Wiki hii Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ametimiza miaka 20 baada ya kifo chake. Hatunaye Mwalimu Nyerere kwa miaka 20 sasa. Na kwa kweli nikuombe radhi msomaji wangu kuwa leo kwa upekee na kwa hili tukio la miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, makala ya ‘Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania’ itaendelea wiki ijayo. Niruhusu leo niandike kuhusu Mwalimu Nyerere.

Sitanii, ninafahamu kichwa cha habari cha makala hii kitapokewa kwa hisia na mitazamo miwili. Binafsi nimekuwa na msimamo wa kusema ukweli, wala siyumbi katika hili. Nimekuwapo wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, waliomfuatia na sasa Rais John Magufuli.

Nikisoma vitabu vya historia na nikikumbuka hotuba za Mwalimu Nyerere wakati tukiwa shuleni, nawiwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa hotuba zake na ujenzi wa taifa anaoufanya, ila pia nitamshauri sehemu ninayoamini anapaswa kurekebisha kidogo.

Sitanii, kwa tuliokuwapo tunakumbuka Mwalimu Nyerere alivyoanzisha mashirika ya umma. Tanzania ya enzi za Mwalimu Nyerere ilikuwa na viwanda vya nguo. Tunakumbuka viwanda kama Mwatex, Mutex, Kilitex, Urafiki, Sunguratex… tulikuwa na kiwanda cha viatu cha Bora.

Nchi yetu ilikuwa na kiwanda cha kutengeneza betri na radio cha National, kiwanda cha kutengeneza sabuni cha Ilula, siagi ya mikate ya Tanbond, vitanda vya chuma vya Banco, kiwanda cha baiskeli za Swala, kiwanda cha Bia cha Tanzania na viwanda vingine vingi vikiwamo vya saruji.

Kwa bahati mbaya, hapo katikati viongozi waliofuatia baada ya Mwalimu Nyerere walikumbana na masharti magumu wakacheza ngoma ya Wazungu. Mzee Ali Hassan Mwinyi, alibanwa mbavu akakubali masharti ya Benki ya Dunia na IMF yaliyofahamika kama Structural Adjustment Program (SAPs), akapunguza wafanyakazi.

Benjamin Mkapa akaingia na sera ya ubinafsishaji, ambapo alianzisha kazi ya kubinafsisha hadi migodi kama Kiwira na mingine, ambapo zaidi ya mashirika 400 aliyoyaanzisha Mwalimu Nyerere aliyabinafsisha au kuanzisha mchakato wake wa kubinafsishwa.

Jakaya Kikwete yeye alipoingia madarakani akakuta nchi ina fedha na inapendwa na wafadhili, basi akaanza kupokea misaada. Alipata msaada mkubwa wa Millennium Challenge Corporation (MCC) ambapo Marekani iliipatia Tanzania msaada wa dola milioni 698.1, sawa na Sh trilioni 1.6.

Ukiangalia kiwango cha kuwanyenyekea watoa fedha hizi na masharti waliyokuwa wanatupa, unaona heri kufa maskini kuliko utajiri wa masimango. Kiasi hiki kilitufanya kubadili sheria zetu nyingi tuweze kupata msaada huu. Hii imenikumbusha maneno ya Mwalimu Nyerere: “Serikali zinazokula rushwa hazikusanyi kodi.” Sh tirilioni 1.6, kwa sasa Rais Magufuli anazikusanya ndani ya mwezi mmoja. Kwa nini nisimpongeze?

Sitanii, hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kuwa na viwanda. Tulifika mahala tukawekeza katika kuomba misaada badala ya kujenga uchumi wetu kwa njia ya kujenga viwanda, wafanyabiashara wakalipa kodi, kodi ikajenga miundombinu kama reli, barabara, shule, hospitali, umeme wa uhakika, viwanja vya ndege, tukanunua ndege na mengine mengi anayofanya Rais Magufuli. Hivi kwa nini nisimpongeze Rais Magufuli kwa haya anayoyafanya?

Mwanzoni sikumwelewa Rais Magufuli. Niliona kama ana chuki na wafanyabiashara, ila sasa nimemwelewa. Hatua ya kuwazuia TRA kufunga biashara badala yake kama mtu anadaiwa kodi wakae wajadiliane jinsi atakavyoilipa ni mapinduzi makubwa katika uchumi wa viwanda na biashara kwa ujumla. Kudai au kudaiwa ni jambo la kawaida. Ukifunga biashara ya mtu, ni wazi hata kodi unayodai umeifunga!

Mazuri yapo mengi, ila nirejee katika machache ninayodhani Rais Magufuli anapaswa kulegeza kamba au kubadilika kabisa. La kwanza ni uhuru wa watu kutoa mawazo. Kwa kweli yeye anaonekana ‘live’ kwenye televisheni kutoka kila kona ya nchi, ila serikali yake ikazuia Bunge ‘live’, hili linatia doa uongozi wake.

Sitanii, kila mara analalamika kuwa kazi anayoifanya ni ngumu, na kweli ni ngumu na ninampa pole, ila anaweza kuifanya iwe rahisi akipenda. Aruhusu vyama vya upinzani kutoa mawazo yao, wamuonyesha penye matundu, badala ya kudhani ni wasaliti na mawakala wa mabeberu muda wote!

Anasema hana uhakika akiacha urais kama kazi hizi zitaendelezwa. Hapo ndipo ninamwambia, badala ya kusimamia kwa mfumo unaoitwa Management By Walking Around (Uongozi wa Kuwapo Kila Mahala), abadili mfumo, atunge sheria zimwezeshe kutumia mfumo wa Management By Objectives (Uongozi wa Malengo).

Mwenzake Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alilijua siku nyingi hili ndiyo maana anatumia mfumo unaoitwa IMIHIGO. Anaingia mikataba na mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya yenye malengo mahususi ya kutekeleza. Akikutana nao anahoji wametimiza malengo kiasi gani, anayeshindwa anamtumbua. Nashauri rais ukijenga mfumo wa aina hii, vituo vyote vitakwenda kilaini.

Hata hivyo, kwa nchi ilipokuwa, hasa hili la kukataa umaskini kwamba nchi yetu Tanzania si maskini ni tajiri, naomba ukubaliane nami nimwombe ruhusa Mwalimu Nyerere nikupongeze kwa mambo mazuri unayolifanyia taifa letu likiwamo hili la kukataa umaskini, na niseme historia itakukumbuka. Hakika, huko Nyerere aliko ninajua anafarijika kwa kazi yako. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri