Sehemu iliyopita, mwandishi alieleza hatari ya kuwa na uraia wa nchi mbili, akisema haufai. Pia akataka wananchi wafikirie kiuzalendo Katiba yetu na iwe kweli ya Kiafrika na hasa hasa ya Kitanzania. Endelea…

Mimi nimeelezea haya kihistoria wala si kama wanasheria wanavyotafsiri. Kwa wanasheria Katiba ya nchi inaelezwa kuwa ni Hati ya Kisheria (a constitution is a Legal Document), au niseme Katiba ni chombo cha kisheria kinachoongoza maisha ya watu, kinatoa mfumo wa utawala katika nchi unaowezesha wakazi wake kuishi kwa amani na utulivu na kuendesha shughuli zao kwa manufaa ya wote.

 

Basi, kwa tafsiri namna hii ya Katiba kila Taifa linatunga katiba yake kulingana na matakwa ya Taifa lile. Hapa napenda kutoa kama kielelezo tu mifano ya Katiba mbili tofauti.  Moja ni ile Katiba ya Marekani na nyingine ni Katiba ya Uingereza, mabingwa wa kutunga Katiba zilizoenea katika mataifa ya madola ya Uingereza (Commonwealth countries).

 

Historia ya Marekani (USA) inaonesha kuwa Katiba yao ilitokana na mapinduzi. Wale walikuwa ni makoloni ya Uingereza. Walipodai uhuru wao kutoka kwa Waingereza walipata baada ya mapigano ya muda mrefu. Ndipo Julai 4, 1776 wakajitangazia uhuru wao kwa kujinasua kutoka ukoloni wa Mwingereza. Kwa kuwa majimbo yao kule Marekani yalikuwa yakijitawala. Basi, waliamua waunganishe majimbo yote wawe kitu kimoja, taifa moja na lenye Serikali moja.

 

Hivyo, viongozi wa yale majimbo (wenyewe wanaita states) walikubaliana wawe na Katiba moja. Ndipo kuanzia Mei 25, 1785-Septemba 17, 1785 walikuwa na mkutano wa Katiba unaojulikana kama “Constitutional Convention” ambako viongozi 55 wa Congrress kutoka majimbo (states) 12 ya Marekani walikutana na kukubaliana aina za Katiba kwa nchi yao.

 

Mkutano ule wa Katiba ulifanyika katika mji wa Pennsylvania, Jimbo la Philadelphia. Viongozi wale 55 walikubaliana Rasimu ya Katiba ya Marekani na kaulimbiu ya Katiba ile ilikuwa “Popular Sovereignty” – ndiyo uwe msingi wa Katiba yao.

 

Maneno haya yalimaanisha Katiba ya Marekani msingi wake utakuwa Dola Huru ya Watu na huo utakuwa ndiyo mfumo wa utawala wao. Basi, Katiba iliyotungwa ilisema hivi, nanukuu;

 

“It makes its constitutioin the permanent medium of its orders or prohibitions to all branches of the federation government and to many branches of the state governments; they must do what the constitution directs and leave undone what it forbids. The people, therefore continually laying their commands on the governments…” (Imenukuliwa kutoka Encyclopedia

Britannica 1768 vol. 22 uk. 755).

 

Kwa Katiba namna hii mimi ningetafsiri kuwa kilikuwa chombo kilichotoa miongozo, amri na makatazo kwa serikali za majimbo, miongozo namna hii inaitwa “decrees” (amri za utekelezwaji zilizokuwa zinatolewa kuelekeza nini cha kufanya na nini kisifanyike katika nchi).

 

Marekani walianzia huko siku zao za mwanzo wa Uhuru wao. Lakini waliweka neno la kuonesha kuwa wananchi walikuwa na nafasi ya kuchangia maongozi ya serikali yao pale Katiba ilipoweka wazi uwezo namna hiyo (the people therefore are continually laying their commands on the governments) mikononi mwa wananchi.

 

Hali kama hii ndiyo iliyotokea Zanzibar mara tu baada ya Mapinduzi. Utawala wa awamu ya kwanza Visiwani enzi za Mzee Karume ulikuwa unatoa “decrees” kuendesha Serikali Visiwani. Jambo hili liliwaudhi sana Waarabu, watu wa sultani na wa nchi zote za Magharibi! Kumbe ulimwenguni baada ya mageuzi ya serikali hatua za kwanza ni utawala wa “decrees” mpaka pale utaratibu wa kikatiba utakapokamilika.

 

Waarabu hawakujua hili? Mbona Marekani walifanya? Waingereza na Marekani wanalijua hilo, lakini basi wote walisitasita kuyatambua yale Mapinduzi ya Visiwani ya mwaka 1964.

 

Tugeukie Uingereza waliotutawala sisi Watanganyika na Wazanzibari.  Uingereza kumbe nao ni nchi ya Muungano wa vinchi vinne tofauti – England, Scotland, Wales na Ireland Kaskazini. Hawa hawana Katiba kabisa iliyoandikwa kama yetu tunayojitahidi kuiandika. Wao wana Katiba ya kimapokeo (have no written constitution).

 

Nchi zao ziliungana katika miaka tofauti tofauti. Lakini mwaka 1801 ndipo walipotunga sheria yao ya muungano inayojulikana kama “The 1801 Act of Union” iliyoziunganisha nchi zote nne na kuunda Umoja wa Uingereza – The United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland” kwa kifupi wanaitwa tu UK.  (Na ndugu zangu Wakerewe eti nao hujigamba kama wana UK!)

 

Basi, Waingereza wanajigamba kuwa Katiba yao ni ya kipekee ulimwenguni na kwamba wao ni mafundi wa kuwatungia Katiba nchi zote za madola ya Uingereza (Commonwealth countries).

 

Katiba yao inatamka hivi na nukuu “…The British Constitution is unique, among existing constitutions in antiquity, endurance, adaptability and influence. Much of the perculiar genius of the constitution is attributed to the fact that it is partly UNWRITTEN and WHOLLY FLEXIBLE” (imenukuliwa kutoka Encyclopedia Britannica 1768 vol. 10 uk. 734 na 736). Kutokana na Katiba yao hiyo kuna lile neno “influence” wanasema wamefanikiwa kuyashawishi mataifa kadhaa kuandikiwa katiba zao huko Westminister – Uingereza.

 

Katiba yetu ya Tanganyika iliandikwa Uingereza mwaka 1961 (Lancaster House) na Katiba ya kwanza ya ndugu zetu wa Zanzibar ya mwaka 1963 iliandikwa huko huko Uingereza- Lancaster House. Katiba ya Zanzibar ilipoandikwa ujumbe wa ASP uliwajumlisha wazee wetu Abeid Amani Karume, Aboud Jumbe Mwinyi, Hasnu Makame na hata mzee mwenzangu Hassan Nassor Moyo alihudhuria kama msikilizaji.

 

Basi, masuala ya Katiba nimeonesha kihistoria kuwa kila taifa lina mtindo wake wa kuandika tangu zamani. Tofauti ni kuwa Katiba za siku zile mawazo ya wananchi wa kawaida hayakuombwa ambako leo hii tumepewa nafasi sisi sote tutoe mawazo yetu ili yaingie kwenye hiyo Katiba mpya na hivyo ionekane kuwa ni yetu sote na wala si ya kubambikiziwa tu!

Baba wa Taifa alitoa utangulizi murua katika Katiba ile ya kwanza kabisa ya Tanganyika kabla ya kupata Uhuru wetu mwaka 1961. Aliandika haya nayanukuu:

 

“A country’s written Constitution is a legal document of some complexity; but the good citizen should not be deterred by its complexity from a strenuous effort to understand the framework of his country’s independence. Hence this special publication will, I hope, be widely read.

 

“In particular, I trust that the young will take particular note of the preamble, where they will find expressed those high ideals by which our country should always seek to direct itself. The concepts of liberty, of equal rights for all, of an independent judiciary should be inculcated into the youth of Tanganyika from the earliest possible stage. It is the duty of all of us to see that these ideals become truly a part of our national life, and not mere catchwords and slogans of no significance”.

 

Mwalimu alishauri kuwa pamoja na ugumu (complexity) wa kuielewa Katiba, lakini raia mwema asikatishwe tamaa na hilo, bali ajaribu kuisoma na kuielewa Katiba ya nchi yake.  Vijana wajitahidi kweli kuielewa na kuitafsiri vilivyo. Katiba hii inasimamia Uhuru na haki sawa kwa Watanganyika wote. Vijana wajengwe au wafundwe tangu mwanzo kuielewa Katiba ya nchi yao.

 

Basi, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuielewa Katiba yetu hii na kuishi kwa misingi yake thabiti kujenga Taifa la nchi yetu changa. Ni Katiba inayosimamia Uhuru, haki sawa kwa wote na Uhuru wa Mahakama. Wala haya yasiwe kama kaulimbiu tu. (Utangulizi katika Katiba ya Tanganyika 1961).

 

Juni 28, 1962 tulipokuwa tunajiandaa kuwa Jamhuri ya Tanganyika, Baba wa Taifa alitoa hoja bungeni namna ya kuandaa Katiba ya Jamhuri mpya ya Tanganyika.

 

Kwa mtazamo wake alionya hivi, namnukuu: “…It was impossible to device a foolproof constitution, and that the only real protection against tyranny is a national ethic…” (Taz. Uhuru na Umoja sura 39 uk. 174).

 

Kwa mtazamo huo, Mwalimu aliweka wazi kabisa kuwa hakuna KATIBA ISIYOKUWA NA UPUNGUFU, la muhimu kwa Taifa ni kuwa na MAADILI YA KITAIFA. Hii maana yake Katiba yoyote kuwa nzuri lazima isisitize kuwapo kwa maadili ya Taifa husika na ndiyo makuzi ya UZALENDO.

 

Nchi ikiwa na uzalendo watu wake wanakingwa kwa Katiba yao hiyo na likitokea jambo lisilowafaa kitaifa wananchi hao wanaweza kulikataa kuwa jambo namna hiyo si la kitaifa lao na hata akitokea kiongozi fedhuli bado wananchi kwa kulindwa na hiyo Katiba yao wanaweza kumkataa kwa kusema uamuzi wake hatuukubali maana si wa kikatiba yao hiyo.

 

Mwalimu alisema maneno hayo kwa Kiingereza namna hii; “that we cannot tolerate, that is un – Tanganyikan if the people do not have that kind of ethic, it does not matter what kind of constitution you frame. They can always be victims of tyranny. (Tazama Nyerere: Uhuru na Umoja uk. 174).

 

Nchi yenye Katiba nzuri ni yenye kuwa na maadili ya kitaifa, wananchi wake wanaweza kukataa kufanya kinyume cha maadili ya taifa hata Katiba ya nchi itamkeje.

 

Mwalimu aliendelea kusema maadam maadili ya kitaifa yapo, hata mkuu wa nchi atasita kutoa uamuzi kandamizi kwa kuchelea uzalendo wa nchi na kuita kitendo kinachokwenda kinyume cha maadili kuwa siyo cha kitaifa. Wakati ule Taifa letu lilikuwa ni Tanganyika ndipo alitamka haya (….which makes the Head of State, who ever he is to say, I have the power to do this under the Constitution, but I cannot do it, it is un-Tanganyikan”).

 

Itaendelea

Please follow and like us:
Pin Share