Jinsi ya kuanzisha biashara Tanzania (31)

Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii katika sehemu ya 30, kwa kuhoji hivi: “Je, unafahamu kiwango cha ushuru wa forodha na taratibu za kulipa ushuru huo unaponunua gari kutoka nje ya nchi? Tafadhali usikose sehemu ya 31 ya makala hii inayolenga kuwafumbua macho Watanzania katika eneo hili la jinsi ya kuanzisha na kufanya biashara Tanzania. Soma JAMHURI kila Jumanne kwa mafanikio ya biashara zako.”

Sitanii, baada ya wiki iliyopita kuhitimisha makala hii na suala la ushuru wa magari, nimepata simu nyingi hadi sikuelewa. Nikajiuliza mbona wasomaji wangu walikuwa wanapiga na kutuma meseji zisizo nyingi kiasi hiki nikiandika mada za maduka, biashara ya mbao, vifaa vya ujenzi na nyinginezo? Baadaye nimepata jibu. Kumbe magari hayaagizwi na wafanyabiashara, bali na raia wa kawaida.

Nilichobaini, baadhi wanasubiri makala hii ya leo kwa hamu wakagombane na mawakala waliowatolea magari yao bandarini. Mmoja amepiga simu akisema: “Kaka naisubiri kwa hamu makala ya wiki ijayo. Mimi nilinunua gari dola 1,500 Japan, lakini ushuru hapa nikaja kutozwa Sh milioni 3. Naamini wakala alinipiga. Toleo lijalo tupe ukweli tumalize ubishi.”

Kimsingi, naomba kutahadharisha hapa. Hizi gharama nitakazoziandika hapa ni ushuru pekee. Kuna tozo za VAT, ushuru wa Bandari, gharama za wakala mwenyewe na tozo nyingine kadha wa kadha. Hata hivyo, viwango vya ushuru wa magari na matrekta ya kilimo yanayoingizwa nchini, kisheria yanatozwa viwango vifuatavyo vya gharama ya kununua gari au trekta:-

Kwanza, ifahamike kuwa ushuru wa forodha unatozwa kulingana na ukubwa wa injini ya gari, lakini kuna tozo nyingine inayoitwa uchakavu, nayo nitataja viwango vyake pia. Magari yenye injini zenye ukubwa wa Cylinder Capacity (CC) zisizozidi 1,000, hutozwa kiwango cha sifuri (0%).

Magari yenye CC kuanzia 1,000 hadi 2,000 hutozwa ushuru wa kiwango cha asilimia 5. Magari yenye CC kuanzia 2,000 na kuendelea hutozwa kiwango cha asilimia 10 ya bei ya ununuzi. Magari yaliyotumiwa na vipuri vyake pia hutozwa tozo (kodi) ya uchakavu.

Kwa magari ambayo tangu limetengenezwa kiwandani umri wake ni miaka 8 na halizidi miaka 10, basi hutozwa uchakavu kwa kiwango cha asilimia 15 ya bei ya kununulia. Magari ambayo yana umri wa zaidi ya miaka 10 tangu yametengenezwa hadi yanaingizwa nchini, hutozwa kiwango cha asilimia 30. Mabasi yaliyotumika kwa zaidi ya miaka 5 tangu yalipotengenezwa yanatozwa asilimia 10. Vipuri vilivyotumika vya magari na pikipiki vinatozwa asilimia 25.

Sitanii, nasisitiza kuwa hivi ni viwango vya ushuru pekee. Ukiagiza gari, ni lazima ufahamu kodi nyingine ikiwamo tozo za Bandari. Wakati nikieleza viwango vya ushuru wa magari, kuna ushuru wa mawasiliano ya kielektroniki unaotozwa kisheria hapa nchini. Kiwango kinachotozwa ni asilimia 17 ya bei anayotoa mteja kwa huduma anayopata.

Huduma ya mawasiliano ya kielektroniki inatamkwa na sheria kuwa ni huduma yoyote inayotolewa na mtu au kampuni kwa njia ya kurusha matangazo kwa njia ya sauti, picha, kupiga simu, kutuma nukushi, kusafirisha picha kwa mawimbi, kusafirisha ishara (signals) kwa njia na teknolojia yoyote iwayo, basi unalipa hiyo asilimia 17.

Hata hivyo, katika eneo hili mtu anayebanwa kulipa hiyo asilimia 17 ni mtoa huduma, ambaye ana jukumu la kukusanya fedha hizo kutoka kwa mteja mmoja mmoja anayetumia huduma yake. Akiisha kukusanya fedha hizi anawajibika kuziwasilisha TRA bila kuchelewa.

Je, unafahamu kuwa ukiingiza mikanda na vifaa vya muziki nchini unapaswa kulipa ushuru? Usikose sehemu ya 32 ya makala hii inayokaribia mwisho. Soma JAMHURI kila Jumanne.