Tutakapokuwa tumewapata, katikati ya mwezi huu wa kumi tutawakutanisha tena na mabenki kwamba hizi ndizo kampuni zitakazokuwa zinashindana kuleta mafuta nchini. Hivyo watakaa na kujadili na kuelewana biashara itakwendaje kwa pamoja. Tunajua inawezekana na biashara itafanyika vizuri.

JAMHURI: Mmejipangaje kukabiliana na udanganyifu ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta nchini?

Mjinja: Katika mfumo huu, bahati nzuri kila kitu kipo wazi, suala la mafuta ni mtambuka, sio wakala tu tunaoshughulikia hili, tunafanya kazi kwa karibu sana na vyombo vyote vya Serikali kwa maana wahusika wote – Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango (TBS), Wakala wa Vipimo (WMA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), na tunatoa taarifa mbalimbali katika vyombo vingine vinavyohusika.

Ni wakala huu kwanza anayepokea oda kutoka kwenye kampuni za mafuta. Ni sisi ndiyo tunaopanga kwamba kiasi fulani kije kwenye meli, na huyu anayeleta hiyo meli sisi ndiyo tunaomwambia kwamba kwenye meli hiyo jaza kiasi fulani cha mafuta. Anapojaza hayo mafuta huko anakoyajazia kwenye hiyo meli, sisi tunamtaka atupatie nyaraka kabla meli haijafika hapa, atwambie amejaza kiasi gani, je, ni kama tulivyoagiza, na je, kiwango cha mafuta ni kama tulivyoagiza? Anatupatia vyeti vyote hivyo, pia tunavitawanya kwenye vyombo vyote husika.

TRA – meli fulani inakuja na kiasi fulani cha mafuta na kampuni zote zilizoagiza mafuta hayo kwa maana ya kiasi husika. TBS –  mafuta yanayokuja tumepatiwa vyeti kutoka huko yalikojazwa hivi hapa, yamekidhi kiwango, lakini nawe kuwa tayari kutimiza wajibu wako, wakala wa vipimo nao vile vile. Meli inapofika nchini kabla mafuta hayajaruhusiwa kushushwa kwenye meli wakala wa vipimo na wataalamu wengine wanatakiwa kuingia kwenye meli na kufanya vipimo akiwapo mwakilishi wetu na mwakilishi wa wasambazaji wa mafuta hayo.

TBS wao wanakwenda kuchukua vipimo wakiwa na mwakilishi wetu, mwakilishi wa msambazaji pia anakuwepo ikiwa ni pamoja na mwakilishi wa Ewura ili kujua ubora wake. TRA nao wanakuwapo pia. Kisha tunaletewa taarifa kuhusiana na mzigo huo. Na masharti ya mkataba wetu ni kile kiasi kilichopimwa na kukutwa ndicho kilichofika katika bandari yetu. 

Mafuta yanayoingia nchini yapo yanayopimwa na flow meter. Sasa hivi kwa mafuta ya dizeli yanayopakuliwa SPM mita inafanya kazi ilishafungwa mpya, angalau tunahesabu kutoka hapo. Kwa KOJ hiyo mita bado hawajaweza kuirekebisha nafikiri itabidi wafunge nyingine mpya. Kwa hiyo, tuna maeneo tofauti tofauti ya kujua ujazo wake. Hatuoni hatari yoyote ya kufanyika ujanja wa aina yoyote. Pia mafuta hayapakuliwi mpaka pale yatakapokuwa yamefanyiwa ukaguzi na TBS na kutoa cheti cha ubora. Kwa mfano, kama kuna utata wa ujazo, wakala wa vipimo vyao ndiyo vya mwisho kwa maana na majibu kuhusu ujazo. Hii iko kwenye mkataba kabisa.

JAMHURI: Nini mkakati wenu katika kuboresha biashara hii nchini?

Mjinja: PBPA tumejipanga kuhakikisha tunakuwa na usalama wa uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini kwa muda wote na kwa gharama stahiki. Biashara ya mafuta na mambo yake yote ni eneo ambalo Watanzania hatujalichangamkia. Si katika biashara, si katika weledi wala taaluma; nikiangalia hata katika kampuni zetu za mafuta ya ndani wafanyakazi wake wengi ambao ni muhimu zaidi wanatoka nje ya nchi. Sababu hatujaliangalia sana hili eneo, tuna upungufu wa wataalamu katika hili eneo. Kwa kweli ni muhimu sana maana mafuta ni moja ya biashara kubwa katika nchi yoyote duniani. Ni fursa ambayo Watanzania wanaweza wakaanza kuingia kufanya biashara lakini pia kujifunza mambo yanayohusiana katika biashara ya mafuta.

Waweze kujua ni vitu gani vipo hapa katikati, mafuta yanapatikanaje, mikataba ya meli inaingiwaje. Kuna vitu vingi sana hapa ambavyo havijafanyiwa kazi. Kwa mfano, wenzetu Kenya wana chuo kinachofundisha mambo ya biashara kwenye mafuta. Na ukiangalia kwa kiasi kikubwa hata wafanyakazi waliopo kwenye kampuni wanachukuliwa kutoka Kenya. Ni vyema tukaiangalia hii fursa na kuitumia. 

Uagizaji wa mafuta ya petroli nchini

Mwaka 2015/16, Bandari ya Tanga ilianza kupokea mafuta kupitia Mfumo wa Uagizaji Mafuta ya Petroli kwa Pamoja (BPS) kuanzia Julai, 2015. Katika kipindi cha Januari na Desemba, 2015 jumla ya lita bilioni 5.16 za mafuta ya petroli ziliingizwa nchini kupitia bandari za Dar es Salaam (lita bilioni 4.25) na Tanga (lita milioni 91.27). Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na lita bilioni 4.63 zilizoingizwa mwaka 2014. Kati ya mafuta hayo, lita bilioni 3.1 sawa na asilimia 60 yalikuwa kwa ajili ya matumizi ya ndani na lita bilioni 2.06 sawa na asilimia 40 yaliyokuwa kwa ajili ya nchi jirani.

Mafuta kwa ajili ya matumizi ya ndani yameongezeka kwa asilimia 9 kutoka lita bilioni 2.84 mwaka 2014 hadi lita bilioni 3.10 mwaka 2015. Aidha, mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya nchi jirani yameongezeka kwa asilimia 15 kutoka lita bilioni 1.79 mwaka 2014 hadi lita bilioni 2.06 mwaka 2015. Ongezeko hilo linatokana na kukua kwa mahitaji ya mafuta ndani ya nchi pamoja na nchi jirani kuongeza uagizaji wa mafuta kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

 

Mwenendo wa bei za mafuta katika soka la dunia

Januari, 2015 bei ya mafuta katika soko la dunia ziliendelea kushuka na kufikia wastani wa dola za Marekani 38 kwa pipa la mafuta ghafi kwa Desemba, 2015. Aidha, wastani wa bei ya mafuta yaliyosafishwa kwa kipindi cha kati ya Januari na Desemba, 2015 ulikuwa kama ifuatavyo: Petroli kutoka dola za Marekani 669 hadi dola za Marekani 437 kwa tani; dizeli kutoka dola za Marekani 570 hadi dola za Marekani 335 kwa tani; na mafuta ya taa/ndege kutoka dola za Marekani 570 hadi dola za Marekani 363 kwa tani ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 35 kwa petroli, asilimia 41 kwa dizeli na asilimia 39 kwa mafuta ya taa/ndege, sawia.

Bei ya mafuta katika soko la ndani hutegemea bei ya mafuta ya petroli katika soko la dunia pamoja na thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2015 wastani wa bei za mafuta katika soko la ndani kwa lita ilikuwa: Petroli shilingi 1,973, dizeli shilingi 1,808 na mafuta ya taa shilingi 1,739 ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,186 kwa petroli, shilingi 2,082 kwa dizeli na shilingi 2,030 kwa mafuta ya taa kwa kipindi kama hicho katika mwaka 2014.

Ewura iliendelea kusimamia shughuli za uagizaji wa LPG nchini. Kati ya Januari na Desemba, 2015 jumla ya tani 70,061 ziliagizwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali nchini ikilinganishwa na tani 65,611 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 7. Ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa uelewa kuhusu manufaa ya matumizi ya LPG, kuboreshwa kwa miundombinu ya kuhifadhi, kujaza mitungi na kusambaza LPG katika mwaka 2016/17.

By Jamhuri