Mawaziri wagombana

*Naibu Waziri adaiwa kumhukumu Kagasheki wizarani

 *Atajwa kutoa matamshi ya kumkejeli huko TANAPA

*Waziri asema atamhoji, yeye asema  wanawachonganisha

 

MGOGORO mzito unafukuta ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo sasa kuna msuguano mkali kati ya Waziri Khamis Kagasheki na Naibu wake, Lazaro Nyalandu.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Wizara hiyo, zinasema kuwa Kagasheki amepata taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji waliokuwa na watu mbalimbali walikuwa Arusha kwenye kikao alichokiendesha Nyalandu kati yake na maafisa wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), alipomkejeli Kagasheki hivi karibuni.

“Katika Mkutano huo, Nyalandu alipoulizwa na wafanyakazi wa TANAPA juu ya hatua ya Waziri Kagasheki kusimamisha watumishi wanne wa TANAPA na askari 28, alisema ‘Waziri alikurupuka.’ Alisema ‘kama Waziri angeshauriana na yeye (Nyalandu) wala asingewasimamisha wafanyakazi hao,” kilisema chanzo chetu.

Wafanyakazi hao huku wakimshangilia Nyalandu, kwa mujibu wa taarifa hizo, walimuomba Nyalandu awafikishie taarifa zao kwa Rais Jakaya Kikwete aweze kuwarejesha wenzao kazini kwa kile walichosema Waziri kisheria hana mamlaka ya kuwasimamisha kazi.

 

“Kwa kweli walipofikia hatua hiyo ya kumuomba awafikishie salaam zao kwa Rais Kikwete, yeye hakutoa kauli ya kukubali au kukataa kwani hii ingekuwa kumsambaratisha Waziri wake moja kwa moja, ila wapo wafanyakazi aliowambia kuwa yeye yuko karibu na Rais Kikwete hivyo wasiwe na wasiwasi atalishughulikia na kulimaliza kwa njia anazozifahamu yeye,” kilisema chanzo chetu.

 

Kusimamisha watumishi

 

Mei 28, 2012 Kagasheki alikutana na waandishi wa habari na kuwajulisha kuwa amewasimamisha kazi watumishi wanne wa TANAPA na walinzi 28 kupisha uchunguzi baada ya faru wawili kuwa wameuawa katika mazingira ya kutatanisha.

Waliokumbwa na panga la Kagasheki ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi Tanapa, Justin Hando, Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Mtango Mtahiko, Mkuu wa Kitengo cha Intelejensia Tanapa, Emilly Kisamo na Mratibu wa Miradi ya Faru Serengeti, Mafuru Nyamakumbati.

 

Walinzi 28 aliowasimamisha ni Askari Mwandamizi Fatael Mtu, Rashid Athuman, Mohamed Athuman, John Fabian, Goodchance Msela, Joseph Darus, Emmanuel Ishalila na Felician Gwangu ambao wote ni askari wa daraja la pili.

 

Wengine ni Jafari Hassan, Malale Mwita na John Urio, ambao ni askari wa daraja la tatu wakati wa daraja la nne ni Majuto Omari, Deogratias Waisiku, Chacha Ndege, Samson Njoghomi, Leonard Kunjumu, Siad Mkamba, Paul Cosmas na Gabriel Ngazama.

 

Wapo pia Rajab Mangachi, Adam Likarawe, Anodisu Mushumali, John Zimbi, Drigue Shaabani, Rashid Mangandali, Edson Mbyazi, John Mbilizi na Emmanuel Kilawe.

 

Wakati wa kuwasimamisha Kagasheki alisema: “Faru wameuawa tangu mwezi Aprili mwaka huu, lakini TANAPA walisema tukio hilo walilijua, lakini hawakutoa taarifa kwa wizara kitu ambacho kinatia shaka kwamba huenda kuna baadhi yao walihusika kwa namna moja au nyingine katika tukio hili.” Aliahidi kuunda Tume ya kuchunguza tukio hili.

“Kumetokea mabadiliko ya mawaziri na sababu ni nyingi, katika wizara hii ya Maliasili na Utalii kuna sura ya wizara imejengeka kwamba kuna uchafu mwingi, wengine wanasema hii ni wizara ya mali za siri wakimaanisha kwamba vitendo vichafu vinafanyika katika wizara, lakini wahusika hawachukuliwi hatua.

“Hii vita siyo ndogo ni kubwa lakini naahidi tutapambana, maana haiwezekani tukio limetokea mwezi Aprili mwaka huu halafu wahusika wamenyamaza kimya tu hawatoi taarifa. Nahisi kuna uhusiano wa tukio hilo na baadhi ya watumishi waliosimamishwa,” alisema Kagasheki.

 

Kauli ya Kagasheki

 

Baada ya Jamhuri kupata taarifa hizi, liliwasilkiana na Kagasheki kujua iwapo taarifa hizo za kubezwa amezipata na kufahamu ni hatua zipi atazichukua dhidi ya Naibu wake Nyalandu.

 

“Hata mimi nimezisikia hizi taarifa, na kwa sasa Naibu Waziri yuko safarini nje ya nchi (India), hivyo sijawasiliana naye, namsubiri akija hapa Dodoma nitamhoji na kumtaka anipe ukweli wa kauli hii ikiwa ameitoa kweli kwamba nimekurupuka, na baada ya hapo nitajua la kufanya. Siwezi kusema zaidi ya hapo ngoja nikutane naye kwanza,” alisema Kagasheki.

 

Nyalandu azungumza

 

Jamhuri lilimtafuta Nyalandu na kufanikiwa kuzungumza naye mwishoni mwa wiki, ambapo alikana kutoa kauli hiyo akisema kuna mkono wa wachonganishi, ila akakiri kukutana na uongozi wa TANAPA ingawa alisema mkutano wao ulihusu usuluhishi kati ya TANAPA na Otterlo waliopelekana mahakamani.

“Kaka mimi ni mwanasiasa mkongwe, nimekuwa bungeni kwa miaka 15 sasa. Inahitaji kutumia common sense tu kufahamu kuwa siwezi kutoa kauli kama hiyo. Hiyo ni complete fabrication (yakutengenezwa). Sijawahi kukutana na wafanyakazi wa TANAPA isipokuwa nilikutana na uongozi wa TANAPA, ambao nilikwenda kuwasuluhisha kutokana na mgogoro wao na Otterlo waliokuwa wamepelekana mahakamani.

“Nitakuwa mjinga sana kama nitatoa kauli kama hii. Hapa katikati nimeona gazeti moja likisema nawaandalia wawindani mkutano mwezi Juni na nimewakutanisha na Waziri, nasema huu ni uchonganishi. Nadhani kuna watu wanataka kutufanya tugombane mimi na waziri wangu tusiwe tunasalimiana.

“Wanasema eti mimi nampelekea Waziri wawindaji, mimi nasema simjui hata mwindaji mmoja na wala sijawahi kuwinda. Nadhani litakuwa jambo jema tukizungumza uso kwa uso (na Waziri Kagasheki) nimweleze nia yangu safi.

“Ukiangalia mara nyingi mimi namshauri Waziri that we even need to go further (tunastahili kwenda mbali zaidi) katika uamuzi anaoufanya. Mimi I’m not confrontational (si mtu wa mapambano). Nina common sense (akili ya kuzaliwa) ya kutosha kaka kutofanya mambo kama hayo… nimetoka India, nakwenda Dodoma kisha Urusi, nitawasiliana na Waziri tuzungumze,” alisema Nyalandu.

 

Otterlo wamruka Nyalandu

 

Hata hivyo, kampuni ya Otterlo Business Corporation Ltd (OBC), imepinga madai ya Nyalandu kwa kusema haina na haijawahi kuwa na mgogoro na TANAPA.

Mkurugenzi Mtendaji wa OBC, Isaack Mollel, ameiambia JAMHURI kwamba kwa miaka yote ya uwepo wa OBC, TANAPA imekuwa ikiwapatia ushirikiano wa hali ya juu.

 

“Hatuna ugomvi kabisa, tena tumekuwa tukishirikiana na TANAPA katika oparesheni za kukabiliana na majangili, wamekuwa wakitupatia ushirikiano wa hali ya juu sana. Nakuhakikishia kuwa hatujawahi kugombana, na wala hatuna ugomvi kabisa. TANAPA ni wadau wenzetu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ujangili, tunashirikiana nao sana kwenye uhifadhi,” amesema Mollel.

 

 TANAPA washangaa

 

Kwa upande wao, TANAPA walipotakiwa kuzungumzia mkutano kati yao na Nyalando na Otterlo, walisema hawajawahi kuwa na mkutano wa aina hiyo.

Msemaji wa TANAPA, Paschal Shelutete, alisema: “Jamani mimi sina taarifa hizi hata chembe. Nina uhakika asilimia 100 hapajakuwapo mkutano kama huu. Otterlo hatujawahi kuwa na ugomvi wowote na wala sijawahi kushiriki kikao hicho. Sijakisikia kabisa.”

 

Mwelekeo wa Nyalandu

 

Kwa muda mfupi alioteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu amekuwa na uhusiano wa karibu mno na wamiliki kadhaa wa vitalu vya uwindaji wa kitalii.

Akiwa bado hata hajaapishwa, tayari alishakutana na wamiliki kadhaa na kufanya nao mazungumzo.

Baadaye, Nyalandu alifanikisha mkutano kati ya Waziri Kagasheki na viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA). Viongozi hao walipitia kwa Nyalandu kufika ofisini kwa Kagasheki.