Kama umemsahau Mungu, umejisahau mwenyewe (1)

Nakukumbusha: Kama umemsahau Mungu; basi umejisahau wewe mwenyewe.  Sizijui funguo zote za mafanikio, lakini ninaufahamu ufunguo mmoja wa kushindwa. Ufunguo huo ni: ‘Kuishi bila Mungu’. Kuishi bila Mungu ni kupotea njia. Ni  kupoteza ufunguo wa mafanikio katika maisha. Unapomtafuta Mungu na Mungu anakutafuta.  Unapomsahau Mungu na Mungu anakusahau.

Padri Dk. Faustine Kamugisha anatufundisha kwamba: “Mungu bila binadamu ni Mungu, binadamu bila Mungu si chochote.” Jitahidi kuishi maisha ya sala ili maisha yako yawe mwanga kwa walio gizani, yawe faraja kwa walio na huzuni, yawe tumaini kwa waliokata tamaa, yawe upendo kwa walio na chuki na yawe njia kwa wasio na njia.

Kuna mchungaji  mmoja alikuwa anataniana na tajiri ambaye hakuwahi kuonekana kanisani hata mara moja. Tajiri alimwambia mchungaji: “Jinsi ulivyo mtu wa Mungu ukienda motoni nitashangaa sana.” Mchungaji naye akamwambia tajiri: “Wewe usivyokanyaga kanisani ukienda mbinguni nitashangaa sana.” Sisi sote tulio dhaifu kiroho, kimwili, kiakili, kiutashi na kimapendo tunahitaji huruma ya Mungu. Tunahitaji huruma ya Mungu ili maisha yetu na matendo yetu yaongozwe na tabia ya upendo. Lengo letu la kwanza katika maisha ni kuwasaidia wengine, kama hatuwezi kuwasaidia wengine basi tusiwaumize.

Fumbua macho yako utazame. Tazama upya mahusiano yako na Mungu wako. Tazama upya mahusiano yako na mke/mume wako. Tazama upya mahusiano yako na watoto wako. Tazama upya mahusiano yako na jirani zako. Tazama upya uhusiano wako na kazi yako. Tazama upya mahusiano yako na wafanyakazi wenzako.

Naomba nipate nafasi ya kukushauri katika makala hii. Usikubali siku ipite bila ya kusoma Maandiko Matakatifu. Maandiko Matakatifu yanapaswa kuwa sehemu ya maisha yako.

Neno la Mungu ni lishe ya kiroho. Mfalme Daudi anasema: “Neno lako ni taa ya miguu yangu.” (Zab 119, 118, 105). Mwanateolojia Gregory Mkuu anafundisha kuwa: “Maandiko Matakatifu yanakaa mbele yetu kama kioo ili kwamba kupitia yenyewe tuweze kuiona sura yetu ya ndani, tugundue ubaya wetu na uzuri wetu, tugundue hatua tulizopiga na mwendo ulio bado mbele yetu.” Unaposoma Maandiko Matakatifu kwa usikivu na utulivu mwanana unakutana na uwepo wa Yesu Kristo katika kurasa za Maandiko Matakatifu.

Maandiko Matakatifu lazima yawe kwako kama mahali pa kukutana na Yesu ambaye amekupenda mpaka mwisho na anatarajia kujenga sura yake ndani yako. Kwa kusoma Maandiko Matakatifu unajenga sura ya kweli ya Mungu ndani mwako. Mwanateolojia na Mwalimu wa Kanisa Katoliki, Mt. Jerome anasema: “Asiyeyajua Maandiko Matakatifu, hajui pia hekima ya Mungu.”

Maisha yako kama Mkristo yanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa katika familia, kanisa, jamii na taifa. Unabaki kuwa ukweli usiopingika kuwa hakuna namna nzuri ya kumshawishi mtu juu ya uzuri wa kitu chochote zaidi ya kuonyesha katika matendo.

Kusali kila wakati ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika Maisha. Mwandishi Robinson Maria anasema: “Hakuna anayeweza kurudi nyuma na kuanza mwanzo mpya, lakini yeyote anaweza  kuanza leo na kutengeneza  mwisho mpya.” Kila tunaposali tunatengeneza mwanzo mpya wa maisha yetu. Kila tunaposali  kwa unyenyekevu na utii tunajenga mahusiano yaliyo imara kati yetu na Muumba wetu.

Una nafasi kubwa ya kubadilisha historia ya maisha yako kila unapokutana na Yesu kwa njia ya sala. Mwanafalsafa Soren Kierkegaard (1813-1855) anasema: “Sala haimbadili Mungu, bali inambadili yule anayeisali.” Kila unaposali unaikarabati roho yako. Unaipaka mafuta matakatifu. Kama vile ambavyo tukikaa karibu zaidi na moto tunapata joto zaidi, kadhalika aliyekaribu zaidi na Mungu anapata utakatifu zaidi. Kama unataka baraka za Mungu katika maisha yako na unataka kujulikana kama mtoto wa Mungu ni lazima uwe mtu wa sala.

Mwenyezi Mungu ni rafiki wa kweli katika maisha yetu  ya kila  siku. Anatulinda. Anatupenda. Anatubariki. Anatuongoza katika njia  iliyo takatifu. Tukumbuke  jambo moja  ambalo ni la muhimu sana. Hatuwezi kufanikiwa kiroho, kimwili, kiuchumi, kimaadili, kifamilia, kama hatumtazami Mwenyezi  Mungu kama rafiki yetu mwema na Muumba wetu.

Yesu Kristo aliwaonyesha wanafunzi wake upendo wake kwao kwa kuwaita rafiki. Tunasoma hivi katika Maandiko Matakatifu: “Siwaiti tena watumwa, kwa sababu mtumwa hajui kazi za Bwana wake. Badala yake ninawaita rafiki, kwa kuwa nilichojifunza kwa baba yangu nimewajulisha.” (Yoh. 15:15).  Huu ni urafiki usioweza kuelezeka kwa maneno ya kibinadamu bali kwa upendo wa Kimungu tu. Yesu Kristo ni rafiki yetu. Ni kaka yetu. Ni mkombozi wetu.