Katika sehemu ya saba ya makala hii nilihitimisha na aya hii: “Je, unafahamu utaratibu wa kisheria wa kusajili Jina la Biashara, gharama ya usajili, muda wa kukamilisha usajili, nyaraka zinazotakiwa, umri wa mtu anayetaka kusajili Jina la Biashara na matakwa mengine ya kisheria? Usikose nakala yako ya gazeti hili makini la uchunguzi JAMHURI Jumanne ijayo.”

Zimepita wiki nne sasa tangu nimehitimisha hivyo sehemu ya makala hii. Nirejee usemi wangu kuwa nia ya msingi wakati makala hii itakapofikia mwisho nitachapisha kitabu cha ‘Jinsi ya Kufanya Biashara Tanzania’. Mada hizi zitakwenda kwa mtiririko sahihi kwenye kitabu.

Sitanii, nililazimika kusogeza mbele majibu ya maswali hayo hapo juu kutokana na maombi ya wasomaji kutaka kufahamu hatua ningine ambazo zilikuwa za awali kabla ya kusajili Jina la Biashara. Leo najibu baadhi ya maswali haya. Baada ya kufikisha umri wa mtu mzima, yaani miaka 21, ndipo unaruhusiwa kusajili Jina la Biashara.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Jina la Biashara ya Mwaka 1930 kama ilivyorekebishwa mwaka 1972, 2002 na 2007, kusajili Jina la Biashara, iwe ni mtu binafsi au kampuni, inakupasa kutuma kwa njia ya posta au barua iliyosajiliwa kwa Msajili wa Kampuni, fomu maalumu iliyojazwa inayoeleza taarifa zifuatazo:-

(a) Jina la biashara; (b) maelezo ya ujumla kuhusiana na biashara; (c) eneo inakofanyika biashara; (d) jina la kampuni (ikiwa inayosajili Jina la Biashara ni kampuni), jinsia ya mwombaji, jina kamili, utaifa wako, biashara nyingine (kama ipo); (e) tarehe ya kuanza biashara; (f) kama biashara ni ya kampuni, majina ya watu wanaoruhusiwa kufungua akaunti na kusimamia masuala ya fedha kwa niaba ya Jina la Biashara lililosajiliwa.

Sitanii, mtu anayeomba kusajili Jina la Biashara anapaswa kuwasilisha tamko lililotiwa saini na mwombaji au wakurugenzi wa kampuni zinazoomba usajili. Taarifa hizi za kuomba usajili wa Jina la Biashara zinapaswa kuwasilishwa kwa Msajili siku 28 baada ya kuanzisha biashara. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 8(1) cha Sheria ya Usajili wa Jina la Biashara.

Katika makala zilizotangulia, nilieleza muda wa mfanyabiashara kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuomba kukadiriwa mapato. Utaona kupitia sheria hii ya usajili wa Jina la Biashara, inataka mtu atume maombi ya kusajili jina la biashara ndani ya siku 28 baada ya kufungua biashara.

Niongeze kuwa mbali na njia za kutuma kwa msajili nilizozitaja hapo juu, siku hizi Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela) umeimarisha taratibu za kusajili majina ya biashara ambapo kwa sasa unasajili jina la biashara mtandaoni baada ya kujiunga kwenye huduma za mtandaoni Brela.

Kwa mantiki hiyo, inaweza kuchukua siku tatu mpaka mwezi mmoja kupata usajili wa biashara yako. Hii ina maana utakuwa umetimiza miezi miwili katika biashara yako. Ukitoka Brela, unapaswa kuiombea Namba ya Mlipakodi biashara yako, ambayo inapaswa kutumia si zaidi ya wiki moja, ila kwa urasimu wa hapa nchini mpaka unaipata hiyo namba, inaweza kukuchukua wiki mbili.

Sitanii, baada ya kupata namba hiyo unapaswa kwenda kuomba leseni ya biashara kwenye halmashauri/wizara, ambayo mchakato wake unaweza kuchukua mwezi na zaidi kwa kufuata taratibu nilizozieleza katika makala zilizotangulia za kuanzia kwa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa hadi halmashauri kama ni ya mji/wilaya/manispaa/jiji au wizara ndipo upate leseni.

Baada ya kupata leseni unarejea tena TRA kwa ajili ya kukadiriwa kodi unayopaswa kulipa. Hapa utajikuta katika mzunguko huu utakuwa umekata miezi minne hadi sita hivi. Kikubwa ni kwamba unapaswa kutunza kumbukumbu za mauzo na matumizi yako yote tangu siku ya kwanza.

Sitanii, kuna watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wanalipishwa kodi kabla ya kuanza kufanya biashara. Kwa nchi yetu ukienda TRA mkusanya kodi anadhani tayari biashara inafanya kazi na kama nilivyoeleza hapo anaona kama umekuwapo sokoni kwa hadi miezi sita au zaidi, hivyo anakukadiria kodi moja kwa moja.

Ikumbukwe katika usajili yapo majina ambayo Msajili anaweza kuyakataa kisheria. Majina haya ni yale yenye sura ya udanganyifu machoni pa watu. Kwa mfano, huwezi kusajili jina la biashara ukajiita “SERIKALI”. Jina hili linaweza kuwadanganya watu wakadhani ni Serikali ya Tanzania, hivyo ukapata biashara ambayo hukustahili.

Pia, sheria hairuhusu kusajili majina yanayoonyesha kwa mfano kuwa biashara hiyo ni ushirika wa jamii fulani. Kwa mfano jina kama “Chama cha Ushirika Dar es Salaam” itakuwia vigumu kulisajili kama ni mtu binafsi au kampuni maana lina viashiria ambavyo vinaweza kuwaaminisha wananchi kuwa ni ushirika wa wakaazi wa Dar es Salaam hivyo mtu akapata biashara asiyostahili.

Ukitoa taarifa za uongo, utafungwa jela mwaka mmoja au faini isiyozidi shilingi 50,000 au vyote kwa pamoja. Adhabu hii itatolewa pia kwa mkurugenzi aliyetoa taarifa za jina la biashara linalomilikiwa na kampuni zisizo sahihi. Zamani gharama ya kusajili Jina la Biashara ilikuwa Sh 6,000. Hata hivyo, gharama hizi zinabadilika, itakupasa kuwasiliana na Brela. Wiki ijayo usikose mwendelezo wa makala hii kwenye eneo la usajili na aina ya kampuni za biashara.

Please follow and like us:
Pin Share