πŸ“Œ Dkt. Biteko atahadharisha hakuna visingizio

πŸ“Œ Apongeza wananchi Mpanda, Kupokea miradi ya Maendeleo

πŸ“Œ Rais Samia kufanya ziara Katavi

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati-KATAVI

Hatimaye Mkoa wa Katavi unatarajiwa kuingizwa katika matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa ifikapo Septemba, 2024 baada ya kuikosa huduma hiyo kwa zaidi ya miaka sitini ya Uhuru Tanzanaia.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Njia Kuu ya kusafirisha umeme Msongo wa KV 132 kutoka Tabora hadi Katavi na Kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme kilichoko Mpanda.

Dkt. Biteko amesema kitendo cha Mkoa wa Katavi kutokuwa katika Gridi ya Taifa kimeunyima mkoa huo fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushindwa kufanya uzalishaji wa uhakika na tatizo hilo limedumu kwa miongo kadhaa.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo imewezeshwa na Imani ya wananchi wa Mpanda ambao walikubali maeneo yao kutumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hata kabla ya kupewa fidia.

β€œNawashukuru wananchi kwa imani mliyoonesha na kuhakikisha miradi inajengwa na inamalizika kama ilivyo katika ujenzi wa mradi huu, natarajia mradi huu utakamilika mwezi Septemba, mwaka huu na nimetoa hadi mwezi Oktoba ili kutoa mwanya kama kuna dharura inayoweza kutokea,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amefafanua kuwa kwa sasa hakuna wakati wa visingizio juu ya kwanini wananchi wasipate umeme wa uhakika ijapokuwa Serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa kipaumbele katika huduma mbalimbali za jamii.

Awali akitoa maelezo kwa Dkt. Biteko, Meneja wa Mradi Mha. Sospeter Oralo amesema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 97 na ujenzi wa laini umekamilika kwa asilimia 63.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mridoko amesema Wananchi wa vijiji vyote 172 na maeneo ya ziada 114, Wanatamani sana kupata umeme wa uhakika na kuondokana na mgawo wa umeme jambo litakalowawezesha kuzalisha bidhaa mbalimbali katika kukuza na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Mrindoko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma na kuridhia ujenzi wa kituo kwa ajili ya kupokea, kupoza na kusafirisha umeme wa uhakika ambao uko mbioni kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa huo, Mbunge wa Mpanda, Sebastian Kapufi amepongeza juhudi za serikali za kupeleka umeme wa uhakika kwa wananchi ili watumie kujiletea maendeleo.

Ameiomba serikali kupitia mpango wa kupeleka umeme wa gridi kwa mikoa ya pembezoni, kupeleka umeme kwa wachimbaji wadogo wa madini ili kuboresha na kuanzisha matumizi ya teknolojia katika sekta hiyo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Biteko amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki na kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kufanya ziara Mkoani Katavi hivi karibuni.

β€œNiwatake mjitokeze kwa wingi kumpokea na kumsikiliza Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia ambaye anatarajia kufanya ziara hapa mkoani” amesema Dkt. Biteko na kuongeza kuwa Mheshimiwa Rais ni kinara wa utatuzi wa changamoto za wananchi. (Tarehe 9, Julai 2024).