Ushindi ni mtihani. Si kila anayepata ‘A’ darasani atapata ‘A’ katika maisha. Si kila anayepata daraja la kwanza kwenye mitihani atapata daraja la kwanza kwenye maisha. Ushindi ni mtihani.

Katika kila kushindwa kuna mbegu za ushindi, na katika kila ushindi kuna mbegu za kushindwa. Kauli hii iliwahi kutolewa na mwanadiplomasia na makamu wa 42 wa Rais wa Marekani, Walter Mondale.

Mbegu za ushindi zipo katika kila kushindwa, kwa maana kukosa njia ni kujua njia. Mbegu za kushindwa zinakuwa katika kila ushindi pale mtu anapobweteka na kufurahia fungate la ushindi.

Yupo aliyesema: “Afadhali nishindwe katika shughuli ambayo najua siku moja nitashinda kuliko kushinda katika shughuli ambayo najua siku moja nitashindwa.”

Fahamu namna ya kutumia ushindi wako. Mwanahistoria aliyezaliwa 200 K.K, Polyybius, Mgiriki alisema kwamba watu ambao wanajua namna ya kushinda ni wengi sana kuliko wale ambao wanajua namna ya kufanya matumizi sahihi ya ushindi wao.

Nini kifuate baada ya ushindi, ushindi unahitaji utulivu na umakini. Wagiriki walipowashinda Waajemi mwaka 490 K.K, Pheidippides – mkimbiaji mashuhuri alikimbia maili ishirini na tano kwenda mji wa Athens kupeleka habari za ushindi. Alipowasili amechoka, alisema kwa shida: “Furahi, tumeshinda,” alianguka na kuaga dunia pale pale. Ushindi ni mtihani.

Panga mipango na kuitekeleza kutokana na ushindi wako. Ukishinda usibweteke, ushindi upo katika wakati uliopita. Unaweza kufanya vizuri zaidi, endelea kujipanga katika maeneo yote, endelea kuongeza ujuzi, endelea kuongeza elimu. Elimu haina mwisho.

Ukiwa unabanika na kuchoma nyama upande mmoja ukiiva unageuza upande mwingine. Kama umeiva katika ujuzi fulani, geuza upande wa pili. Wewe kama ni mzuri katika kuuza, angazia na uwezekano wa kuzijua vizuri sheria.

“Kama umeshindwa kuwa na matumaini kuwa utashinda, moyo wako uweke kwenye ushindi. Matumaini ni mwanzo. Lakini matumaini yanahitaji kitendo kuweza kushinda,” alisema David Joseph Schwartz, Profesa wa Marekani na mtunzi wa kitabu ‘The Magic of Thinking Big’ (1959).

Matumaini bila vitendo ni kama jua bila mwanga, ni mti wa matunda bila matunda, ni kisima cha maji bila maji.  Kubali kushindwa na kufanyie kazi kushindwa. Asiyekubali kushindwa si mshindani.

“Kama hushindwi, huwezi kufurahia ushindi. Hivyo nakubali vyote viwili,” alisema Rafael Nadal, mchezaji mashuhuri wa mpira wa tenisi. Kushindwa ni vijilia ya kushinda. Diamond Dallas, muigizaji mashuhuri alisema: “Baadhi ya matukio ya ushindi wangu yamekuja moja kwa moja baada ya matukio makubwa ya kushindwa.”

Zipende changamoto ni daraja la kukupeleka kwenye ushindi.  Zifanyie kazi changamoto, ni fursa ya ushindi. Victoria Arlen, muigizaji mashuhuri alisema: “Nilijifunza mapema kuwa changamoto zisizo za kawaida zinasababisha ushindi usio wa kawaida.”

Kuna watu ambao huzungumzia ushindi kama suala la bahati, ushindi ni suala la kupanga, ushindi ni suala la kazi. Huwezi kupanga kushindwa, lakini kutopanga ni kupanga kushindwa. Kama unapata matatizo lakini ukijua kuna uwezekano mkubwa wa kushinda, unayaangalia matatizo kwa mtazamo chanya, kwa vile kuna uwezekano mkubwa wa kushinda.

Boresha mbinu za kuendeleza ushindi. “Wakati mwingine zawadi ya ushindi hailingani na gharama, njia tunazotumia kufikia ushindi ni muhimu kama ushindi wenyewe,” alisema Brandon Sanferson.

Jali mambo madogo madogo katika kutafuta ushindi.  Kuna aliyesema: “Mlango ni mdogo ukiulinganisha na nyumba, ufunguo ni mdogo sana kati ya vyote, lakini ufunguo unaweza kufungua nyumba yote. Hivyo suluhisho dogo lililofikiriwa linaweza kutatua matatizo makubwa.”

Ukipata wazo ambalo ni suluhisho la tatizo lifuatilie hadi mwisho.

Muingize Mungu katika ushindi wako. “Hakuna jambo ambalo linashindwa kabisa kama mafanikio bila Mungu,” alisema Vic Pentz.

Mtegemee Mungu na tembea na Mungu, kwa vile unapanga na Mungu anapanga.

Please follow and like us:
Pin Share