Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetoa siku saba kwa wananchi wote ambao wana nguo ama mavazi ya kijeshi,kuyawasilisha katika Makambi ya Jeshi,Vituo vya Polisi au katika Ofisi za Serikali za Mitaa na atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.

Luteni Kanali Gaudentius Ilonda ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Habari na uhusiano Makao makuu ya Jeshi (JWTZ) amateoa taarifa hiyo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo amesema hivi sasa kumekuwa na kadhia kubwa ya uvaliwaji wa sare hizo ikiwemo tasisi jambo ambalo linahatarisha Usalama wa Nchi.

Katika hatua nyingine,Luteni Ilonda amesema kuwa wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mavazi hao kutapeli wananchi na wengine kufanya vitendo viovu ambao wamekuwa wakidhaniwa kuwa ni wannajeahi vitendo ambavyo ni uvunjifu wa sheria.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ametoa angalizo kwa wazazi kuwa makini na watoto wao kuhusiana na mavazi hayo.

Ikumbukwe kuwa katazo hilo ni kwa mujibu wa kifungu Cha 99 Cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa ( NDA) Sura ya 192,Sheria namba 24 ya Mwaka 1996 iliyofanyiwa marejeo Mwaka 2002.

By Jamhuri