, ila Watanzania wote wamekuwa wakipata huduma hizo muhimu.

Kwa kutambua mchango mkubwa wa uwapo wa taasisi hizi, ndiyo sababu ya msingi iliyomfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aone haja ya kwenda Vatican, Italia kukutana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.

Mazungumzo ya wawili hawa yalifanyika Februari 12, 2024, yakiongeza chachu ya ushirikiano katika kuhudumia wananchi wa Tanzania.

Kwa nchi kama Tanzania inayohaha kujiletea maendeleo, vikao na ziara kama hizi zinafanyika wakati sahihi kwa sababu zinaibua hisia za uungwaji mkono katika pande zote mbili.

Aidha, zinawathaminisha wadau hawa ili waendelee kuiunga mkono nchi yetu. Akiwa Vatican, Rais Samia alifanya mazungumzo ya faragha na Papa Francis, kabla ya kujumuika na watendaji wengine.

Hii ni heshima si tu kwa Dk. Samia, bali kwa Watanzania wote.

Huwezi kuwa kiongozi mzuri kama hauna ushawishi. Aidha, lazima uwe na uwezo wa kusikilizwa kwa sababu yapo mambo unayohitaji msaada wa wengine.

Ni kwenye mazungumzo hayo ambayo viongozi hawa waliangazia hoja za uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania, mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu hususan kwenye sekta muhimu kama vile elimu, afya na ustawi wa jamii bila kusahau changamoto mbalimbali ambazo nchi inapitia.

Hoja nyingine muhimu ni masuala yote ya kijamii, kikanda, kimataifa pamoja na suala la amani ambayo siku zote nchi yetu imekuwa alama nzuri ya kutiliwa mfano katika mataifa mengine duniani.

Taarifa zinaonyesha Rais Samia si kiongozi wa kwanza kutembelea Vatican. Miaka 12 iliyopita, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, alizuru nchini humo na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Januari 19, 2012, wakizungumza faragha kwa dakika 15.

Kama ilivyokuwa kwa Rais Samia, kikao cha Rais Kikwete na Baba Mtakatifu Benedikto kilijikita kwenye ajenda ya dini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, afya, ustawi,maendeleo na mafao ya wengi.

Kwa kuangalia kwa haraka, utagundua mbali na kujikita kwenye miradi inayoisaidia nchi yetu, bado kanisa hili limekuwa likisisitiza mno umuhimu wa amani na uimarishaji wa demokrasia.

Kanisa linaamini demokrasia na amani vikitamalaki hata maendeleo yanayopigiwa
kelele yatapatikana kwa urahisi.

Bila amani hakuna uwekezaji unaoweza kufanyika si kwa wazawa, hata wageni kutoka nje ya nchi watashindwa kufanya hivyo.

Hivyo hoja hizi zinazozingatiwa na Rais Samia sanjari na Kanisa Katoliki zina tija.

Historia inaonyesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa Aprili 19, 1968 na Askofu Mkuu Pierluigi Sartorelli akiteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania.

Tangu wakati huo hadi leo kanisa limekuwa likipigania ajenda zenye manufaa kwa wananchi, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ustawi na maendeleo makubwa kwa nchi yetu.

Kupitia nyanja kama vile elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, ni vigumu kama huko kote hautakutana na ramani nzuri iliyosimikwa kufuatia uwapo wa Kanisa Katoliki.

Nchini Tanzania, taarifa zinaonyesha Kanisa Katoliki pekee ukiacha taasisi nyingine za kidini, linamiliki na kuendesha shule za awali 240, shule za msingi 147, wakati sekondari ni 244.

Kama hiyo haitoshi, Tanzania pia kuna vyuo vya ufundi vitano; taasisi za elimu ya juu tano na vituo vya vyuo vikuu viwili vinavyomilikiwa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT).

Vyuo hivi vina jumla ya wanafunzi 31,000 Haya ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu kutokana na ushirikiano wa serikali ya Rais Samia na uwapo wa Kanisa Katoliki.Bahati nzuri yanafanyika haya hadharani, kiasi kwamba kila mtu anaona.

Hivyo juhudi za dhati za taasisi hii zinakwenda sambamba na uwapo wa viongozi wa juu wenye makusudi ya kuendeleza mipango ya serikali kwa kudumisha ushirikiano wa taasisi zenye dhamira ya dhati ya kuwakomboa wananchi.

Juhudi hizi hazipaswi kudharauliwa, kwa sababu zinafanyika kwa nia nzuri. Leo hii
katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, huwezi kukosa mradi ambao unaendeshwa kwa nguvu za wadau hususan taasisi za dini, hasa Kanisa Katoliki.

Bahati nzuri serikali yetu inatambua juhudi hizi. Ndiyo maana unaona serikali imekuwa ikifanya kila namna ili kuzitambua na kuziweka hadharani kama njia ya kukuza ushirikiano mbele ya jamii.

Ni wazi serikali haiwezi kufanya kila jambo. Kwa nchi kama Tanzania, utendaji wa
ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo ni dalili nyingine ya
kulikwamua taifa na kufika pale inapokusudiwa.

Haya ni mambo yanayotakiwa yaungwe mkono na Watanzania wote. Kanisa
linapojenga shule au kituo cha afya wanaokwenda kupata huduma ni Watanzania
wote bila kujali dini zao.

Taifa letu ili liendelee linapaswa kutambua na kuheshimu juhudi za wadau wa maendeleo ili kuvutia muwanda huo kama njia ya kupiga hatua kubwa.

Kwa nchi kama Tanzania, hasa kwa miaka ya karibuni, kamwe haina uwezo wa kufanya kila jambo zaidi ya kutegemea wadau mbalimbali, zikiwamo taasisi za dini.

0712053949

By Jamhuri