Jinsi ya kuanzisha biashara Tanzania (29)

Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii katika sehemu ya 28 kwa kuhoji hivi: “Je, unafahamu jinsi ya kufanya marejesho ya VAT kwa njia ya mtandao na faida zake? Usikose sehemu ya 29 ya makala hii Jumanne ijayo. Hapa nia ni kuhakikisha unafanya biashara kwa njia sahihi na bila bughudha. Tukutane wiki ijayo.”

Sitanii, wiki iliyopita nilihoji iwapo msomaji unafahamu mfumo mpya wa uwasilishaji wa malipo ya VAT kwenda TRA kwa njia ya mtandao. Mfumo unaotumika ni mbadala wa kuwasilisha makaratasi TRA, badala yake sasa unawasilisha hesabu zako za mapato na matumizi ya VAT kupitia wavuti (website) wa TRA.

Kuwasilisha mrejesho wa VAT kwa njia ya wavuti wa TRA, unapaswa kujisajili kwa ajili ya kuwasilisha marejesho ya VAT kwa njia ya mtandao. Mlipa kodi aliyesajiliwa kulipa VAT anapaswa kuingia kwenye wavuti wa TRA www.tra.go.tz na kugonga kwenye kitufe cha e-filing. Ukibonyeza mtandao unakupeleka kwenye ukurasa wa kufanya marejesho kwa njia ya mtandao.

Mlipa kodi, awe ni binafsi au kampuni anapaswa kujisajili katika mfumo wa TRA, ambapo anapewa utambulisho unaofahamika kama Electronic Filer Identification Number (e-fin).

Mlipa kodi pia anapewa nywira (password) ya kuanzia kuwezesha atengeneze akaunti yake na nywira yake kwa ajili ya kuingia kwenye mtandao na kufanya marejesho. Kwa kuwa kila anayefanya marejesho anapaswa kusaini marejesho hayo, mtumiaji wa huduma hii anapaswa kupata saini yake kutoka katika mfumo unaofahamika kama Automatic Finger Identification System (AFIS).

Wala usijiulize saini yako itapatikanaje. Ikiwa mlipa kodi au mkurugenzi wa kampuni inayojisajili kufanya marejesho ya VAT kwa njia ya mtandao aliwahi kuomba huduma zifuatazo kutoka TRA, basi saini yake itakuja moja moja, yaani ulipata kuomba; Leseni ya udereva, kusajili gari au uliomba Namba ya Mlipa kodi (TIN), basi saini yako iko kwenye mtandao wa TRA.

Kwa kampuni, mfumo unatumia moja ya TIN za wakurugenzi kutafuta iwapo amepata kuomba moja kati ya huduma hizi zilizotajwa, hivyo saini yake inaletwa. Ikiwa hakuna saini ya mkurugenzi yeyote inayopatikana kati ya wanahisa kwenye kampuni, basi wahusika wanapaswa kwenda ofisi za TRA wanakofanya marejesho na kuchukuliwa saini zao zikaingizwa kwenye mfumo.

Sitani, zipo faida nyingi za kufanya marejesho ya VAT kwa njia ya mtandao. Unapofanya marejesho kwa njia ya mtandao, mlipa kodi anawasiliana na TRA akiwa ofisini kwake. Mfumo huu unamwondolea mlipa kodi adha ya kupanga mstari siku ya marejesho katika ofisi za TRA. E-filing inapunguza makossa na inaharakisha mchakato wa kupitia nyaraka, tofauti na mfumo wa zamani wa makabrasha. Mlipa kodi anaweza kuhifadhi kumbukumbu zake za ulipaji kodi katika mtandao na wakati mwingine anachapa nakala ngumu (hardcopies) na kuhifadhi nakala tete (soft copies) ofisini kwake.

Sitanii, mfumo huu unawaondolea wafanyabiashara manyanyaso ya kukutana na maofisa wanafunzi wanaokuwa TRA wenye usumbufu wa hali ya juu. Kwa kuwa mfumo huu unafanya kazi saa 24, unatoa fursa kwa mlipa kodi kufanya marejesho hata usiku, au muda wa saa zinazoitwa saa za baada ya kazi kwa mazoea, sikukuu au Jumapili.

Kodi hii ya VAT ni kodi inayorahisisha ulipaji kodi. Kama nilivyoeleza katika makala zilizotangulia, kodi hii inalipwa na mtumiaji wa mwisho. Hii ni kodi isiyokuwa ya moja kwa moja. Kwa maana inalipwa baada ya kuongeza thamani ya bidhaa katika hatua mbalimbali.

Mfano, mwenye matunda akiuza matunda, mnunuzi anapaswa kulipa VAT. Aliyenunua akizalisha sharubati (juice) anayemuuzia analipa VAT. Aliyenunua sharubati jumla, wakati anauza kwa mfanyabiashara wa rejareja analipa VAT na mwisho huyu wa rejareja anaongeza VAT wakati anauza sharubati kwa mtumiaji wa mwisho/mlaji.

Kama kuna uelewa wa kutosha wa mfumo huu wa kodi, kila aliyelipa kodi hii kasoro mtumiaji wa mwisho anapaswa kudai kiwango cha kodi alicholipa iwapo kitazidi kiwango alichopokea kutoka kwa wanunuzi wa mwisho katika mkondo wake. Ingawa utaratibu ni mgumu kama nilivyoueleza awali, iwapo umelipa VAT kubwa kuliko uliyopokea, basi unafuata utaratibu na kurejeshewa kodi uliyolipa.

Kwa upande wa kodi za serikali kuu, makala hii inakomea hapa, isipokuwa nitagusia ushuru, stempu, kodi ya michezo ya kubahatisha na Ushuru wa Stempu ya Eelektroniki. Hadi sasa nimejadili kodi ya mapato kwa mtu binafsi, kodi ya makampuni, kodi ya Lipa Kadiri Unavyopata (PAYE), Kodi ya Maendeleo ya Ujuzi, Kodi ya Zuio, Kodi ya Ongezeko la Mtaji na sasa VAT. Wiki ijayo katika sehemu ya 30 nitazungumzia ushuru, stempu, kodi ya michezo ya kubahatisha na stempu ya elektroniki. Asante kwa kusoma JAMHURI.