Ndugu Rais, serikali ni sawa na mwanadamu. Haiwezekani kila kinachofanywa na serikali kikawa ni kibaya. Yako mazuri yanayofanywa na serikali. Na kuna maovu yanayofanywa na serikali. Hii ni kwa serikali zote – siyo hapa kwetu tu. Timamu hasifii kila jambo linalofanywa na serikali, na wala timamu hakosoi kila jambo linalofanywa na serikali. Timamu hushauri katika kweli na kwa nia njema bila kuchoka. Wenye masikio ya kusikia husikia. Vimbulu wakaendelea.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Tanganyika na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye amepewa heshima ya kuitwa Baba wa Taifa hili, alikuwa ni mwalimu wa kuzaliwa. Bahati haijawa njema kwetu kwamba katika marais wote waliokuja baada yake hakuna wa kumlinganisha naye. Si kwa unyofu wake na ucha Mungu wake wa kweli, bali hata kwa mapenzi yake makubwa aliyokuwa nayo kwa wananchi wa nchi hii na kwa nchi yake. Uzalendo wake haukuwa wa mdomoni. Mzalendo wa kweli hajijui kama ni mzalendo. Anayejitangaza mwenyewe anakiri kuwa huyo si mzalendo.

Rais Julius Kambarage Nyerere alitumia muda wake mrefu kutufundisha Watanzania kama wanafunzi wa darasa lake. Alitufundisha kuwa nchi yetu Tanzania ina maadui watatu. Akiwataja kwa mfuatano wa uzito alisema, ujinga, maradhi na umaskini. Hakututajia wakoloni au mabeberu kama wanavyopwayuka siku hizi. Kwa kuzingatia uzito huo huo Rais Nyerere aliweka juhudi kubwa katika kutoa elimu. Tangu elimu kwa wote (UPE) hadi  ngumbaru, kisomo cha watu wazima. Alijua na kuamini kuwa angefaulu kuwapatia wananchi wake elimu wale maadui wawili, maradhi na umaskini wangekimbia wenyewe kwa sababu elimu ni silaha nzito. Kwa kodi yao hiyo hiyo Rais Nyerere aliwatibia Watanzania wote bila kutoza ziada yoyote. Leo madaktari ni mabingwa wa kuwaandikia wagonjwa, dawa wakajinunulie wenyewe. Labda ahadi ya milioni 50 kwa kila kijiji kama itaheshimiwa na haitakuwa hewa itasaidia. Elimu na matibabu alivyotoa Rais Nyerere vyote vililipiwa kwa kodi yao. Si elimu wala si matibabu hakuna kilichotolewa bure!

Rais Nyerere aliwapatia wana wa nchi hii elimu bora tangu ya awali hadi elimu ya juu bila kuwatoza fedha zaidi ya kodi waliyolipa.

Tukubali, tuliosoma wakati wa Rais Nyerere tulisoma kwa kujinafasi.

Vitabu bora vya kumwaga. Walimu waliohamasika na madarasa na madawati kwa kila mwanafunzi. Vidau, wino, nibu, rula, penseli na mfuto Rais Nyerere aligawa katika kila shule bila kutoza ziada ya kodi. Mtu huyu alikuwa mcha Mungu wa kweli bila unafiki. Hakumlaghai Mtanzania yeyote kuwa alitoa elimu bure. Kwa unyofu wake alijua kuwa kuwaambia Watanzania anatoa elimu bure ingekuwa ni kuwadanganya. Kwa dini yake kusema uongo ni dhambi. Rais Nyerere hakuwa tayari kuitenda dhambi hiyo.

Waziri mwenye dhamana ya elimu ya nchi hii kukiri hadharani kuwa baadhi ya vitabu wanavyotumia watoto wetu kujipatia elimu shuleni ni sawa na matangopori, ungekuwa wakati wa Rais Nyerere, huyu angefanana na mtu aliyemeza wembe. Tungekwishamsahau. Kauli ya waziri imeachwa ipite kama maji yapitavyo mferejini. Nani anajali? Kwa wingi wa pesa zilizotumika katika kuchapisha vitabu-sumu (vitabu matangopori) na kisha kuvikusanya na kuvichoma moto kwa gharama nyingine, halafu vikachapishwa tena vitabu-sumu vingine kwa pesa nyingine ambavyo navyo ni vya kuteketezwa, aliye na hofu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu hawezi kufikiria kuingia katika uchaguzi ujao. Kuwaomba kura wazazi ambao watoto wao hawana vitabu huku wakikaa chini wakati kodi wamelipa, ni kuwasanifu. Hakuna kiongozi wa juu yake aliyeonyesha kushtushwa na kauli ile. Hata ilipotangazwa kuwa wanafunzi licha ya kufaulu wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa na madawati, hakuna kiongozi aliyetikisika. Nenda Baba Nyerere, nenda! Iko siku baadhi ya viongozi uliotuachia watakukumbuka kama tunavyokukumbuka sisi! Ukishaua elimu, yote uyafanyayo ni ubatili mtupu!

Baba umetwambia mwenyewe kuwa Watanzania siyo wajinga sana. Wanajua kuchambua na ‘kuanalaizi’ mambo. Hili la elimu kupuuzwa Watanzania wameli-‘analaizi’ na kulichambua kwa makini. Wanalipa kodi watoto wao wanasomea chini huku mambo makubwa yakifanyika kwa fedha hizo hizo. Kwa hakika mioyo yao baba, haiwezi kuwa ‘clear’. Wakiwasikia wanaosema Mwenyezi Mungu akiwajalia uwezo, watakuja na vipaumbele vitatu; kipaumbele cha kwanza kitakuwa ni elimu. Kipaumbele cha pili kitakuwa ni elimu na kipaumbele cha tatu kitakuwa ni elimu; wanaomba wakati huo ufike mapema wafarijike. Baba hapendwi mtu hapa, lakini fikra pevu kama hizi zinawasukuma timamu kuzikumbuka fikra pevu za Rais Nyerere.

Wakati Watanzania wanaambiwa kuwa Rais Thomas Sankara aliendesha baiskeli yake kwenda vijijini kukagua miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake, baba katika ziara yako hii ndefu hukuonekana popote ukiwa katika kijiji ukishiriki maisha halisi ya wananchi. Kila ulipoonekana pamepambwa. Unaweza ukadhani ni Bustani ya Edeni. Ukifika Morogoro lazimisha wakupeleke ukaione Shule ya Kasanga iliyoko Kata ya Mindu. Wanafunzi wa darasa la tatu 262 wamerundikwa katika darasa moja huku wakiwa wamekaa chini.

Mwalimu anapoingia darasani, anakosa hata sehemu ya kukanyaga kwa ajili ya kuandika ubaoni kwa kuwa wanafunzi wamejaa kila eneo darasani.

Mwanafunzi wa darasa la tatu, Neema Justine atakuambia kuwa wamekuwa wakikaa kwa kukunja miguu, kulala na kuinama wakati wakitafuta njia bora ya kuandika; jambo ambalo linawakwaza kitaaluma.

Baba, hawa watoto wana akili. Wana uwezo wa kuchambua na ‘kuanalaizi’ mambo. Wanaposikia tambo kuwa serikali ya awamu ya tano inafanya mambo makubwa kama kununua ndege nyingi kwa mpigo na sasa inajenga treni ya mwendokasi huku wao wakiachwa katika hali hii ya kuhuzunisha, mioyo yao haiwezi kuwa ‘clear’. Ukiwaendea watoto hawa katika hali hii yao duni ukawaambia haya makubwa yanayofanyika, ndiyo maendeleo, itakuwa vigumu kukuelewa.

Hata yangefanyika makubwa kiasi gani, kama hayagusi maisha ya wananchi hawa duni, basi hawataacha kusononeka. Na kwa hakika haya yanayofanyika, kwao wanao si maendeleo yao, bali ni ya wenye uwezo kiuchumi na kimamlaka!

By Jamhuri