Wiki mbili zilizopita nilihitimisha makala hii katika sehemu ya 29 kwa kuhoji hivi: “Kwa upande wa kodi za serikali kuu, makala hii inakomea hapa, isipokuwa nitagusia ushuru, stempu, kodi ya michezo ya kubahatisha na Ushuru wa Stempu ya Elektroniki. Hadi sasa nimejadili kodi ya mapato kwa mtu binafsi, kodi ya makampuni, kodi ya Lipa Kadiri Unavyopata (PAYE), Kodi ya Maendeleo ya Ujuzi, Kodi ya Zuio, Kodi ya Ongezeko la Mtaji na sasa VAT. Wiki ijayo katika sehemu ya 30 nitazungumzia ushuru, stempu, kodi ya michezo ya kubahatisha na stempu ya elektroniki. Asante kwa kusoma JAMHURI.”

Sitanii, wiki iliyopita nilishindwa kuendelea na mada hii kutokana na Mhariri wa Gazeti hili la Uchunguzi la JAMHURI, Godfrey Dilunga, kufariki dunia. Mbio tulizokuwa nazo za kuanzia kumuuguza hadi mazishi, zilinifanya nishindwe kuandika makala hii inayohitaji utulivu mkubwa wakati wa kuiandika. Bado nia ni ile ile ya kuhakikisha kuwa ninaandika makala hii itakayochapishwa kwenye kitabu kuwezesha Watanzania kufanya biashara kwa kufuata misingi ya kisheria.

Leo ninazungumzia ushuru wa forodha. Ushuru huu ni tozo inayolipishwa kwenye mizigo na huduma maalumu zinazozalishwa hapa nchini au kuagizwa kutoka nje katika viwango tofauti. Kila mwaka inaposomwa bajeti ya serikali, huwa tunamsikia Waziri wa Fedha na Mipango akitangaza bidhaa mbalimbali na viwango vya ushuru zinaotozwa zinapoagizwa kutoka nje ya nchi kuingizwa nchini au zinapozalishwa hapa nchini. Viwango vya ushuru vipo vya aina mbili; viwango maalumu au uwiano.

Bidhaa zinazolipishwa ushuru kwa viwango halisi vinavyofahamika ni pamoja na mvinyo, vinywaji vikali, bia, vinywaji baridi, sharubati za matunda, DVD zilizorekodiwa, VCD, CD, kanda za sauti, sigara, tumbaku, bidhaa za petroli na gesi asilia. 

Pia zipo bidhaa zinazotozwa ushuru kwa uwiano mbazo ni pamoja na huduma za kifedha, mawasiliano, malipo ya TV, samani zilizoagizwa nje, magari, mifuko ya plastiki, ndege maalumu, silaha, mifumo maalumu, vipodozi na dawa. Ushuru wa bidhaa hizi upo katika viwango vya 0%, 5%, 10%, 17%, 15%, 20%, 25% ,30% na 50%.

Sitanii, ushuru unatozwa kwa bidhaa zote zinazoagizwa nje ya nchi iwapo zipo kwenye orodha iliyotangazwa na waziri kwenye Gazeti la Serikali, hadi itakapoelezwa vinginevyo. Pia kwa bidhaa zinazotengenezwa ndani, bidhaa hizi zinalipa ushuru mara tu mtengenezaji anapoiuza bidhaa au pale bidhaa inapoondolewa katika eneo ilipotengenezewa.

Kwa bidhaa zilizosamehewa ushuru, zinaendelea kutumika nchini, lakini siku ambayo aliyesamehewa ushuru akiiuza bidhaa (kwa mfano gari), basi aliyelinunua anapaswa kulipa ushuru mara moja.

Kwa simu za mkononi, za mezani au ya aina yoyote, ushuru unalipwa wakati pesa inapokuwa inakatwa kwa mtumiaji. Pia TV za kulipia, pale mteja anapolipia kuona matangazo yanayorushwa kwa satelaiti, basi hapo hapo ushuru unapaswa kulipwa pia.

Sitanii, iwapo unafanya biashara au unazalisha mojawapo kati ya bidhaa nilizozitaja, unapaswa kuwasilisha marejesho TRA kila mwezi. Kwa bidhaa zinazozalishwa kwa oda, ushuru wake unapaswa kulipwa ndani ya siku 21 baada ya kutengeneza bidhaa. Mtengenezaji wa bidhaa hiyo anapaswa kutoa taarifa za bei inayouzwa bidhaa hiyo na taarifa nyingine kadiri itakavyotakiwa.

Inapotokea mabadiliko ya aina yoyote ya taarifa za idadi ya bidhaa au bei, basi mtengenezaji anapaswa kumfahamisha Kamishna wa TRA mabadiliko hayo ndani ya siku 15 tangu yalipotokea.

Marejesho yanayopelekwa kila mwezi TRA yanapaswa kuonyesha idadi ya bidhaa zilizouzwa na mzalishaji ndani ya mwezi mmoja, bei ambayo bidhaa hizo zimeuzwa na taarifa nyinginezo. Kwa bidhaa zinazotozwa ushuru, kampuni inayozalisha au mtu anapaswa kufanya marejesho kabla ya siku ya mwisho ya kazi ya mwezi unaofuata.

Sitanii, kwa yeyote anayeshindwa kufanya marejesho ya bidhaa alizouza kwa ajili ya kulipa ushuru kwa Kamishna, akibainika anapigwa faini ya Sh 100,000 au asilimia 1 ya kodi iliyostahili kulipwa.

Je, unafahamu kiwango cha ushuru wa forodha na taratibu za kulipa ushuru huo unaponunua gari kutoka nje ya nchi? Tafadhali usikose sehemu ya 31 ya makala hii inayolenga kuwafumbua macho Watanzania katika eneo hili la jinsi ya kuanzisha na kufanya biashara Tanzania. Soma JAMHURI kila Jumanne kwa mafanikio ya biashara zako.

986 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!