Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amewataka wote wanaoendesha shughuli za kilimo na ufugaji katika misitu ya Ruvu Kusini na Kazimzumbwi wilayani humo kuondoka mara moja kabla hajatumia nguvu.

Jokate ametoa agizo hilo leo Agosti 7 akiwa kwenye msitu wa Ruvu Kusini ambako alienda na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na maofisa wa Wakala wa Misitu ( TFS) kwa ajili ya kuwaondoa wavamizi waliopo humo.

Akiwa ndani ya msitu wa Ruvu Kusini Jokate amezindua operesheni ya kuwaondoa wavamizi na kuipa jila la “Operesheni Jokate”.

Amesema lengo lake ni kuwasaka na kuwaondoa wavamizi ambao hawataki kufuata sheria na utaratibu wa hifadhi ya misitu katika msitu wa Ruvu Kusini uliopo wilayani humo.

Jokate amesema operesheni hiyo ni ya siku sita na imeanza leo Agosti 7 ambapo katika siku ya kwanza ng’ombe zaidi ya 150 walikamatwa ndani ya msitu huo na zoezi la kuwakamata wamiliki wake linaendelea.

“Kwa kuanza na utekelezaji wa maagizo ya mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo nimeamua nianze msitu huu wa Ruvu Kusini baada ya kupata dondoo ya kuwepo wavamizi,” amesema.

Amesema atahakikisha anasimamia na kuona kazi hii inakwenda vizuri na misitu yote inaendelea kulindwa na kuwa katika hali nzuri.

Amewataka wakazi wanaoishi maeneo ya jirani na msitu huo kuheshimu mipaka na taratibu zilizopo ili kuepuka kuingia kwenye mkono wa sheria.

Kwa upande wake, Meneja wa TFS Kanda ya Mashariki, Caroline Makundo amesema msitu huo umevamiwa kwa shughuli za kilimo na ufugaji kwa maaana ya mifugo kuingizwa humo na kwamba kazi ya kuwasaka wavamizi itafanyika usiku na mchana kwa siku hizo sita.

Please follow and like us:
Pin Share