Wiki tatu zilizopita nilihitimisha makala hii katika sehemu ya 26. Nilieleza nani analipa VAT, utaratibu wa kujisajili, tarehe za kulipa VAT na taratibu nyingine. Nikiri kuwa nimekabiliwa na majukumu mengi ya kitaifa, ikiwamo kuchunguza matreka ya URSUS yanayowatia hasara wakulima. Niombe radhi kuwa sikuandika mada hii kwa wiki mbili zilizopita na nimekuwa nikipokea simu nyingi za kuuliza kulikoni.

Sitanii, leo naendeleza pale nilipoishia. Hatua iliyokuwa inafuata ni kueleza taratibu za jinsi mtu aliyelipa VAT nyingi kuliko alivyopokea anavyopaswa kudai VAT aliyolipa. Ukisikia marejesho ya VAT ni kuwa mfanyabiashara analipwa fedha alizolipa zaidi za VAT ambazo ni nyingi kuliko alizopokea yeye katika biashara.

Mlipa kodi anapokuwa amelipa kodi nyingi ya VAT anarejeshewa fedha alizolipa moja kwa moja kwenye akaunti yake kwa kutumia mfumo wa TISS. Mlipa kodi aliyelipa zaidi anapaswa kujaza fomu Na ITX260.02E, inayoambatana na Cheti cha Uhalisia.

Cheti cha Uhalisia kinatolewa na Mkaguzi wa Hesabu aliyesajiliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu na TRA pia kama Mshauri wa Kodi. Baada ya kupokea madai ya kurejeshewa VAT, Kamishna Mkuu wa TRA anafanya uamuzi katika maombi hayo kulingana na taarifa zilizowasilishwa. Anapaswa ndani ya siku 90 kumjulisha mlipa kodi kiasi atakachorejeshewa na utaratibu utakaotumika kumlipa.

Sitanii, mabalozi na taasisi za kimataifa pia zinapaswa kuomba kwa Kamishna Mkuu wa TRA kurejeshewa VAT waliyolipa kwa kutumia fomu Na. ITX 262.02.E. Kuthibitisha kuwa anayeomba kurejeshewa VAT ni balozi au shirika la kimataifa, madai hayo yanapaswa kuthibitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Pia wanapaswa kuambatanisha ankara za malipo yanayoombewa marejesho.

Hata hivyo, VAT anayopaswa kurejeshewa mlipa kodi, inaweza kutumika kulipia madeni mengine aliyonayo mlipa kodi kwa TRA kama kodi nyingine, faini na riba anazodaiwa na mamlaka hiyo. Hata hivyo, Kamishna Mkuu anapaswa kumwandikia mlipaji kuthibitisha hayo kuwa kodi aliyokuwa anadaiwa imelipa madeni hayo mengine.

Marejesho ya VAT yanapaswa kufanywa kwa mlipa kodi si zaidi ya siku 30 baada ya miezi 6 ya kipindi cha hesabu za mlipa kodi. Ikiwa malipo yamepitiliza siku 30, mlipa kodi anaanza kulipwa riba ya viwango vya benki za biashara zilizopitishwa na Benki Kuu.

Sitanii, kwa mlipa kodi kurejeshewa VAT anapaswa kuwasilisha Cheti cha Uhalisia kilichotolewa na Mhasibu aliyesajiliwa na NBAA na TRA kama Mshauri wa Kodi. Taarifa za ankara zilizozaa madai ya VAT zikiwa zimepangiliwa vizuri zinahitajika. Kwa wafanyabiashara wa mara kwa mara wanapaswa kuwa na Single Bill of Entry, Bill of Lading, Airway bill, Road consignment note, Landing certificate na EFDs receipts/invoices.

Pia inapaswa kuwapo taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu inayoonyesha nini kimenunuliwa na mauzo yaliyozaa hiyo VAT. Kwa watu wenye nia ya kudai kodi waliyolipa, wanapaswa kutambua kuwa ikipita miezi 6 tangu tarehe ya mwisho ulipopewa ankara, basi ufahamu kuwa umesamehe kodi hiyo huwezi kuidai tena hata kama unazo risiti za EFD.

Sitanii, wapo watu wanalipa kodi vizuri lakini mwisho wa siku wanapata matatizo kwa kutopeleka ushahidi kuwa wamelipa kodi TRA. Je, unafahamu kodi zinalipiwa wapi ikiwamo VAT? Usikose sehemu ya 28 ya makala hii Jumanne ijayo ili uweze kukomboa biashara yako na uache kufukuzana na TRA. Tunaanzia wanapoishia wengine. Soma JAMHURI kila Jumanne.

1080 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!