Ligi kuu nchini Uingereza leo inaendelea tena ikizikutanisha wapinzani wakubwa kutoka jiji la Manchester, Manchester United na Manchester City ambazo zote zikiwa kwenye mbio za kupigania ubingwa.

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amesema mchezo mkubwa baina yao na Manchester City chini ya Kocha Pep Guardiola hautabiriki.

 

Timu hizo mbili zitakutana kwenye Uwanja wa Old Trafford katika mwendelezo wa Premier League, leo Jumapili.

 

“Soka halitabiriki,” Mourinho alisema na kuongeza: “Kama meneja, naweza kujaribu kuelezea mipango ya mchezo na kuonyesha mwelekeo wangu lakini huwezi jua nini kitatokea. Kuna mambo mengi ambayo yapo nje ya uwezo wangu ambayo yanaweza kuubadili mchezo kabisa.

 

“Kwangu mimi, ni mechi kubwa nyingine dhidi ya timu kubwa katika nchi hii. Tumekuwa timu bora kuliko mwaka jana, nadhani pia Man City ni bora zaidi ya msimu uliopita.”

 

City hawajafungwa katika ligi msimu huu lakini wamepoteza mechi yao ya kwanza katika kampeni za msimu huu katikati ya wiki baada ya kufungwa 2-1 na Shakhtar Donetsk Ligi ya Mabingwa.

 

“Mimi ni meneja mwenye uwezo wa kucheza mechi hizi katika hatua kubwa kama hivi. Ndiyo maana tupo hapa,” alisema Pep Guardiola na kuongeza: “Nitafurahia mechi, ni wazi. Nasubiri kwa hamu kufika pale na kucheza. Napenda kucheza kwenye uwanja ule, tutafanya kila tuwezalo kuwafunga. Baada ya kushikana mikono.

 

“Kushinda, kusare au kufungwa, hatuendi kushinda au kupoteza Ligi ya Uingereza. Ni mechi muhimu kwa sababu tunaweza kushinda pointi, lakini ni hivyo hivyo kwao pia. Tunachowaza ni namna ya kucheza vizuri na kushinda mchezo.”

 

 

By Jamhuri