Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii katika sehemu ya 27 kwa kuhoji hivi: “Sitanii, wapo watu wanalipa kodi vizuri, lakini mwisho wa siku wanapata matatizo kwa kutopeleka ushahidi kuwa wamelipa kodi TRA. Je, unafahamu kodi zinalipiwa wapi ikiwamo VAT? Usikose sehemu ya 28 ya makala hii Jumanne ijayo uweze kukomboa biashara yako na uache kufukuzana na TRA. Tunaanzia wanapoishia wengine. Soma JAMHURI kila Jumanne.”

Nilikwishaeleza tarehe za kulipa kodi na taratibu zake, na sasa kuna suala ni bora nikaligusia. Kuna biashara ambazo zina msamaha wa kodi ya VAT. Biashara hizi ni pamoja na uchimbaji madini, mafuta na gesi na Kanda Maalumu za Kiuchumi (SEZ). Hata hivyo, mfanyabiashara anayefanya biashara hizi anapaswa kujaza fomu Na. ITX263.02.E. Fomu hizi zinapatikana katika mtandao wa TRA.

Sitanii, kuna Watanzania wengi hawafahamu jambo jingine. Mfanyabiashara akiingiza nchini mitambo ambayo ni mtaji wa kuanzisha biashara kama mashine na bidhaa nyingine zinazohesabiwa katika kundi la mtaji, anapaswa kuomba kuahirisha kulipa VAT hadi afanye biashara ndani ya miaka 10.

Utaratibu huu wa kuahirisha kulipa VAT kwa muda wa ndani ya miaka 10 tangu umeanzisha biashara katika bidhaa zinazochukuliwa kuwa ni mtaji, unafuatwa pale tu VAT inayopaswa kulipwa inazidi Sh milioni 20. Kama ni chini ya hapo, utaratibu wa kawaida wa kulipa kodi unaendelea.

Mwagizaji wa mzigo hata kama ataahirisha kulipa kodi husika, anapaswa kuionyesha katika hesabu zake za mwaka husika. Muda wa kuahirisha kulipa kodi unapokwisha, kodi hiyo inakuwa hailipwi tena. Hata hivyo, fursa ya kusamehewa kodi hii iliyoahirishwa inatolewa pale tu bidhaa zinazozalishwa zinapokuwa zinalipa kodi na si bidhaa zilizosamehewa kodi.

Sitanii, je, wewe msomaji unafahamu taratibu za kulipa VAT? Kwa makusudi nimeamua kuandika makala hii ambayo inanipa burudani kubwa. Inaniburudisha kwa maana kwamba wafanyabiashara wengi wanapata tabu katika kuendesha biashara. Makala hizi ambazo natarajia kuzichapisha kama kitabu mara nitakapozihitimisha, zinalenga kuwapa majibu Watanzania waliothubutu kufanya biashara.

Kwa kufuata taratibu za sasa, walipa kodi wanapaswa kulipa kodi kupitia benki na kuwasilisha ushahidi wa malipo husika TRA. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka utaratibu kuboresha utendaji kwa njia ya mtandao na huduma bora kwa mlipa kodi. TRA na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zimetengeneza mfumo unaofanana. Mfumo huu unaitwa Revenue Gateway. Mfumo huu mbali na kuziunganisha TRA na BoT, unaziwezesha Benki za Biashara nchini kuunganishwa zikakusanya kodi.

Mfumo huu unasaidia kuonyesha malipo yaliyofanyika katika mifumo ya TRA, ila fedha zinakwenda moja kwa moja Benki Kuu. Mlipa kodi anapoanzisha mchakato wa kulipa kodi kwa kutumia mfumo wa TRA, mfumo unampa mlipa kodi namba maalumu yenye tarakimu 8, hii inaitwa control number. Namba hii inatumika kufanya ulinganisho wa malipo kati ya benki za biashara na TRA.

Mlipa kodi anapeleka ankara ya malipo benki na kuielekeza benki kuhamisha malipo kutoka kwenye akaunti yake kwenda kwenye akaunti ya Kamishna wa TRA iliyopo Benki Kuu. Mfumo huu wa Revenue Gateway unaokoa muda wa mlipa kodi. Kwa sasa imeboreshwa zaidi ambapo mlipa kodi anaweza kulipa kodi husika kwa kutumia mitandao ya simu bila kulazimika kwenda benki.

Mfumo huu umeimarisha kazi ya uhasibu serikalini na ukaguzi wa aina ya malipo yaliyolipwa na mlipa kodi. Mfumo huu unapunguza uwezekano wa binadamu kuingilia mchakato wa malipo, unaongeza uadilifu katika takwimu na umeboresha utunzaji wa kumbukumbu.

Sitanii, mfumo huu umeongeza usalama wa malipo na kwa sasa kila mlipa kodi akifanya malipo, anapokea ujumbe mfupi kwenye simu yake wa kuthibitisha malipo kufanyika. Mfumo huu unapunguza gharama za uendeshaji kwa TRA kwani Mamlaka inakuwa na dirisha moja la kuangalia malipo yanayotoka kwenye benki zote za biashara, ambayo ni rahisi kusimamia na kuendesha.

Je, unafahamu jinsi ya kufanya marejesho ya VAT kwa njia ya mtandao na faida zake? Usikose sehemu ya 29 ya makala hii Jumanne ijayo. Hapa nia ni kuhakikisha unafanya biashara kwa njia sahihi na bila bughudha. Tukutane wiki ijayo.

Please follow and like us:
Pin Share