Kwaheri Dilunga, pengo halizibiki

GODFREY DILUNGA

Wiki iliyopita tumepata pigo. Mhariri wetu wa Gazeti la JAMHURI, Godfrey Dilunga, amefariki dunia Septemba 17, 2019. Namshukuru Mungu tulipata fursa na nafasi ya kufanya kazi na Dilunga. Dilunga aliajiriwa JAMHURI Media Ltd Februari 1, 2019. Kabla ya hapo alifanya kazi na magazeti ya Raia Mwema na Mtanzania.

Alianza kueleza kuwa anapata maumivu ya tumbo Julai, mwaka huu. Alitoka ofisini Alhamisi Septemba 5, hakurejea hadi Jumatatu Septemba 9. Septemba 9, 2019 Mkurugenzi Manyerere Jackton alimpigia simu, akatwambia hali aliyomsikia nayo Dilunga ni vema wakurugenzi tukaenda kumwona.

Tulikwenda nyumbani kwake Kibangu wakurugenzi wawili. Tulipofika mke wake akatwambia wako Hospitali ya Mwananyamala. Tulipofika Mwananyamala hospitalini hali tuliyomkutana nayo, tukashauri apewe rufaa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dilunga aliendelea kuwa pale Muhimbili Wodi ya Mwaisela No. 6, kitanda No. 24 hadi Septemba 16, 2019 tulipomhamishia ICU kitanda No. 3, Wodi No. 6 hiyo hiyo. Kwa bahati mbaya alfajiri ya Septemba 17, 2019 saa 10, akafariki dunia. Nilikuwa mtu wa mwisho kumshuhudia Dilunga akiwa hai baada ya kumhamishia ICU majira ya saa 4 usiku.

Kifo cha Dilunga kimekuwa pigo kubwa kwetu na fundisho kwetu. Alikuwa mchapa kazi, mnyenyekevu, mpole na mwenyekujituma kwa kiwango cha juu. Tumepoteza. Hata hivyo, kuumwa kwa Dilunga kumetufahamisha umuhimu wa bima ya afya. Katika ofisi yetu wafanyakazi wote tumewakatia Bima ya Afya (NHIF) na Bima ya Majanga (WCF). Hakika bima zimetusaidia mno.

Dilunga alielewana na vyama vyote vya siasa na kuwa na urafiki navyo. Upinzani na chama tawala. Ushahidi ni Alhamisi iliyopita pale Mnazi Mmoja. Wanasiasa wote waliosimama walimgombea Dilunga na kusema alikuwa sehemu ya mkakati wao.

Mwaka 2015 wakati Rais John Magufuli anafanya harakati za kugombea urais, alifanya mahojiano na Naibu Mhariri Mtendaji, ambaye pia ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni yetu ya JAMHURI Media Limited, Manyerere Jackton pekee. Manyerere ndiye aliyetangaza nia ya Rais Magufuli kugombea urais.

Baada ya kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mchakato wote wa kugombea urais, Rais Magufuli alifanya mahojiano na mwandishi mmoja tu kipindi chote cha kampeni. Huyu si mwingine bali ni Godfrey Dilunga.

Ni kutokana na uungwana wa Dilunga, pamoja na kukaa naye kwa kipindi kisichozidi miezi sita, kampuni iliamua kutimiza wajibu wa kisheria na kibinadamu kwa ndugu yetu Dilunga. Ilitoa jeneza na kujengea kaburi lake kwa vigae, tukisema mpendwa wetu Dilunga asikandamizwe na udongo.

Tulitoa gari kwa ajili ya kumsafirisha mke wake na wanafamilia kutoka Dar es Salaam hadi  Morogoro na kuwarejesha Dar es Salaam. Wafanyakazi wote wa JAMHURI walioko Dar es Salaam tulikodi gari na kuwatengenezea sare waende Morogoro kumzika Dilunga na kurejea Dar es Salaam. Tulitoa gharama za kuendesha msiba pale Dar es Salaam na Morogoro.

Sitanii, tumefarijika kupokea salamu za pole ambazo nasi tunazifikisha kwa familia kutoka kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli; Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali ambaye alimtuma Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam na Mjumbe wa NEC, Angel Akilimali, aliyemwakilisha Morogoro.

Pia Kiongozi Mkuu wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe (ambaye pia alitoa gari lililopeleka mwili wa Dilunga kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro).

Aidha, Zitto pia alishiriki kumuaga Dar es Salaam na maziko yake Morogoro. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, naye alituma salamu za pole. Orodha ni ndefu, itoshe tu kuwashukuru wote waliotuunga mkono au kututumia salamu katika kipindi hiki kigumu.

Tunawashukuru wadau wote wakiwamo; Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) waliokodi gari hadi  Morogoro ambako tulikuwa nao wahariri zaidi ya 30. Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, vyombo vya habari vyote nchini kwa kuchapisha na kutangaza habari za kifo cha Dilunga, maofisa mawasiliano serikalini (TAGCO) na kundi la tasnia ya habari likiongozwa na Thompson Kasenyenda.

Kipekee niwashukuru PSSSF, ambao walimtuma Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano aliyetoka Dodoma, Unice Chiume hadi Morogoro kushiriki mazishi. Tunawashukuru madaktari wa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala na Hospitali ya Taifa Muhimbili waliomhudumia Dilunga hadi alipoaga dunia.

Sitanii, kwa jinsi tulivyoishi na Dilunga pamoja na kwamba tumekaa naye miezi sita tu, kama tulivyoahidi jijini Dar es Salaam, tunapenda kurejea ahadi tuliyoitoa kuwa Kampuni ya Jamhuri Media Limited itamlipia ada mtoto wa kwanza wa Dilunga katika shule na vyuo vyenye viwango vinavyohimilika, kuanzia saa hadi atakapohitimu digrii ya kwanza.

Watoto wawili wanaosalia, tunaomba mama na familia nao wawasomeshe. Michango iliyokusanywa tutashirikiana na mke wake kufungua akaunti maalumu, ambayo fedha hizo zitawekwa ziwe kianzio cha ada kwa watoto wawili tulioomba mke wa Dilunga na wazazi wawasomeshe.

Hadi tunakamilisha maziko, niliangalia katika makundi mbalimbali michango ilikuwa imefikia kama Sh milioni saba. Tunadhani zitasaidia watoto hao kwa kuanzia.

Familia tunaomba tuendelee kuwa na mawasiliano ya karibu na tuendeleze mshikamano. Tunasikitika Dilunga ametutoka, ila ameacha alama. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana limihmidiwe.