Obama amedhihirisha ugaidi ni tishio

Tanzania imepata bahati ya kutembelewa na Rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye ni miongoni mwa viongozi wakuu maarufu wachache duniani. Marekani ni taifa lenye nguvu kubwa ya kijeshi na kiuchumi. Ni miongoni mwa mataifa yanayounda Umoja wa G8 – yaani mataifa manane yenye nguvu za kiuchumi na kijeshi duniani.

Hatua ya Rais wa Marekani kuzuru Tanzania imeleta matumaini mapya kwa Watanzania ingawa wapo wanaosema kuwa ziara hiyo ni mahususi kwa maendeleo ya taifa la Marekani.

 

Lakini ni imani yangu kuwa miradi iliyozinduliwa, mikakati pamoja na mipango ya maendeleo, hususan matumizi ya gesi kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya umeme, ajira kwa vijana, huduma za afya kwa jamii, elimu na uboreshaji wa miundombinu, vyote hivi vikitekelezwa kwa wakati na kwa ushirikiano, taifa letu litasonga mbele kimaendeleo katika nyanja nyingi.

 

Katika dunia ya leo, suala la uwekezaji wa ndani na nje kwa kutumia sekta binafsi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, halikwepeki. Marekani itasaidia kutoa fursa za maendeleo na kupatikana kwa ajira kwa kuwekeza nchini na kufanya biashara kwa pamoja.

 

Msukumo na nia ya kuandika makala haya leo ni kutaka kuzungumzia suala la tishio la ugaidi na ugaidi duniani.  Nalizungumza hili kutokana na nilivyoshuhudia Wamarekani  wanavyoweza kuwa na tahadhari ya kupambana na hujuma zozote za ugaidi na magaidi ndani na nje ya nchi yao. Nimeshuhudia jinsi uimarishwaji wa ulinzi wa hali ya juu kabla na baada ya kuwasili kwa Rais Obama hapa Tanzania, akifuatana na ujumbe wa watu takriban 700 wakiwamo mke na watoto wawili.

 

Pamoja na ukweli kuwa kulikuwa na ugeni mwingine wa viongozi mbalimbali kutoka Afrika na kabla ya kuondoka Rais Obama, aliwasili Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush, lakini ulinzi mkubwa uliandaliwa kwa ajili ya usalama wa Rais Obama na ujumbe wake. Je, rais mstaafu, Bush hastahili kuwa na ulinzi mkubwa kiasi hicho?  Je, azma ya magaidi ni kumlenga kiongozi wa Marekani aliyeko madarakani tu? Na kama ndiyo kusudi lao, kwanini iwe hivyo?

 

Baada ya kutafakari kwa kina, nimegundua kuwa Marekani inahisi kuwa bado ina maadui wengi hata baada ya kumuua Osama bin Laden, Kiongozi wa Kundi la Al Qaeda. Uvamizi wa kijeshi nchini Afghanistan na Iraq, uliofanywa na watangulizi wa Obama na hatimaye yeye (Obama), kujikuta inamlazimu kupambana na ugaidi na hatimaye kufanikisha kuuawa kwa Osama bin Laden; kumemfanya awe adui wa kundi la Al Qaeda na wafuasi wake.

 

Kwa mantiki hiyo, taifa la Marekani linalazimika kutumia gharama kubwa kuhakikisha ugaidi unatokomezwa. Aidha, Serikali ya Marekani imekuwa ikihakikisha ziara za rais wao huyo nje ya nchi zinaratibiwa vema na kwa gharama kubwa, lengo likiwa ni kulinda usalama wake na ujumbe anaoambatana nao.

 

Tanzania ni nchi yenye utulivu na amani lakini imezungukwa na nchi zenye migogoro ya ndani na nje, mathalani Somalia. Kikundi cha Al-Shabaab cha Somalia kimekuwa ni miongoni mwa vikundi vya ugaidi vilivyoorodheshwa na Marekani tangu mwaka 2008. Al-Shabaab wamekuwa tishio kwa usalama wa ndani na nje ya Somalia. Aidha, ni wapinzani wakubwa wa sera za Kimagharibi na za Marekani.  Hivyo, kutokana na ujirani wao na Tanzania, Serikali ya Marekani pamoja na makachero wake wa FBI, ililazimika kufanya kazi kubwa ya kiintelejensia kuhakikisha ziara ya rais wao inafanikiwa.

 

Serikali ya Marekani iliratibu ziara ya kiongozi wao kuzuru nchi tatu za Afrika – Senegal, Afrika Kusini na Tanzania. Kote huko ulinzi uliimarishwa na kufanikisha rais wao anahitimisha ziara yake na kurejea Marekani salama salimini.

 

Tumeshuhudia ujio wa meli kubwa yenye zana za kivita, ndege vita na magari, mbwa na wanausalama (FBI) wa kutosha katika ziara ya saa zisizozidi 48 hapa nchini. Tunajifunza nini katika hili? Je, sisi tuko salama kweli? Na kama ndivyo, kwanini Wamarekani waweke ulinzi uliotia fora?  Kwa mtazamo wangu, sisi pia hatuko salama katika suala zima la kupambana na ugaidi. Si wote waliofurahishwa na ujio wa Rais Obama hapa nchini. Sasa kama hilo linaweza kuwa ni jibu sahihi, basi na sisi hatuna budi kuimarisha ulinzi hapa nchini.

 

Vikundi vya ugaidi bado vipo na vingine kuzaliwa kwa sura mpya, lakini vikiwa na itikadi zilezile. Milipuko ya mabomu iliyotokea nchini Kenya mwaka uliopita baada ya Kenya kuivamia Somalia, imeifanya nchi hiyo kuwa macho dhidi ya ugaidi. Wapiganaji wa Al-Shabaab bado wana uchungu na kusambaratishwa kwao na majeshi ya kigeni.

 

Milipuko ya mabomu iliyotokea mkoani Arusha na kusababisha vifo na majeruhi kwa watu kadhaa, inanifanya niwaunge mkono Wamarekani katika suala zima la kujihami wakati wowote na mahali popote dhidi ya ugaidi na magaidi.

 

Kuna kila sababu za kuendelea kuimarisha ulinzi katika mipaka yetu. Kuna kila sababu ya kuimarisha ulinzi kwenye maghorofa yanayoendelea kujengwa kila kukicha sehemu mbalimbali nchini. Kuna kila sababu ya kuimarisha ulinzi shirikishi kuanzia ngazi ya kifamilia hadi taifa. Kuna kila sababu ya kuwapo tathmini ya mara kwa mara ili kubaini idadi ya wahamiaji haramu nchini na kuchukua hatua za kisheria.

 

Kumekuwapo na uuzwaji holela wa silaha katika maeneo ya mipakani mwa nchi yetu. Kumekuwapo na ujangili wa mara kwa mara na vifo vya raia wetu katika maeneo hayo, vinavyosababishwa na raia wa nchi jirani, wengi wao wakitoka kwenye makundi ya waasi wa serikali zao.  Natambua kuwa hatuna uwezo na zana bora kama walizonazo Wamarekani katika kuimarisha ulinzi, lakini ni imani kuwa tuna vyombo vya usalama vinavyofanya kazi ya kuhakikisha mipaka ya nchi yetu inalindwa pamoja na raia na mali zao.

 

Hofu yangu ni kwamba ulinzi wetu mara kwa mara umekuwa si endelevu sana. Mara nyingi umekuwa ni ule wa zimamoto, kama tulivyojionea wenyewe wakati wa ziara ya Rais Obama na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi yetu.

 

Pamoja na uhaba wa vifaa bora na vya kisasa, bado tuna uwezo wa kuendelea kupambana na hali yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wa taifa letu. Kinachotakiwa ni vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha usalama unakuwapo mahali popote. Tuwafichue wahalifu wa aina zote wakiwamo wahamiaji haramu, majangili, majambazi, wauza dawa za kulevya na wengineo. Lakini yote haya yanataka mshikamano na uzalendo.

 

Wamarekani wameweza kuimarisha demokrasia ya kweli, uzalendo wa taifa na leo tunashuhudia wanavyopewa hadhi kimataifa kwa kuitwa taifa kubwa duniani lenye nguvu kubwa ya kijeshi na kiuchumi.

 

Itatuchukua muda mrefu kufika huko lakini hatuna budi kujitahidi kwa kutumia rasilimali watu tulionao.

 

 

0763 – 400283

[email protected]