Suzy Butondo,JamhuriMedia, Shinyanga

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Patrobas Katambi ambaye ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amekabidhi gari la kubebea wagonjwa ‘ Ambulance’ na vitanda nane kwa ajili ya wagonjwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni pamoja na majiko ya gesi 145 kwa makundi mbalimbali ya jamii.

Akikabidhi gari, vitanda na majiko ya gesi leo Februari 8,2024 katika stendi ya magari ya Kambarage, amesema vitanda hivyo vitasaidia wananchi katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na gari itasaidia kuwawahisha wagonjwa kuwapeleka kupata matibabu katika hospitali kwa wakati.

“Leo nakabidhi gari hili ‘Ambulance’ niliyopewa na mama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili lisaidie kuboresha huduma mbalimbali za afya katika hospitali yetu ya Manispaa ya Shinyanga.”amesema Katambi.

“Nimefanya zoezi hili lakini pia bado ninaendelea na zoezi la kugawa majiko ya gesi kwa makundi mbalimbali yasaidie katika kutunza mazingiria ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo nakabidhi majiko 145 kwa ajili ya wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga,”ameongeza Katambi.

Waliopewa majiko hayo ni Mwenyekiti na Katibu wa Chama cha Walimu Manispaa ya Shinyanga,Maafisa tarafa, watendaji wa kata, shule za sekondari na msingi na Hospitali za Manispaa ya Shinyanga ili kupambana na tabia nchi.

Katika hatua nyingine Katambi amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, barabara na ujenzi wa masoko.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Revocatus Lutundu amemshukuru Mbunge Katambi kwa kushughulikia haraka changamoto ya gari la wagonjwa, kwani kulikuwa na changamoto ya gari la wagonjwa katika hospitali ya manispaa ya Shinyanga.

Kwa upande wake mganga mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Dkt. Elisha Robert amesema gari hilo litasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto,kwani walikuwa na magari mawili, moja likapata hitilafu,wakabaki na moja ambalo pia lina changamoto, hivyo wamekuwa wakilazimika kutumia gari la utawala kama Ambulance sasa baada ya kupata gari hilo litasaidia.

Naye katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odiria Batimayo amesema gari hilo la wagonjwa litasaidia kupunguza changamoto ya usafiri kwa wagonjwa, lakini pia vitanda vitasaidia wagonjwa wodini ikiwa ni matunda mazuri yanayotokana na uongozi mzuri wa Rais Samia Suluhu Hassan.

By Jamhuri