Arobaini ni mwarubaini (1)

Wakatoliki pote duniani wameanza kipindi cha kufunga siku arobaini. Kipindi hiki kinaitwa Kwaresima na kinafunguliwa rasmi kwa kupakwa majivu kwenye paji la uso. Ni kipindi cha kufanya toba, kufunga, kusali na kutenda matendo ya huruma.

Siku arobaini zinaunganishwa na siku arobaini ambazo Bwana Yesu alishinda jangwani akifunga. Tunasoma hivi katika Biblia: “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku.” (Mathayo 4: 1-2).

Bwana Yesu Kristo alikuwa anajiandaa kuanza kazi yake rasmi. Siku arobaini ni ishara ya kipindi cha majaribu, majaribio na taabu. Siku arobaini ni kipindi cha maandalizi. Kujiandaa ni kujiandaa kushinda.

Namba arobaini inakutwa katika methali na misemo mbalimbali. Maisha yanaanza kwenye mwaka wa arobaini. Ni msemo wa Waingereza. Unapofikia miaka arobaini unafikia kipindi cha mapumziko cha mchezo wa maisha. Unatoka kwenye mafanikio kwenda kwenye kuacha alama. “Kuwaelewa watu lazima kuishi nao siku arobaini.” (Methali ya Waarabu). Namba arobaini imetajwa mara 146 kwenye Biblia.

Arobaini ni kipindi cha somo la unyenyekevu kwa wana wa Israeli.  Waisraeli walizunguka miaka 40 kabla ya kuingia nchi ya ahadi. “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako.” (Kumbukumbu la Torati 8: 2).

Musa alikuwa mlimani Sinai siku 40. “Musa aliingia ndani ya wingu. Akaupanda mlima, akashinda huko siku arobaini mchana na usiku.” (Kutoka 24:18). Bwana Yesu alifunga siku 40. Tangu ufufuko wa Yesu na kupaa kwake ni kipindi cha siku 40. Kwaresima ni siku arobaini.

Namba arobaini inapatikana kwa kuzidisha tano mara nane. Tano ni ishara ya neema ya Mungu. Ikizidishwa kwa yenyewe ni neema juu ya neema (Yn 1:16). Nane ni ishara ya mwanzo mpya. Kumaliza ni kuanza. Yesu alitahiriwa siku ya nane.

Arobaini ni kipindi cha muungano bora kati ya Mungu na watu wake kupitia kutoa. “Je, mlinitolea sadaka na matoleo jangwani muda wa miaka arobaini, ee nyumba ya Israeli?” (Amosi 5:25).

Kipindi cha siku arobaini ni kipindi cha ukarimu. Kufunga ni ukarimu. “Tunachoacha kwa kufunga kitolewe kama sadaka kwa maskini.” (Papa Leo I). Tuwe wakarimu kwa wasio wakarimu. “Tendo la ukarimu wa kiwango cha juu sana ni ukarimu kwa wasio wakarimu.” (Joseph B. Buckminster). Ukarimu unaona hitaji. “Hakuna barabara ya juu zaidi kuliko barabara ya ukarimu na ni wanyenyekevu tu hupitia barabara hiyo.” (Mt. Augustino). Kuna aliyemuuliza malaika: “Niendelee kutoa na kutoa mpaka lini?” Malaika alimjibu: “Mpaka hapo Mungu atakapoacha kukupa.” Kama ulikwishawahi kuwa mhitaji utafurahia utoaji. Kuwasaidia wale walio katika aina yoyote ya uhitaji ndiko kunafanya mfungo uwe wa kumpendeza Mungu.

Arobaini ni mwarubaini. Mwarubaini ni mti mchungu wenye matawi yaliyotanda, maua na majani madogo huaminiwa kufaa kutengeneza dawa za maradhi mbalimbali. Kanisa Katoliki husali kipindi cha siku arobaini. “Tunapofunga, unazuia vilema vyetu, unainua moyo wetu, unatujalia nguvu na tuzo; kwa njia ya Kristu Bwana wetu.” (Utangulizi, Kwaresima IV). Vilema saba vya dhambi ni: majivuno, uroho, uzinifu, hasira, ulafi, kijicho na uzembe. Kufunga kunasaidia kudhibiti vilema hivi. Kwa msingi huo arobaini ni mwarubaini.

Lengo la kufunga siku arobaini ni kumrudia Mungu. “Mungu anapotoweka, lengo linatoweka. Lengo linapotoweka, maana inatoweka, thamani inatoweka na maisha yanafia mikononi mwetu,” alisema Carl Jung. Kumrudia Bwana kunahitaji nidhamu ya kufunga, kusali na kuwasaidia maskini.

Mashujaa wa imani walijipaka majivu

Majivu ni salio la moto, makazi yake ni jalalani. Ila yakisugua sufuria yenye masizi huifanya itakate! Japo tu dhaifu, tuna thamani zaidi ya sufuria. Majivu ya leo yakutakase kiroho!

Huu ni ujumbe ambao nilipokea kwenye simu siku ya Jumatano ya Majivu Februari 22, 2012. Ni siku ambayo Wakatoliki walipakwa majivu. Kupakwa majivu ni kuanza kipindi cha kufunga, kutoa sadaka, kusali kwa ajili ya kufanya toba. Ni kipindi ambacho kinaitwa Kwaresima.

Ujumbe mwingine ambao niliupokea katika simu unabainisha ya kufanya katika kipindi hiki. Ujumbe huo ni: Ukitaka kujua salio la mema yako –  bonyeza Kwaresima, kuongeza salio – toa sadaka, huduma ya kuongea na Mungu – piga sala, kwa maelezo zaidi, kwaresima njema.