Napenda kuchukua fursa hii kumpa pole Rais Jakaya Kikwete kwa majukumu mazito yanayomkabili kwenye uendeshaji wa Serikali, kutokana na mikinzano na vitisho anavyopata kutoka kwa baadhi ya wabunge na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Simpi pole kwa kuwa anafanya kazi ya urais, la hasha, kufanya kazi ya urais ni jukumu lake kama alivyowaomba Watanzania kupitia kampeni zake za mwaka 2005 na 2010.

Tuko kwenye mchakato muhimu na adhimu kwa mustakabali wa nchi yetu, mchakato unaoenda kuamua Tanzania ya miaka 50 au 100 na vizazi vijavyo.

Mchakato huo unakwenda kujenga misingi mipya ya ujenzi wa Tanzania imara kuliko hii tuliyokuwa nayo sasa,  mchakato ambao kwa mara ya kwanza unawashirikisha Watanzania kwa makundi tofauti bila kujali itikadi zao na maeneo waliyotoka, namuomba Rais Kikwete asimame imara na kuwa rais na asiwe mrahisi kwenye huu mchakato muhimu wa kuipatia Tanzania Katiba mpya na bora.

Nimeamua kusema haya kwa nia njema na upendo kwa Taifa langu, nikitambua kuwa hii ni fursa adhimu kwa Rais Kikwete kwenda kuandika historia mpya kwa Taifa hili.

Kama ataweza kuliacha likiwa salama bila mivurugano na bila machafuko ambayo yanaweza kumgharimu mara baada ya kumaliza kipindi chake cha urais na hatimaye kujikuta akiwa mbele ya Mahakama akijibu tuhuma za kuiingiza nchi yake kwenye machafuko.

Baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali pamoja na baadhi ya wabunge wa chama ambacho rais ni mwenyekiti wake, wamejitokeza mara kadhaa mbele ya vyombo vya habari na tumewashuhudia hata kupitia bungeni, wakitoa kauli tata na zenye kuacha ‘sintofahamu’ kwa mustakabali mwema wa nchi, zikiashiria kukwaza mchakato wa kupata Katiba mpya na bora kwa mustakabali mwema wa nchi yetu.

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alishawahi kusema kuwa Tanzania haihitaji Katiba mpya, akafuatiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ambaye naye hakuona umuhimu wa kuwa na Katiba mpya.

Baadaye rais alikubaliana na nguvu ya wapinzani na kuona kuwa ni busara kutengeneza Katiba mpya, japo haikuwa kwenye moja ya sera kwenye Ilani ya CCM.

Kwa Mwanasheria Mkuu, pamoja na rais kukubali kuanzishwa mchakato wa Katiba mpya, lakini bado yeye amekuwa anaonekana dhahiri kuwa hayuko tayari kuona Tanzania inapata Katiba mpya, kutokana na aina ya miswaada tata aliyoshiriki kuitengeneza inapopelekwa bungeni.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, naye hana tofauti na mtangulizi wake. Yeye amekwenda mbali zaidi hadi kumtishia rais kwa kusema eti rais asiposaini muswaada atakuwa anatengeneza mgogoro na Bunge huku Waziri wa Uhusiano, Stephen Wasira, akiwananga wapinzani kuwa Ikulu imefunga milango na haina tena bajeti ya juisi kwa ajili ya wapinzani.

Mawaziri hawa hawakuona umuhimu wa hoja zilizokuwa zinapiganiwa na upinzani ziingizwe kwenye sheria ya marekebisho ya muswaada wa Katiba, wao waliangalia mambo yasiyokuwa na tija na kuonekana kulinda maslahi ya chama badala ya kuangalia kwa upana wa kipekee maslahi ya Taifa.

Kama rais ataamua kuwa mrahisi na kuwasikiliza viongozi aina ya Chikawe, Celina Kombani, Wassira, Jaji Werema na wengine ndani ya CCM aina ya Kigwangwalah na Lusinde.

Viongozi hawa wamewahi kunukuliwa wakisema kuwa Katiba si muhimu kama maji na barabara, nachelea kusema kuwa atalitumbukiza Taifa hili kwenye machafuko yasiyokuwa na sababu.

Kwani kauli na matendo yao haviashirii kulivusha Taifa hili kwenda salama kwenye huu mchakato na fursa adhimu yenye umuhimu wa kipekee, wa kulipatia Taifa Katiba mpya na bora kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Namuomba rais asiwe mrahisi, tena ikiwezekana kwa maslahi ya nchi awe tayari hata kuvunja Bunge kama wabunge wa CCM wataendelea kukwaza au kugomea mambo muhimu yaliyoko kwenye sheria ya mabadiliko ya mchakato huu.

Muhimu kwa nchi yetu, asiogope wala kuwaonea haya maana wanaonekana kabisa kuwa nia yao si njema kwani wanajali maslahi binafsi na vyama vyao, na nchi ikiingia kwenye machafuko atakayekuwa wa kwanza kunyooshewa kidole na kuwajibishwa atakuwa ni yeye.

Natambua kuwa CCM wanaogopa uchaguzi kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha upinzani, ikibidi kwa maslahi ya nchi hii, JK awe rais na kuchukua uamuzi mgumu wa kuvunja Bunge ili sisi wananchi tuamue upya tunayemtaka aingie bungeni.

Kwenye mchakato huu muhimu wa kupata Katiba mpya, bora na yenye kujali maslahi mapana ya Tanzania na si maslahi binafsi, ni wakati wa JK kuwaonesha wana-CCM wenzake kuwa yeye ni rais na si mrahisi japo baadhi ya wana-CCM wasiolitakia mema Taifa hili hawapendi kuona anakubaliana na hoja za wapinzani na kuachana na baadhi ya hoja muflisi za wana-CCM wenzake.

1329 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!