Jinsi ya kuanzisha biashara Tanzania (21)

Wiki iliyopita sikuzama sana katika mada hii ya kodi. Nawashukuru wasomaji wangu kwa kuendelea kuniletea mrejesho mkubwa katika eneo hili la kodi. Hakika sikufahamu kuwa kumbe watu wengi wana matatizo ya jinsi ya kuanzisha biashara kiasi hiki hadi nilipoanza kuandika makala hii.

Nimeahidi kuwa makala hii nitaichapisha kama kitabu, lakini pia nikiri kuwa kuna baadhi ya maeneo nitapaswa kuyarekebisha maana serikali imefanya mabadiliko makubwa katika eneo la ulipaji kodi kwenye bajeti ya mwaka huu 2019/2020 na sasa ufanyaji biashara unaanza kurahisika, wakirekebisha machache yaliyosalia na nchi ikabadili msimamo, ikatambua kuwa taifa haliwezi kuwa tajiri bila kuwa na wafanyabiashara matajiri.

Sitanii, kwa lugha nyingine, wawekezaji kutoka nje tunaowakaribisha kwa mikono miwili tukitumaini walipe kodi tuweze kuongeza mishahara ya wafanyakazi, kuboresha huduma za jamii kama maji, hospitali, dawa, barabara, viwanja vya ndege, ndege, umeme, treni za umeme, elimu na nyingine nyingi, kwa lugha nyepesi kabisa ni wafanyabiashara wa kimataifa, ila sisi tumewabatiza na kuwaita wawekezaji.

Kwa mantiki hiyo hamu tunayoipata tunapompata mwekezaji kutoka nje tukaona kuwa huyo sasa atakuwa mkombozi kwa kulipa kodi ya maana, tunapaswa kujenga mazingira bora ya kufanya biashara wazawa na kuwaongeza kiwango cha faida. Dunia sasa imebadilika, na hili ni somo nitakuja kulieleza kwa kuliandikia makala ndefu.

Kuna mwelekeo mpya, badala ya kutoza KODI YA MAPATO, dunia sasa inatoza KODI YA MATUMIZI. Kampeni ya kudai risiti tuliyoianzisha, ikienda sabamba na kupunguza kodi ya mapato, nchi yetu itaongeza makusanyo kupitia kodi ya matumizi, ila hapa kwetu tunaiita Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Hili ni eneo linalohitaji siku nzima, kwa maana hata sheria yetu ya kodi haijalirushia jicho kadiri inavyostahili.

Sitanii, mara kadhaa nimeahidi kuwa nitaandika juu ya Kodi ya Makampuni (corporate tax). Wapo watu wanaojiuliza Kodi ya Makampuni ni nini? Kodi hii inatozwa kutokana na kiwango cha faida ilichopata kampuni. Kwa mfano, kama umepata faida ya Sh 100,000 kwa mwaka, basi unapaswa kukata asilimia 30 ya faida hiyo kuilipa TRA kama kodi ya makampuni, ambayo itakuwa ni Sh 33,000.33.

Hapo juu nimetangulia kusema kuwa duniani nchi zinahama kutoka kwenye kodi ya mapato kwenda kwenye kodi ya matumizi. Kwa mfano, kampuni nyingi hapa nchini zimekuwa hazilipi hii kodi kwa

kuonekana zinapata hasara, maana karibu maisha yao yote ni ya biashara.

Hili limekuwa tatizo hadi serikali ikatunga sheria inayotaka kampuni inayopata hasara mfululizo kwa miaka mitatu tangu mwaka 2017 sasa itozwe asilimia 0.3 ya mzunguko wa fedha (turn over) za kampuni kwa mwaka mzima.

Hii ilipitishwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018 zikiwa ni juhudi za kufanya watu walipe kodi. Nimesema nitaiandikia makala juu ya mfumo huu wa kodi kwani kuna njia rahisi ya serikali kupata fedha kutoka kwa wafanyabiashara bila kutumia nguvu. Hii ni kupitia kodi ya matumizi. Nitaizungumzia nitakapofika kwenye eneo la VAT.

Kodi ya makampuni inatozwa katika faida yanayopata mashirika (kampuni), taasisi, vikiwamo vyama vya kijamii, umoja, miungano, ushirika, wasamaria na umoja wowote ambao haukuundwa kama kampuni, iwapo tu utapata faida kutokana na biashara unayoifanya, unalipa hii kodi.

Taasisi nyingine zinazowajibika kulipa kodi hii ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, matawi ya kampuni za kimataifa, vyama vya siasa na wakala wa serikali. Hata hivyo, taasisi mpya zinazowekeza katika utengenezaji wa dawa na uchakataji wa ngozi na mazao yake zikiwa na mkataba wa utekelezaji na serikali zinapaswa kutozwa kodi katika kiwango cha asilimia 20 kwa miaka mitano mfululizo tangu zimeanza biashara.

Kodi hii inatokana na faida inayotokana na kufanya biashara, faida inayotokana na uwekezaji na kodi inayolipwa kutokana na kampuni hesabu zake kuonyesha kuwa imepata hasara kwa miaka mitatu mfululizo.

Je, mfanyabiashara unaufahamu mwaka wa kodi wa taasisi au kampuni yako? Unafahamu makisio na taarifa ya mapato ya biashara au shughuli zako yanafanywaje? Usikose sehemu ya 22 kupitia Gazeti la JAMHURI kila Jumanne kupata majibu haya. Wapo wanaoniuliza namba yangu ya simu, hakika ipo hapo juu kwenye picha yangu. Tuwasiliane.