Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, amemwagiwa sifa kwa jinsi alivyowabana watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kufanikisha upatikanaji wa mita 85,000 za umeme.

Mbali na mita, Maswi amemwagiwa sifa pia kwa kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuwa na umeme wa uhakika usiokatika kwa saa 24 sasa, na kupunguza moshi na makelele yanayopigwa na majenereta.

Wakizungumza na Gazeti la JAMHURI kwa nyakati tofauti, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamesema kauli aliyoitoa Maswi wakati anaingia katika wizara hayo, imetekelezeka na imethibitisha kuwa kumbe mambo mengi yanawezekana hapa nchini.

“Mimi nilimsikiliza kwenye vyombo vya habari wakati anaingia wizarani hapo. Alisema atahakikisha umeme haukatiki Dar es Salaam. Leo hili kauli hiyo imekuwa kweli. Kubwa zaidi, alituahidi transfoma na tumeipata. Mimi nasema Mungu amjaalie na asante sana,” alisema Julius Mzale, mkazi wa Kitunda, Dar es Salaam.

Mzale alisema tatizo la umeme mdogo lilikuwa limemfikisha mahali jokofu lake nymbani halifanyi kazi, lakini tangu imefungwa tansfoma wiki iliyopita, hadi fundi aliyekuwa amemwita amtengenezee jokofu lake amemwambia asije tena.

“Mwanzo nilidhani jokofu langu limeharibika. Nimenunua stabilizer (kifaa cha kuchunguza mtiririko wa umeme) lakini muda wote ilikuwa inalia jii, jii, jiii, ila tangu transfoma imefungwa mambo yametulia. Kilichonifurahisha zaidi ni kuwa transfoma imefungwa hadi saa nane usiku… sikuzoea kuona hali hii kwa TANESCO,” alisema Mzale.

Denis Vedasto anasema alipata mshangao baada ya wiki iliyopita kupigiwa simu na wafanyakazi wa TANESCO karibu saa moja jioni wakimtaka awaeleze anapoishi wakamfungie mita ya luku.

“Nakwambia haya ni maajabu. Nilishakwenda TANESCO nikawaambia wanirejeshee hela yangu nikanunue solar, lakini juzi nilipopokea simu wakasema wanataka niwaelekeze kwangu wanifungie mita sikuamini. Kwanza TANESCO huwa hawafanyi kazi baada ya saa 11 jioni, sasa juzi wamefunga mita usiku kwangu, ama kweli huyu Katibu Mkuu abarikiwe,” alisema Vedasto.

Fundi umeme Jason Trasias anachokishuhudia kwa sasa haamini macho yake. “Juzi Kitunda kulikuwa na magari saba yanatafuta nyumba hadi uchochoroni kuwafungia wateja mita. Kama kuna mtu atalalamika kuwa hajapata mita, basi kutakuwa na tatizo fulani,” alisema Trasias.

Katika maeneo ya Mtoni Mtongani na Mbagala imeelezwa kuwa umeme umetulia kwa kiwango cha kufurahisha.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema kuwa Mameneja wa Mbagala na Kigamboni wamefukuzwa kazi baada ya kuzembea katika kazi ya kuwafungia mita wateja.

Tofauti na muda uliopita, maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam kwa sasa hakuna tena kelele za majenereta au moshi utokanao na majenereta hayo.

Tangazo la Katibu Mkuu lililochapishwa kwenye gazeti hili, linawataka wananchi wote waliolipia mita za umeme hadi Mei 31, mwaka huu ikiwa watakuwa hawajafungiwa mita ifikapo Juni 30, wapeleke taarifa kwake yeye Katibu Mkuu na watendaji wakuu wa wizara kisha hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya waliokwamisha ufungaji mita. Soma tangazo hilo.

1320 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!