Majeshi ya vyama vya siasa yafutwe

Kuna haja ya serikali kutafakari upya kwa kuangalia uwezekano wa kufuta majeshi katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuepusha mfarakano wa Watanzania.

 

Ninatoa angalizo hili kwa sababu muundo wa majeshi katika vyama vya siasa hapa nchini unaonekana kuwa na sura isiyo ya moja kwa moja (indirect) ya kupanda mbegu ya uadui baina ya viongozi, wanachama na mashabiki wa vyama hivyo.

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitangulia kuunda na kutangaza jeshi lake linalojulikana kwa jina la Green Guards. Baadaye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nacho kikaunda na kutangaza jeshi lake linafahamika kwa jina la Red Brigade.

 

Vikiwa ndivyo vyama vyenye nguvu kubwa ya kisiasa hapa Tanzania, CCM na Chadema kila kimoja kimekuwa kikitaja kazi ya jeshi lake kuwa ni kulinda usalama wa viongozi na wanachama wake. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kwamba majeshi hayo yamejipachika majukumu ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

 

Hata hivyo, msisitizo mkubwa umekuwa ni kuwa jeshi la Green Guards lipo kwa ajili ya kudhibiti wanachama wa vyama vya upinzani watakaojaribu kushambulia au kuhatarisha usalama wa viongozi na wanachama wa CCM. Vivyo hivyo, jeshi la Red Bregade limetangazwa kujikita katika kuwalinda viongozi na wanachama wa Chadema dhidi ya vitendo vya kushambuliwa na wapinzani wao.

 

Wiki iliyopita, Chadema ilitangaza mpango wake wa kuanzisha kambi katika mikoa yote kwa ajili ya kuwapa walinzi wake mafunzo maalum, yatakayowawezesha kuwalinda viongozi na wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani hapa Tanzania.

 

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alitaja sababu ya kuchukua hatua hiyo kuwa ni baada ya kuona serikali na vyombo vyake vya dola vimeshindwa kushughulikia malalamiko kuhusu mauaji, vitisho na matukio mengine maovu yanayowakumba baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho.

 

“Ni wajibu wa chama kutafuta njia za kujilinda, hatulindwi na Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wala Usalama wa Taifa. Watu wetu wanapigwa na wanauawa, hata tukienda polisi hatupati haki yetu.

 

“Ni bora tuendeshe mafunzo na tujilinde wenyewe kwani tukiendelea kupiga magoti na kulia tutakuwa wajinga,” alisisitiza Mbowe.

 

Kimsingi suala la kujilinda si baya ila madhumuni ya majeshi hayo ya Chadema na CCM yanaonekana kuzungukwa na dhana ya kujenga uhasama baina ya viongozi na wanachama wa vyama hivyo.

 

Lakini kitu kingine cha kujiuliza katika hilo ni kwamba viongozi wa Chadema na CCM hawajapata kutangaza wakufunzi wanaowezesha au watakaowezesha mafunzo ya kijeshi kwa walinzi wa vyama hivyo. Hawajatwambia walimu wa mafunzo hayo wanatoka au watatoka katika majeshi yapi ndani na nje ya Tanzania. Lakini pia, haijabainishwa ni silaha za aina gani zinatumiwa au zitatumiwa na wanajeshi hao.

 

Tunaojua maana ya jeshi tunaamini kwamba watu wanaotumikia majeshi ya vyama hivyo wana silaha za moto. Kwa hivyo, tunaweza kuamini pia kwamba Tanzania haiishii kuwa na Jeshi la Polisi, JWTZ, Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Mgambo pekee.  Hofu nyingine iliyopo ni kuwa vyama vya siasa vinaweza kutumia uhuru wa kujiundia majeshi kupanda mbegu mbaya ya uhasama na mfarakano wa Watanzania, achilia mbali kujihalalishia matumizi holela ya silala za moto.

 

Kwa mantiki hiyo, ninadhani serikali ifike mahali ifanye uamuzi mgumu wa kufuta utaratibu wa kuruhusu vyama vya siasa kujiundia na kumiliki majeshi. Vyama vya siasa virejeshwe katika dhana ya kushindana kwa sera na nguvu ya hoja, lakini pia chachu ya amani na mshikamano, si vinginevyo.

 

Jukumu la ulinzi wa raia na mali zao libakie kuwa la vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinavyotambulika kisheria.

 

 

Please follow and like us:
Pin Share