Waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda cha nguo cha Morogoro Polyester Textile cha mjini Morogoro, wameiomba Serikali kuingilia kati ili waweze kulipwa madai yao baada ya kuachishwa kazi miaka 18 iliyopita.

Akizungumza na JAMHURI, Laurian Kazimilli, Mwenyekiti wa wastaafu hao, anasema miaka 18 imepita tangu waanze kuhangaikia madai yao na kuna wenzao wengi ambao tayari wametangulia mbele ya haki.

Anasema idadi kamili ya watu waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho ni watu 1,267 na kati ya hao waliobahatika kulipwa mpaka sasa ni watu 84 tu, hali ambayo imesababisha wenzao wengi kupoteza maisha kwa kukata tamaa.

“Kinachotushangaza ni kwamba misingi ya madai yetu sote 1,267 ilikuwa sawa, iweje wachomolewe watu 84 tu ndiyo waonekane wanafaa kulipwa na tuliobaki malipo yetu yaonekane kama si halali… hakika huu si uungwana,” anasema Kazimilli.

Anasema msingi mkubwa wa madai yao ulianza kuanzia tarehe 1 Desemba 1998 mara tu baada ya kukabidhiwa barua zao za kuachishwa kazi huku wakielezwa kuwa hatua za kulipwa madai yao yangefuata.

Kazimilli anabainisha mara baada ya kiwanda hicho kuuzwa malipo ya mafao yalitolewa kwa upendeleo na ubaguzi kwa njia ya siri huo ulikuwa ni mwaka 2011 na kampuni ya PRSC/CHCC Consolidated Holding Corporation na yalifanyika katika kituo cha zimamoto.

Kazimilli anasema kwa kipindi cha miaka mingi madai yao yamekuwa yakizuiwa na baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu ndani ya Serikali.

Anasema kwa mara ya kwanza walianza kufikisha kero zao ngazi ya tarafa, wilaya, mkoa, ofisi za PSRC, ofisi zote za CCM, Hazina, Wizara ya fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es Salaam na Dodoma lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na mamlaka hizo kulimaliza tatizo lao.

Kazimilli anabainisha kuwa wamefanya jitihada za kuonana na viongozi mbalimbali nchini, lakini imeshindikana huku wakikutana na vikwazo visivyoisha.

Anasema walimwandikia barua Waziri wa Fedha tarehe 10/12/2013 kupinga barua ya Hazina ya tarehe 26/11/2013 na pia waliomba kuonana na Waziri wa Fedha wa wakati huo, bila ya mafanikio.

Anasema mwaka 1993 Tanzania ilianza kutekeleza sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma vikiwamo viwanda ambapo ilisema kuwa imeamua kujitoa katika uendeshaji wa biashara, hali iliyosababisha Watanzania wengi kukosa ajira baada ya baadhi ya viwanda kufungwa na watu wengi kupoteza haki zao.

Anaeleza kuwa ubinafsishaji wa mashirika ya umma umesababisha maumivu kwa Watanzania wengi huku jumla ya mashirika 374 yalibinafsishwa yakiwamo ya Kilimo 95, Viwanda 94, miundombinu 23, Maliasili 34 , Nishati 15 ambapo viwanda 32 kati ya hivyo vimefungwa.

Anasema kutokana na utapeli mkubwa uliofanywa na baadhi ya watendaji waliokabidhiwa majukumu ya kusimamia zoezi hilo, Watanzania wengi walijikuta wakipoteza haki, hali iliyochangia kwa kiwango kikubwa wengi kufariki.

“Hata wengi wa wafanyakazi wenzetu tuliokuwa nao wameshapoteza maisha baada ya kukabiliwa na hali ya sintofahamu, kujikuta wakikosa huduma muhimu na kuishi katika umasikini kwa miaka mingi huku mamlaka husika zikishindwa kulifanyia kazi suala hili,” anasema Kazimilli.

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Aziz Abood, alipoulizwa juu ya madai hayo ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho alikiri kuyafahamu madai ya wafanyakazi hao na kusema kuwa ni ya miaka mingi ambayo yalishafika ngazi za juu.

“Haya ni madai ya miaka mingi sana, na wengi wa wazee hawa walishatangulia mbele ya haki, huku hata hawa waliopo wakiendelea kuishi katika mazingira magumu,” anasema Abood.

Anasema madai ya wazee hao yamegawanyika katika maeneo mengi; kuna wale waliostaafishwa baada ya kampuni kubinafsishwa, walioomba kustaafu na madai mengine.

“Mpango huu wa kubinafsisha mashirika ya umma ulikuwa mzuri uliolenga kuinua uchumi wa nchi, lakini baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu walitumia nafasi hiyo kutenda isivyo,” anasema Abood.

Anasema wazee hao ambao wengine wameshatangulia mbele ya haki ni wahanga wa uliokuwa mpango wa kubinafsisha mashirika ya umma ambayo mengi yaliuzwa kwa watu binafsi.

Waziri wa Sera, Bunge,Kazi, vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alipoulizwa juu ya suala hilo anasema masuala ya madai ndani ya ofisi yake ni mengi sana na hawezi kulijua suala hilo mpaka aitishe faili lao.

“Unajua ofisi ni taasisi kubwa kwa maana hiyo malalamiko yanayoingia na kutoka pale ni mengi sana kwa jinsi hiyo siyo rahisi kukumbuka kila lalamiko,” anasema Mhagama.

Anasema yapo madai mengi sana yaliyotokana na kuuzwa kwa baadhi ya mashirika na makampuni ya kiserikali miaka ya nyuma lakini wengi wao walishapewa haki zao.

Anasema tatizo lililopo hapa nchini kwa sasa ni watu wengine kufikiria kuwa kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni mpya wanadhani kuwa inaweza kubatilisha uamuzi ambao ulishafikiwa wakati wa awamu iliyopita, kitu ambacho si kweli.

3043 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!