Yapongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi wa Maji uliojengwa eneo la Butimba Wilayani Nyamagana mkoani Mwanza unaozalisha kiasi cha lita milioni 48 kwa siku.

Hayo yamedhihirishwa Januari 8, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Daniel Sillo (Mb) wakati wa ziara ya kukagua hatua ya utekelezwaji wa mradi huo.

“Kamati imeridhishwa na mradi huu wa maji na tunatoa pongezi kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani, tumejionea namna mradi huu ulivyotekelezwa umezingatia viwango vyote vya ubora,” amesema.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikishuhudia hatua za uchujaji wa maji wakati wa ziara kwenye mtambo wa kuzalisha maji wa Butimba, Jijini Mwanza

Sillo amesisitiza kuwa Kamati haitokuwa kikwazo katika upatikanaji wa fedha ili miradi mingi itekelezwe na ikamilike kwa ubora na kwa wakati hasa ikizingatiwa kuwa jukumu lake la msingi ni kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi

Katika ziara hiyo, Kamati imeielekeza Wizara ya Maji kuhakikisha inaendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa miradi ya maji kote nchini ili dhamira ya Rasi. Dkt. Samia Suluhu Hassan itimie kikamilifu.

“Tunaipongeza Wizara ya Maji, chini ya usimamizi wa Waziri wake Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kwa kuwa msitari wa mbele kuhakikisha dhamira ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani inatimia; Rai yetu ni kwamba Wizara ihakikishe hairudi nyuma na inapeleka miradi kwenye maeneo yote yenye changamoto,” ameelekeza Sillo.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo (kulia) akiongozana na wajumbe wa kamati na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya kukagua mradi wa maji wa Butimba

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb) alipokea maelekezo ya Kamati na ameihakikishia kuwa Wizara haitorudi nyuma kuhakikisha dhamira ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani inatimia

“Sisi kama Wizara hatutokuwa kikwazo kwa Watanzania kupata majisafi, salama na yenye kutosheleza, tutapambana muda wote kuhakikisha miradi inajengwa kwa ubora unaotakiwa na inakamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma,” amesisitiza Aweso

Mhe. Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo mkubwa wa maji Jijini Mwanza ambao amesema umeanza kunufaisha baadhi ya maeneo na hivyo kupunguza adha ya maji iliyokuwepo katika baadhi ya maeneo.

Amebainisha kuwa uelekeo wa Serikali kupitia Wizara ya Maji ni kujenga miradi ya maji ya kimkakati kwa kutumia vyanzo vya maji toshelevu hususan katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji ili kufikisha asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya mijini na aslimia 85 kwa maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2025.

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiwa ameambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati wa ziara katika mradi wa maji wa Butimba

“Tunamshukuru sana Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu mkubwa ambao tayari tumeanza kushuhudia matunda yake katika baadhi ya maeneo hasa ikizingatiwa kuwa changamoto ya maji kwa Jiji la Mwanza hapo awali ilikuwa ni kubwa,” amesema Waziri Aweso.

Waziri Aweso ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanaunganishwa na huduma ya maji na kusiwe na sababu zisizo za lazima katika kutimiza zoezi hilo.

Aidha, ametoa pongezi kwa Wabunge wa Nyamagana na Ilemela, uongozi wa Mkoa wa Mwanza na Wilaya zake na Bodi ya Wakurugenzi MWAUWASA kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri na wa karibu wa mradi.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza