Kama nilivyoahidi wiki iliyopita, kwamba baada ya kuwa tumemaliza kulizungumzia suala la Muungano kwa urefu na upana, ningeanza kuzungumzia suala la ardhi katika Taifa letu na jinsi Katiba ya sasa inavyolieleza suala hilo na umiliki wake kwa Watanzania.

 

Hebu tuikumbuke dhana ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba ili nchi iendelee, inahitaji Ardhi, Watu, Siasa Safi na Uongozi Bora.

 

Sasa sina budi kulizungumzia suala hili la ardhi ili angalau Watanzania tupate kujua fursa yetu ya kurekebisha matatizo yanayohusu ardhi. Uzalendo wa kweli na wa dhati huzaliwa, hujengwa na kudumishwa pale palipo na heshima katika misingi ya usawa na wananchi kuwa na nafasi katika kumiliki rasilimali za nchi.

 

Swali linalozuka mara nyingi hutokana na wananchi kuhoji mara kwa mara ‘serikali ni nini?’ ile inayoitwa mali ya ‘umma’ kwa kawaida huwa ni ya nani? Ikiwa wawakilishi wa wananchi (Bunge) hawana ruhusa ya kuona, mathalani mikataba ya nchi na wawekezaji, (mikataba ya madini na kadhalika), swali linabaki, je, “umma ni nani?’ na “ mali ya umma ni nini?”

 

Kwanza niseme kwamba ardhi ni rasilimali muhimu sana katika taifa lolote. Tanzania ina ardhi kubwa ukilinganisha na nchi zote za Afrika Mashariki kwa pamoja. Lakini si ukubwa wa eneo (ardhi) tu, bali ni eneo lenye rutuba na kila aina ya madini hata mengine yasiyopatikana kwingine kokote duniani. Ardhi imekuwa ndiyo rasilimali ya kwanza hata kwa mataifa yaliyoendelea, kwani bila ardhi hakuna uwekezaji wa aina yoyote.

 

Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 pamoja na Sheria ya Ardhi ya Kijiji ya mwaka 1999 (The Land Act, 1999 and The Village Land Act 1999), ndizo sheria zinazosimamia masuala yote yanayohusu ardhi. Labda kwanza niseme kwamba ardhi ya Tanzania imegawanywa katika makundi matatu ambayo ningependa Watanzania wenzangu pia wayafahamu.

 

Kwanza ni ardhi ya jumla (general land ); pili ni ardhi ya kijiji (village land ) na tatu ni ardhi ya hifadhi (reserved land).

 

Sasa ardhi ya kijiji ambayo ndiyo sehemu kubwa na ambako ardhi yenye rutuba inapakitikana na madini ya kila aina, ndiko idadi kubwa ya Watanzania wanakoendesha maisha yao; tofauti na sehemu za mijini ambako hakuna madini na ardhi yenye rutuba. Ardhi hii ya kijiji inamilikiwa chini ya Baraza la Kijiji ambalo ndilo yenye kuamua juu ya ardhi ya kijiji husika.

 

Ardhi ya jumla ni ardhi nyingine yote ukiachilia mbali ardhi ya kijiji na ardhi ya hifadhi. Kwa upande mwingine, ardhi ya hifadhi ni yale maeneo ya wazi, hifadhi za mbuga za wanyamapori, hifadhi za maeneo ya misitu na maeneo yote ambayo hayajapatiwa kazi husika kwa muda mwafaka, kwa maana nyingine yanasubiri shughuli za kimaendeleo ya kitaifa.

 

Sasa kwa mujibu wa sheria ya nchi yetu, ardhi yote ni mali ya Watanzania na inamilikiwa na Rais kwa niaba ya Watanzania wote. Lakini pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaweza kubadili matumizi ya eneo moja kwenda eneo jingine kadiri mazingira ya uhitaji yatakavyokuwa. Rais anaweza kubadili kutoka ardhi ya kijiji na kuwa ardhi ya jumla; na vivyo hivyo kutoka ardhi ya hifadhi kuwa ardhi ya kijiji na, au ardhi ya kijiji.

 

Sasa katika suala la umiliki wa ardhi Watanzania wengi na hasa katika suala la umiliki wa rasilimali hii, bado wanakumbwa na matatizo mengi. Matatizo mengi ya ardhi ni kati ya serikali na wamiliki hao, au ni kati ya wanakijiji na wawekezaji. Kwa hapa kwetu Tanzania na hasa ukizingatia suala la uwekezaji ni suala linalopewa kipaumbele. Wawekezaji hawa wanakuja katika ardhi yenye tija.

 

Jambo la msingi kujiuliza ni kwamba, je, lini Watanzania waishi katika ardhi yao kwa amani kwa kutohofia kunyang’anywa inapogundulika ina rasilimali za kutosha? Kwa maeneo kama ya Shinyanga, Kahama, Arusha, Mara, Songea, Arusha na Mtwara tumeshuhudia wananchi wakipokwa ardhi.

Napenda Watanzania tujue kwamba suala la ardhi ni fursa muhimu mno kuzungumziwa kwenye suala la marekebisho ya Katiba yetu ili hatimaye tupate Tanzania tunayoitarajia siku za usoni, na si Tanzania ambayo Watanzania wenyewe hawana uhakika wa ardhi yao katika Taifa lao wenyewe. Lazima kuishi kwa hofu ya kuondolewa na wawekezaji iwatoke wananchi.

 

Ni mambo gani ya kutazamwa ili tupate Katiba nzuri itakayozungumzia rasilimali hii ya ardhi kwa faida yetu Watanzania kwa kuilinda kwa manufaa yetu wenyewe? Tukutane wiki ijayo katika makala hii ya Katiba Mpya Tanzania Mpya.

 

Mwandishi wa makala haya Marco Samwel ni msomaji mahiri wa JAMHURI. Anapatikana kwa simu namba 0762022737; email:mansamwel@gmail.com

 

 

 

1224 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!