*Uraia wa nchi mbili haufai, tuuache

Baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa Rasimu ya Katiba mpya kwa wananchi kuitafakari, nchi nzima imelipuka. Natumia neno kulipuka kusisitiza furaha ya wananchi kwa tukio hili.

Wanasiasa wametoa matamko yao juu ya rasimu hiyo. Wazee wameongea vyao juu ya rasimu hiyo. Vijana wamelonga yao, akina mama nao hawakuwa nyuma katika kuelezea furaha yao. Huku ni kudhihirisha wazi wananchi wameipokea rasimu ile kwa mitazamo tofauti. Tumeguswa na namna ilivyoandikwa. Imeleta miale ya matumaini katika Taifa.

 

Wenye kununa, basi na wanune na yao mioyoni lakini wengi wetu tumeridhia na mtazamo wake hasa katika hatua hii ya mwanzo kumekuwa na matumaini makubwa. Rasimu imeunganisha (incorporate) mawazo ya wananchi kadhaa. Nchi ngapi ulimwenguni zimetunga Katiba yake kwa mtindo namna hiyo?

 

Historia    inaonesha tu kuwa baadhi ya nchi zimetunga Katiba zao baada ya kutokea tawala za mabavu. Lakini sisi hatukusukumwa kwa mabavu, bali tumejitafiti na kutafakari kwa amani na utulivu hata kufikia hatua hii ya kujitungia KATIBA MPYA. Ndiyo maana tumechukua hatua za kukusanya mawazo yetu na watalaamu wa Tume wameyapanga na hatimaye imetokea rasimu hii tunayoichambua kwa nia ya kuiboresha tupate Katiba bora ya wananchi.

 

Ningeweza kusema imeonesha mkusanyiko wa mawazo ya makundi yote ya wananchi wa Taifa hili (it is a crosscutting manuscript). Ni hatua nzuri kama mahali pa kusimamia Katiba yetu. Hatuna budi kushukuru na kuwapongeza wanakamati kwa kazi nzuri.

 

Angalizo hapa ni kwamba sisi wachambuzi wa rasimu hii kwa mwonekano tusifanane na wale vipofu watatu katika riwaya ya zamani. Vipofu wale walikuwa wanasikia habari za tembo, ukubwa wake na uwezo wake, lakini kwa ule upofu wao hawakuweza kupata dhana halisi ya tembo bila ya kumwona kwa macho. Siku moja walielezwa kuwa kuna tembo ameuawa karibu na sehemu zile kama walipenda wangeweza kwenda huko na kumuona tembo alivyo. Wote vipofu watatu walikwenda kwa furaha kubwa kumwona tembo alivyo.

 

Walipofika mahali pale tembo alipokufa kila kipofu alifanikiwa kugusa sehemu moja ya tembo yule. Kisha wote watatu wakatoa maoni na ufahamu wao juu ya tembo. Kipofu mmoja aliyegusa sehemu za tumbo la tembo yule alielezea furaha yake na kusema jamani, “tembo kweli mkubwa, ni kama kichuguu pale alipolala”. Kwake kipofu huyu tembo alikuwa mkubwa kweli kama kichuguu.

 

Kipofu wa pili aligusa miguu ya tembo, akaipapasa na kuinyanyua. Huyu naye maelezo yake juu ya tembo alisema, “He he he, kumbe tembo mwenyewe ni kama kinu cha kutwangia”. Kipofu wa tatu yeye alifikia kupapasa sikio na kwa mshangao mkubwa akasema, “Masikini, hivi tembo tunayemsikia kumbe ni kama ungo wa kupepetea tu!”

 

Vipofu wale wote hakuna aliyemwona tembo, bali kila mmoja alifanikiwa kumtambua kwa kupapasa au kushika sehemu fulani ya tembo na sehemu ile kwake kipofu yule ikawa ni picha na tafsiri yake ya tembo!

 

Hadithi hii ya vipofu ndiyo mimi naifananisha na sisi tunaoitafakari rasimu yetu ya Katiba. Kila mmoja wetu anasoma kifungu fulani cha rasimu ya Katiba kisha anakurupuka na tamko juu ya Katiba. Swali langu ni je, tumeisoma rasimu yote kisha kuitafakari kwa ujumla wake (in its totality?) na ndipo tutoe haya matamko tunayotoa wakati huu? Ninavyoona ni kama ile hadithi ya wale vipofu na tembo.

 

Wapo waliosoma kifungu kile cha Serikali tatu wakaanza kutoa maoni, “Mnaona! sisi tulisema hayo tangu miaka ile ya 1990 tulipodai Serikali tatu tukaonekana wakorofi, leo chepi mbona hii rasimu inatuunga mkono?”

 

Wapo wale waliosoma sehemu ya wagombea binafsi kwamba Katiba sasa inasema wanaweza kusimama katika uchaguzi. Basi hawa wanasema, “Jamani sisi tulisema hii ni haki ya kila Mtanzania kuchagua au kuchaguliwa, siyo lazima asimamishwe na Chama fulani. Leo si hayo, rasimu imetuunga mkono! Kumbe madai yetu yalikuwa halali kikatiba!”

 

Wapo wale wa Visiwani waliosema, “Tumeomba Wazanzibari tupatiwe Uhuru wetu sasa chepi? Serikali tatu maana yake huku Visiwani tutakuwa tunatambulika kimataifa (national identity) tutaweza kuwa na kiti chetu kwenye Umoja wa Mataifa, tutaweza kufungua balozi zetu nchi za nje na hata FIFA itatutambua na timu ya Zanzibari hapo na itashiriki michezo ya kimataifa.”

 

Hawa wanadiriki kusema “al-hamdulillah, sasa, Wazanzibari tutapumua, tutakuwa na pasipoti zetu bwana. We acha tu! Tutaachana kabisa na kero za wabara hawa. Tumekuwa tukidai dola yetu Wazanzibari hii rasimu inatukubalia kuwa na dola kamili.”

 

Rasimu yetu hii imetoa changamoto kweli hapa nchini. Watoto wamefurahia, wazee tumefarijika, watu wazima wamefurahia na vijana ndiyo hasa wamerukaruka. Lakini rasimu hii naona imekuwa na mafunzo kwa kila kundi la watu.

 

Kila kundi lina cha kujifunza kutoka kwenye rasimu hii. Lina  cha kuchangia katika rasimu hii na pia lina cha kukosoa kwa maana ya kuboresha rasimu hii. Kwa vyovyote vile, lengo au hatima ya yote hayo ni kupatikana kwa KATIBA MPYA YETU WANANCHI SOTE. Tukifanikiwa tutakuwa tumeandika historia mpya na ya pekee (unique) katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Tutakuwa na Katiba ya watu (popular constitution) wenyewe.

 

Mimi kihistoria napata ugumu fulani. Nchi ya Tanzania mwaka wa sensa (2012) inasemekana tuko jumla ya wananchi zaidi ya milioni 44. Wengi wa wananchi hawa mimi nasema ni Watanzania kwa maana wamezaliwa baada ya Muungano ule wa Aprili 26, 1964. Hebu tufikirie kwa kadiri ya hesabu ya watu ya mwaka 1967 (miaka minne baada ya ule Muungano) Watanganyika tulikuwa 11,958,654; Wazanzibari walikuwa 354,815. Ilipofika mwaka 2002 sisi huku Tanzania Bara tulikuwa 33,461,849; wakati Watanzania Visiwani walikuwa 981,754. (taz. Analytical Report ya Sensa Vol. X tebo No. 1 uk. 1).

 

Hii kwa mtazamo wangu nathubutu kusema leo hii tunapokuwa watu zaidi ya milioni 44, basi idadi kubwa sana ya hawa ni WATANZANIA halisi. Wamezaliwa katika nchi inayoitwa Tanzania. Hawa jamani leo tuwageuze uraia wao tuwaite wengine Watanganyika na wengine eti Wazanzibari itakuja hiyo?

 

Kusema kweli Watanganyika wengi tu wazee; mfano halisi kama mimi niliyezaliwa mwaka 1930 Utanganyika wangu ni wa miaka 33 tu, kumbe kuanzia mwaka 1964 nimekuwa MTANZANIA, hivyo utanzania wangu una miaka takribani 50 leo hii (miaka 49 na miezi 7 hivi). Ni busara kweli Katiba inirudishe kwenye Utanganyika tena? Naweza kusema wananchi wapatao milioni 10 hivi ndiyo Watanganyika na wapatao 300,000 tu ndio Wazanzibari. Wengine wote ni WATANZANIA kwa mujibu wa KUZALIWA KWAO na Katiba inawatambua hivyo.

 

Kwa kule visiwani hivi sana wapo zaidi ya watu milioni 1.5. Lakini wakati ule wa Mapinduzi Wazanzibari walifikia kama 300,000 tu. Hawa laki tatu kweli wanastahili kuitwa Wazanzibari kwa kulingana na agizo lililotolewa na Zanzibar Nationalist Party kule visiwani mwaka 1961 kwamba raia wote wa visiwani waitwe Wazanzibari lisitumike neno Mwarabu/Mshirazi na kwa wengine waitwe machotara Afro-Arab (tazama Historia ya Zanzibar its society and its politics uk. 13 by John Middleton na Jane Campbell).

 

Hivyo, wale wote waliozaliwa baada ya Muungano wa Aprili 26, 1964, siyo WAZANZIBARI, bali ni WATANZANIA. Maagizo ya viongozi wao mwaka 1961 ilikuwa sahihi kuwa na utaifa mmoja kule Visiwani na utaifa ule ndiyo Uzanzibari wao bila kubagua mbari za asili zao (kama uarabu, utumbatu, uhindi, uhadimu na kadhalika).

 

 

 

 

 

 

 

Tazama Ramani ya visiwani mgawano wa wakazi wake wa asili waarabu walikuwa wachache sana sana, lakini ndiyo walikuwa watawala huko enzi zile.

 

Hali ya visiwani mwaka 1960 ilikuwa na wakazi Waafrika 299,000; Waarabu 50,000, Wahindi 18,000 (imenukuliwa kutoka “A History of Zanzibar 1934 – 1964 by S. G. Ayan uk. 34 – EAst Africa Literature Bureau.

 

Kumbe viongozi wetu wazee Abeid Aman Karume na Julius Kambarage Nyerere waliamua jambo jema kabisa la kuunganisha ile Jamhuri ya Tanganyika (Desemba 9, 1962) na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar (Januari 18, 1964) tukawa na muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Aprili 26, 1964. Sisi sote tumekuwa Watanzania.

Sasa kwa historia namna hii kundi hili kubwa la vijana na watu wazima wa nchi hii au Jamhuri hii tuwageuze kuwa Watanganyika na Wazanzibar itakuwa sawa hiyo? Sidhani. Hawajui hiyo Tanganyika ni nini! Kwa nini tuwapakie kasumba ile ya miaka 1958 – 1963 ya Utanganyika na Uzanzibari? Tunafufua ubaguzi!

 

Jambo hili ninaliona na kulilalamikia sana kwa sababu Jamhuri yetu ya Muungano imeshindwa kuwajenga kimalezi ya uzalendo wa kitaifa vijana wa Taifa letu hili na hivyo ‘wajanja’ wamefanikiwa kuwarubuni vijana Wazanzibari kuwa siyo Watanzania. Hapo uzalendo umetushinda. Ningeomba tusome ile hadithi aliyoitoa Mwalimu Nyerere zamani ipo katika kijitabu chake “Uhuru wa Wanawake (by Mwalimu Julius. K. Nyerere uk. 63) Tai aliyelelewa na kuku – hatimaye aligutushwa na mjanja akarubuniwa na hatimaye alipojitambua kuwa kumbe kweli yeye alikuwa Tai wala hakuwa kuku, basi aliruka moja kwa moja.

Tanzania Visiwani – Waarabu wanawaeleza vijana wao kuwa wao siyo Watanzania, bali ni Waraabu waamke waruke kudai Uzanzibari waliopewa na ZNP miaka ile ya 1960 kabla ya Mapinduzi.

 

 

 

Tume iwe angalifu katika mchakato huu wa Katiba mpya kusije kukatokea Uzanzibari na Utanganyika au Uzanzibari na Uzanzibara. Hivi kukiwa na Serikali tatu uraia utakuwaje? Watu watakuwa raia wa Tanganyika na wa Muungano na pia watakuwa na uraia wa Zanzibar na wa Muungano? Kitu namna hii ndicho tulichokikataa tangu siku nyingi tusiwe na uraia wa nchi mbili (Dual citizenship). Hapa Tanzania litaepukwaje hilo katika mazingira ya Serikali tatu? Uzalendo wa taifa lipi utajengwa hapo? Itakuwa ni Katiba ya aina ya pekee kabisa ulimwenguni. Hebu tazama, hata mseto wa kule Uingereza kati ya England, Scotland, Wales na Ireland hauko namna tunayotaka kubuni sisi kwa Katiba yetu mpya hiyo.

Wazee nadhani tunakumbuka mara baada ya Uhuru tuliwahi kuwa na mawaziri wenye asili ya Usia na Uzungu. Watu wale walipofariki dunia hakuna aliyezikwa katika ardhi hii ya Tanzania. Mmoja kwa kuwa na uraia wa nchi mbili alikwenda kuzikwa Canada. Huyu mwingine naye kwa kuwa na uraia wa nchi mbili majivu ya mwili wake aliagiza kabisa yakazikwe Uingereza!

Ndiyo matokeo ya kuwa na uraia wa mataifa mawili. Hiyo jamani ni tabia ya popo ambaye si ndege wala si mnyama. Lakini ana sifa za ndege na za mnyama! Ni madhara ya kuwa na uraia wa mataifa au nchi mbili. Ni kutaka kujinufaisha binafsi na wala siyo kwa maendeleo ya nchi. Je, wanasheria katika Tume mnaliona hilo kiupande huo au mradi sheria za kimataifa zinatafsirika, basi tuzifuate? Tufikirie kiuzalendo Katiba yetu na iwe kweli ya Kiafrika na hasa hasa hasa ya Kitanzania.

 

 

ITAENDELEA…

Please follow and like us:
Pin Share