Uongozi Wetu na  Hatima ya Tanzania (4)

Huu ni mtiririko wa maandishi yaliyomo kwenye kitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1994. Sehemu iliyopita, Mwalimu alisema, “Kwa kweli hata kesho Nchi za Afrika ya Mashariki zikiamua kuungana, na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali Mbili – ya Zanzibar na ya Tanganyika – kuliko Tanzania yenye Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar. Wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa Nchi Moja, kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.” Endelea…..

Siku ya pili yake tarehe 15:8:1993, Wabunge wenye hoja yao, na wengine zaidi, waliomba tena kuja Msasani ‘Tunywe chai’. Na baada ya mazungumzo nao ilikuwa ni dhahiri kabisa kwangu, kwamba hata kama hawakuondoa hoja yao, (wala mimi sikuwaomba waiondoe), wataitumia kutoa dukuduku zao tu; hawataitumia kung’ang’ania kudai Serikali ya Tanganyika.

 

Kwa hiyo sikushangaa baadaye niliposikia kuwa waliiondoa hoja yao ya awali, na badala yake wakaleta hoja ya kutafuta maoni ya wananchi.

 

Mimi kwa upande wangu nilihisi kuwa hoja mpya hii ilikuwa na shabaha ileile ya “kunawa uso”, kama Zanzibar kusema kuwa wanatoka katika OIC, lakini utafanywa uchunguzi wa kuona kama Tanzania inaweza kuingia katika OIC.

 

Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar, wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendumu Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa, kwa sababu safi kabisa. Maoni haya ya Wabunge wa Bara, ambao mimi naamini kabisa si wapinzani wa Muungano, nayo yangeweza kukataliwa na Chama na Serikali, kwa sababu zile zile na mambo yakesha.

II SERIKALI INASARENDA

Baadaye, nadhani siku iliyofuatia, niliitisha kikao cha Watangazaji wa Habari, nikapinga kwa kirefu hoja ya Utanganyika. Wakati naondoka Dar es Salaam ili kurudi Butiama, nilitumaini kabisa kwamba Serikali itaeendeleza Bungeni, na kama hapana budi nchini, kazi tuliyoanza pamoja, ya kupinga hoja Serikali tatu. Sikuwa na sababu yoyote ya kuhofia kuwa siku chache tu baadaye Serikali itageuza msimamo wake na kufanya “abautani”.


Sijui lililotokea, maana kila nilipouliza sikupata maelezo. Kama nilivyokwisha kusema hapo nyuma baadaye wabunge wahusika waliiondoa hoja yao ya awali ya kutaka Bunge lipitishe azimio la kudai Serikali Tatu, wakaleta hoja mpya ya kutaka Serikali ifanye referendamu ya kutafuta maoni ya wananchi kuhusu suala hili. Nasema, Serikali ingeweza kuikataa hoja hii kwa maelezo safi kabisa na mambo yakesha Au kama wangeona kuwa si siasa nzuri kuipinga hoja hii nayo, wangeweza kuikubali, na mimi nina hakika, wananchi wangeikataa na mambo yakesha.


Lakini Serikali ya Muungano, bila maelezo ilikataa hoja mpya ya Wabunge ya kutaka maoni ya wananchi, na yenyewe ndiyo ikafufua hoja ya Utanganyika, na kupendekeza kwamba badala ya hoja ya Serikali Tatu kujadiliwa Bungeni na kupigiwa kura, Bunge zima, pamoja na Serikali yenyewe, likubali hoja hiyo, bila mjadala!


Kumbe jambo ambalo viongozi wetu walikuwa wanahofu kabisa kabisa ni mjadala, maana huo ungewalazimisha kujitambulisha kama si katika mjadala wenyewe, basi wakati wa kupiga kura, hasa ikiwa ni kura ya kuita mbunge mmoja mmoja kwa jina, pamoja na Mawaziri wetu! Badala ya kupita katika adha hiyo wakaona afadhali wakubali Serikali Tatu, bila ya mjadala. Basi Serikali yetu ikanywea ghafla tu, kama mpira uliotoboka au puto lililopasuka. Nadhani hata wabunge wenye hoja ya awali walishangaa!


Kuongoza ni kuonyesha njia. Viongozi wetu walikuwa Wametumwa na chama chao waende bungeni, Bunge la wanachama watupu wa CCM wakawaonyeshe njia.


Wakawaambie wabunge wahusika kwamba hoja yao ya kutaka Serikali Tatu ni kinyume cha sera ya chama chao, na ina hatari ya kuigawa na kuiangamiza Nchi yetu.


Waliagizwa wazi wazi wakaipinge hoja hiyo. Wakapata mtihani mdogo sana Bungeni. Wakasarenda. Wakatupa silaha chini; wakasalimu amri. Viongozi hawa hawawezi kusimama mbele ya Kamati Kuu, au mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa kusema kwa fahari kama wao ni hodari: Kazi mliyotutuma tumeikamilisha! Wala hawataki kukubali matokeo ya kusarenda kwao.


Kwa sababu uamuzi wa kutaka Serikali ya Tanganyika ‘ndani ya muungano’ ulifanywa na viongozi wetu kwa hila, na kupitishwa Bungeni bila mjadala, sisi wengine hatukujua lililotokea. Baadaye tulifahamishwa kuwa huo ndiyo ulikuwa uamuzi wa “Bunge zima” kutokana na kauli ya Mheshimiwa Pius Msekwa aliyekuwa msimamizi wa kikao cha Bunge kilichofikia uamuzi huo.


Nadhani viongozi wetu walitaka kuendelea kuficha na kuuvuga vuga, lakini yeye akatoboa. Nasikia baadaye aliitwa akakemewa. Sijui kwa nini.

DODOMA II 14:10:I993

Nilipokwisha kuhakikishiwa kuwa sasa sera ya Serikali Tatu ndiyo sera rasmi ya Bunge la Muungano na Serikali ya Muungano, nilijaribu kupata maelezo kutoka kwa viongozi wetu; lakini sikufanikiwa.


Waziri Mkuu nilipomuuliza kama kweli wamebadili sera, alicheka tu! Nilikuwa na safari ya kutembelea nchi za Asia kwa ajili ya shughuli zinazotokana na uenyekiti wangu wa Tume Nchi za Kusini.


Niliporudi kutoka safari nilijaribu tena kuonana na viongozi wetu ili nipate maelezo. Lakini sikufanikiwa kumpata kiongozi yeyote mhusika.


Nilipopata habari kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana Dodoma ,  nilihisi kuwa bila shaka viongozi wetu wataeleza kwa nini wameacha msimamo wa Chama na maagizo ya Kamati Kuu ya kupinga hoja ya Utanganyika, wakaamua kukubali hoja hiyo.


Basi nikaomba angalau nipatiwe nafasi nihudhurie kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Taifa, ili nami nisikie maelezo watakayotoa.


Baada ya maajabu ambayo haina maana kuyaeleza, nilikubaliwa nikaenda Dodoma.

KIKAO CHA FARAGHA

Safari hii tulikuwa na vikao viwili. Kwanza kikao cha faragha wakiwapo Viongozi Wakuu wote wa Chama na Serikali, na wengine wa nyongeza.


Kilikuwa kikao kirefu na kigumu. Sina kawaida ya kulizwa na mambo ya siasa, lakini katika kikao hiki nilishindwa kujizuia kulia.


Sikupata maelezo ya maana ya kuwafanya watu wazima wafanye walivyofanya. Nilipouliza kwa nini hawakupinga hoja ya Serikali Tatu kama tulivyokuwa tumekubaliana, majibu ya viongozi wetu Wakuu yalikuwa ni ya ajabu kabisa.


Ati Wabunge wenye hoja baada ya kuonana na mimi Msasani walikwenda Bungeni wakiwa wakali kama mbogo! Tena walikuwa wakiwatukana wenzao (yaani Wabunge wa Zanzibar ), kwa kuwataja majina.


Hizi ni sababu za ajabu sana za kuwafanya viongozi watu wazima watekeleze msimamo mzima wa Chama chao na makubaliano ya watu makini kuutetea msimamo huo, na waamue kuikumbatia hoja ya mbogo wakali!


Huu ni uongozi wa ajabu kabisa! Nilipowabana zaidi niliahidiwa kuwa maelezo mazuri yatatolewa kesho yake na Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa.

KIKAO CHA HALMASHAURI KUU:

Hakika siku ya pili yake waligawiwa ‘TAARIFA YA SERIKALI JUU YA AZIMIO LA BUNGE KUHUSU HAJA YA KUUNDA SERIKALI YA TANGANYIKA NDANI YA MUUNDO WA MUUNGANO’. Taarifa yenyewe ni ndefu ina maelezo mengine ya mapambo tu, au ya kiini macho. Lakini vipengele vinavyohusika na suala lenyewe vilikuwa vichache na nimevinukuu kwa ukamilifu (tazama kisanduku 2)

 

“9 Tarehe 30 Julai, 1993 wakati wa mkutano wa Bunge la Bajeti ukiendelea, zaidi ya Wabunge 50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai, miongoni mwa mambo mengine;


KWA KUWA kuendelea mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea na kudumu kwa Muungano na pia kuathiri uelewano kati ya watu pande zote mbili; na ………………..

 

KWA KUWA uwezekano wa kuunda Serikali moja ya Jamhuri ya Muungano kwa nchi nzima kwa mambo yote haujajionyesha; …………………..


HIVYO BASI Wabunge hawa wanaliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano katika Mkutano wake wa kumi na mbili unaofanyika Dar es Salaam liazimie kwamba;  Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilete Muswada Bungeni, kabla ya Februari 1994, kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muungano.


Tarehe 12 Agosti, 1993 hotuba ya Kuwasilisha Makadirio ya Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba ilisomwa Bungeni.


Katika hotuba hiyo, Serikali ilieleza kusudio la kuanda waraka wa Serikali (White Paper) kutafuta maoni ya wananchi kuhusu muundo wa Muungano.


Tarehe 20 Agosti, 1993 Wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine inayobadilisha ile hoja ya awali iliyosambazwa kwa Wabunge wote.


Hoja mpya ilikuwa inalitaka Bunge liazimie kwamba:

Serikali ya Jamhuri ya Muungano iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa Muungano utakaozingatia mabadiliko hayo.


Kutokana na taarifa hizi, Baraza la Mawaziri lilifanya kikao cha dharura ili kutafakari taarifa hizi na athari zake kama zingewasilishwa Bungeni na kupigia kura.


Kwanza kabisa, inaonekana kwamba hoja ya awali ingekuwa vigumu kutekelezeka kutokana na muda mfupi uliowekwa kufikia Februari, 1994, na pia haikutoa fursa kupata maelekezo ya Chama wala Serikali zetu mbili kushauriana.

 

Itaendelea

 

By Jamhuri