Wiki hii Bunge la 11 linakutana jijini Dodoma kwa ajili ya kuendelea na vikao vyake kama ilivyo ada.

Pamoja na changamoto za hapa na pale katika maisha ya Mtanzania, naamini bado Watanzania wanayo imani na Bunge hili.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ni kamati yenye jukumu kubwa nchini. Jukumu lake hasa ni kuhakikisha nchi na watu wake wote tunaendelea kuwa salama wakati wote.

Kutokana na majukumu ya Bunge nchini, kupitia Bunge hili na kamati hii, ni muda muafaka sasa kushughulikia kwa kina usalama wa raia na mali zao.

Maisha ya Mtanzania sasa yanaonekana kuwa shakani kutokana na kuibuka mtindo wa kutekana, ambao haukuwapo hapo awali.

Watanzania hatujazoea maisha ya kutekwa na kutekana. Tumezoea kuishi kwa upendo na amani, lakini sasa tumejikuta tukihamishiwa kwenye maisha ya hofu kila uchwao.

Kupitia kamati hii nyeti ya Bunge, vitendo hivi vya hovyo vitakoma iwapo itatekeleza wajibu wake ipasavyo. Naamini hili linawezekana.

Ikumbukwe mwenyekiti wa kamati hii ni miongoni mwa makachero wazuri waliokuwa viongozi wa Jeshi la Polisi nchini. Hili analiweza kwa kushirikiana na kamati yake.

Wabunge wetu wanatakiwa kukumbuka kuwa nchi yetu isipokuwa na ulinzi wa uhakika huku watu wake wakiishi maisha ya kuweweseka, huko bungeni hakutakalika pia.

Naamini kupitia Bunge hili, wabunge wetu watatafakari hatima ya usalama wa raia na mali zao, ikiwa ni pamoja na kukutana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kupata suluhisho la usalama wetu.

Tanzania ni nchi inayosifika kwa amani, hivyo ni jukumu letu sote kupitia kwa wawakilishi wetu kulinda tunu hii adhimu.

Vitendo vya utekaji na utekwaji vinaweza kuota mizizi iwapo havitachukuliwa hatua za makusudi, hivyo kuhatarisha usalama wetu.

Kamati hii ya Ulinzi na Usalama ina jukumu kubwa la kukaa na kutafakari kwa kina kuhusu usalama wa nchi yetu kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kamati hii nyeti inalo jukumu la kuketi na kutafakari tulipotoka kiusalama, tulipo na tunapoelekea kutokana na viashiria hivi vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na wahuni wachache wasioitakia mema nchi yetu.

Wahenga walisema: “Samaki mkunje angali mbichi.” Hivyo iwapo hatua za haraka na makusudi zisipochukuliwa tutajikuta tunaanza kuishi kwa kuuzoea uhalifu na wahalifu.

Ni jukumu letu sote kukataa nchi yetu pendwa kuvurugwa na wahuni wanaoamua kufanya vitendo vya kihuni na kuichafua bila huruma.

Tanzania italindwa na inalindwa na Watanzania, lakini pia inachafuliwa na Watanzania.

Nina imani kubwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama katika kukomesha mtindo huu wa hovyo ulioibuka nchini. Nina imani na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutetea masilahi ya nchi na watu wake.

Tusimame pamoja kusema sasa imetosha.

Please follow and like us:
Pin Share