π Yampongeza Rais Samia kutekeleza miradi inayoleta mageuzi ya kiuchumi
π Dkt. Mataragio asema mradi umefikia asilimia 39.2
π Tanzania kufaidika na shilingi trilioni 2.3 kipindi cha ujenzi na uendeshaji
π EACOP yawezesha manunuzi ya USD milioni 462
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti leo wamekagua utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika kituo kitakachotumika kupokea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda ambapo wameahidi kuzidi kuupa msukumo mradi huo wa kimkakati katika mageuzi ya kiuchumi.
Mara baada ya kukagua kituo hicho kilichopo Kata ya Chongoleani wilayani Tanga, Mkoa wa Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Oran Njeza amesema Kamati hiyo ambayo inasimamia mipango na uchumi wa nchi imeona mradi wa EACOP una umuhimu kiuchumi hivyo wataendelea kuupa msukumo mkubwa ili ukamilike kwa wakati.
Kamati hiyo imempongeza, Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mabadiliko ya kiuchumi anayoyafanya kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama wa EACOP ambayo inaendana na jinsi dunia inavyokwenda kwa sasa.
“Mradi mkubwa kama wa EACOP haukutegemewa kufanyika kwenye nchi za kiafrika lakini maono ya Viongozi Wakuu wa nchi Uganda na Tanzania yamepelekea mradi huu kufanyika ili kuwezesha mafuta sasa kusafirishwa kwa njia ya mabomba ambayo pia yanasaidia katika ulinzi wa mazingira.” Amesema Mhe. Njeza
Aidha, Kamati hiyo ya Bajeti imeitaka Wizara ya Nishati kuweka kipaumbele katika ujenzi wa mabomba yatakayosafirisha nishati za aina mbalimbali kama vile Gesi na Mafuta na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kituo cha usafirishaji wa nishati hizo barani Afrika.
Vilevile, Kamati imeliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza nguvu ya kuutangaza mradi huo ili wananchi wafahamu jinsi Serikali inavyoendelea kutekeleza miradi yake.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kuwa mradi wa EACOP unafaida mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo kutoa ajira takriban 900, kuongeza mzunguko wa fedha, kuongeza fursa za biashara ikiwemo katika kituo cha kupokelea, kuhifadhi na kusafirikisha mafuta kilichopo Chongoleani Tanga, kuuza rasilimali kama vile simenti na kupata mapato mbalimbali kupitia ushuru.
Ametilia mkazo masuala ya afya na usalama pahala pa kazi katika miradi mbalimbali nchini ambapo ameipongeza EACOP kwa kutekeleza suala hilo kwa ufanisi ambapo katika masaa zaidi milioni mbili waliyofanya kazi hakuna ajali iliyotokea kwenye maeneo yao ya kazi.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alisema mradi wa EACOP ni wa kielelezo na kimkakati kutokana na faida zake mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato ya nchi katika kipindi cha ujenzi na uendeshaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 2.3, kutoa ajira kwa watanzania ambapo mpaka leo umeajiri takriban wananchi 7,584 huku ajira hizo zikitarajiwa kuongezeka.
Aliongeza kuwa, kampuni 146 za kitanzania zimehusika kutoa huduma mbalimbali kwenye mradi na kunufaika kwa takriban Dola za Kimarekani milioni 246 na pia mradi umepelekea kufanyika kwa manunuzi ya Dola za Marekani milioni 462 pamoja na vijana wa kitanzania kupata mafunzo ya teknolojia mbalimbali ambapo ujuzi huo watautumia kwenye miradi mingine ya ujenzi wa mabomba kuelekea mbalimbali kama Kenya na Zambia.
Alitaja wanahisa wa mradi huo kuwa ni Kampuni ya Total Energies ya Ufaransa (62%), CNOOC ya China (8%), Kampuni ya Mafuta ya Uganda (15%) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (15%).
Alisema, kwa ujumla mradi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 39.2 huku baadhi ya kazi zikikamilika kwa asilimia 100 ambapo ujenzi wa kiwanda cha kuwekea mabomba mfumo wa kuhifadhi joto cha Sojo ukifikia asilimia 90 na katika eneo la Chongoleani mradi umefikia asilimia takriban 40 na kueleza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2026.
Alieleza kuwa, Serikali inashirikiana vizuri na wanahisa wengine kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na Serikali ya Tanzania imekamilisha kuchangia mtaji wake kama mwanahisa ambapo mpaka leo Serikali imechangia Dola za Marekani milioni 308 ambayo ni sawa na asilimia 100 ya kiwango ambacho ni cha awali cha gharama za ujenzi kwa asilimia 15 ya hisa za Tanzania.
Kuhusu utwaaji wa ardhi ya mkuza wa EACOP kwa upande wa Tanzania alisema kuwa imekamilika kwa asilimia 99.2 na asilimia iliyobaki inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo masuala ya mirathi. Amesema kuwa kwa upande wa Uganda mradi huo pia unaendelea vizuri.