Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mlinda lango namba moja wa klabu ya Singida Black Stars, Beno Kakolanya anadaiwa kutoroka kambini saa chache kabla ya mechi yao dhidi ya Yanga iliyochezwa jana katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisa habari wa Singida BS, Hussein Massanza baada ya mechi amesema Kakolanya aliomba ruhusa kwa uongozi ya kuondoka kambini lakini aliambiwa aondoke baada ya mechi hiyo, amekaidi na kuamua kuondoka.

“Kwa sasa zipo tuhuma ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi, yapo madai ya uhujumu katika mechi hii yalikuwa yanafanyika, kamati ya nidhamu inaendelea kuyashughulikia ikikamilisha ripoti yake tutawafahamisha.

“Beno Kakolanya ni golikipa namba moja katika kikosi chetu ni nahodha pia, sio mchezaji wa kawaida, ni mchezaji kiongozi na mwenye uzoefu wa mechi kubwa kama hii ya Yanga, ni kipa ambaye anaitwa mara nyingi timu ya taifa anategemewa.

“Hatukutarajia kuona yeye kwa uzoefu wake akafanye vitu kama hivyo, tumesikitika kama timu, lakini tutachukua hatua za kinidhamu na kuhakikisha kwamba mambo kama haya hayajitokezi tena, lazima ifikie hatua wachezaji waheshimu mikataba na vilabu vyao ili tuweze kufanya kazi kwa kuheshimiana”, amesema Massanza

Mchezo huo ulimalizika kwa Yanga kuvuna alama tatu baada ya Singida BS kuruhusu kichapo cha mabao matatu yaliyofungwa na mawili Joseph Guede na moja Aziz Ki.

Beno kakolanya amewahi kuwa na skendo kama hii ya kutoroka kambini akiwa anaichezea Yanga miaka mitano iliyopita, ambapo baadae alionekana akitambulishwa Simba sc.

By Jamhuri