Masuala yoyote yanayohusu taifa letu yasipoendeshwa kwa mtazamo chanya, hasa wa kifikra na kivitendo, tusitarajia kuwa na taifa lenye amani, upendo na umoja – tunu ambazo huzaa maendeleo ya taifa lolote duniani.

Maendeleo huletwa na watu kwa kutumia rasilimali walizonazo. Endapo katika eneo husika watu hawapendani, katu hawataweza kutumia vizuri rasilimali walizonazo kwa manufaa ya wengi.

 

Hakuna upendo, hakuna amani. Katika hali kama hiyo wajanja wachache hutumia udhaifu uliopo kujinufaisha na itachukua miongo kadhaa kubaini ujinga mliofanya leo, mchana kweupe.

 

Naanza makala haya kwa angalizo na tahadhari kubwa ili nami nisije nikatumia kauli za wanasiasa waliolewa madaraka na kujikuta wanaropoka maneno bila kuwa na tahadhari na kauli zao kwa jamii.

 

Leo nazungumzia kauli za Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema (Mb), na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pamoja na zile za Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye.

 

Wote hawa ni viongozi wa ngazi za juu ndani ya vyama vyao. Ni miongoni mwa viongozi ambao baadhi ya wananchi na wanachama wao, siwezi kusema ni watu wote, sitakuwa mkweli, wamekuwa wakiwaamini hasa kutokana na kusimamia misimamo ya vyama vyao.

 

Lakini kutokana na kauli walizozitoa hivi karibuni baada ya mlipuko mwingine wa bomu mkoani Arusha, hakika nimeanza kuwa na wasiwasi juu yao. Sina uhakika endapo huwa wanatathmini athari ya kile kitakachotokea vinywani mwao kwa taifa.

 

Kauli za viongozi wa kisiasa huwagusa watu wote, wanachama na wasio wanachama wa vyama vya kisiasa. Hivyo, kauli ambazo haziruhusiwi kuchujwa kwa kufikiri kwanza, kauli za ushabiki, jazba, chuki, zenye mashaka, uchochezi hakika hazina dalili njema kwa taifa letu hata kidogo.

 

Kufuatia tukio la mlipuko wa bomu Arusha, viongozi mbalimbali wametoa kauli zao juu ya tukio hilo baya kabisa katika historia ya nchi yetu.

 

Mbowe amediriki kuliambia taifa muda mfupi tu baada ya tukio kwamba ana ushahidi wa kutosha na anamtambua mtu aliyehusika, kwa kusisitiza kabisa bila kupindisha kauli kuwa aliyehusika ni askari wa FFU, na tayari wana ushahidi wa picha za video.

 

Sina tatizo kama ushahidi anao, lakini najiuliza: Je, ni ushahidi wa kweli? Je, endapo ikibainika aliyehusika si askari wa FFU, atakubali kubadili kauli yake? Mtu yeyote mwenye nia mbaya anaweza kujibadili asitambulike. Hivyo, adui anaweza kuvaa mavazi yanayoweza kudanganya mkusanyiko wa watu.

 

Pale kulikuwa na mkutano na walinda amani na usalama ni polisi. Hivyo, adui angeweza kutumia mbinu yoyote ile ya kiuhalifu mojawapo ikiwa hiyo ya kuvaa sare za Polisi au Jeshi. Mara ngapi tumesikia watu wakikamatwa kwa utapeli, kwa kutumia sare za Jeshi la Polisi au Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)?

 

Unapolipaka matope Jeshi la Polisi kwa kuuambia umma kuwa ndiyo wahusika wakuu, unatengeneza chuki baina ya wananchi na polisi. Chuki hii ilijidhihirisha pale polisi walipofukuzwa na wananchi kwa mawe na kuwalazimu kutumia silaha za moto na mabomu ya machozi.

 

Narudi nilikotoka. Ukipoteza tunu mojawapo hakuna maendeleo. Vurugu za Arusha zimeharibu mali za watu vikiwamo magari na pikipiki. Sasa hayo ni maendeleo au ni kutaka kuwarudisha watu nyuma?

 

Tukumbuke kuwa tukio la bomu halikuwa vurugu kwa kuwa ni tukio ambalo limetokea bila matarajio ya waliokuwapo mkutanoni. Lakini vurugu zilizotokea baadaye ni matokeo ya kauli za viongozi wa kisiasa waliokuwa katika eneo husika, hasa Mbowe aliyewalenga moja kwa moja polisi kwamba ndiyo wahusika wa tukio hilo. Katika hilo wananchi walipoteza imani na polisi hao na kusababisha vurugu.

 

Hayo ni ya Mbowe. Sasa jingine ni hili alilotamka afisa wa juu kabisa ndani ya CCM, kada mahiri anayeelekea kumezwa na mbwembwe za madaraka. Huyu si mwingine yeyote bali ni Nape Nnauye. Yeye ametamka bayana kuwa ChademaA ndiyo wahusika wakuu wa mlipuko wa bomu uliotokea Arusha na kusababisha watu wanne kufariki na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa vibaya.

 

Hapa napo napata mashaka kuhusu kujiamini kwa kiongozi huyo. Amejigeuza mwanausalama, polisi na mahakama. Mahakama ndiyo sehemu inayotoa hukumu.

 

Sasa Nape ametoa uamuzi ambao ungetolewa na wanaotafsiri sheria. Je, kauli yake ataifuta kwa mtindo gani endapo itabainika alichonena si cha kweli? Je, CCM na Chadema ni vyama visivyokuwa na miiko na kanuni za uongozi? Nasema hivi kwa kuwa siku hizi kila kiongozi hutamka atakavyo bila kuchuja anachokitamka.

 

Nimefurahishwa na kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari. Tendwa alisema bayana kuwa hivi vyama vinaelekea pabaya. Yeye kama Msajili ameliona hilo na kutoa tahadhari kwa wahusika kuhusu hatima ya chama cha siasa kisichofuata taratibu na kanuni za uendeshaji wa vyama vya siasa. Adhabu kubwa kabisa inayoweza kutolewa ni kufutiwa usajili.

 

Hivyo basi, kwa mtazamo wangu, nilitarajia viongozi wa kisiasa baada ya tukio lile la kigaidi, walitakiwa kuweka kando itikadi zao na kuungana pamoja ili kuweza kubaini adui.

 

CCM na Chadema wanaweza kunyoosheana vidole kwa kutafutana uchawi, kumbe adui akawa ni wa kutoka nje ya nchi. Serikali lazima itumie rungu lake katika kusimamia sheria za nchi, isiruhusu viongozi wachache kutaka kuivuruga nchi.

 

Watanzania wote hatuna budi kujiuliza kuhusu chanzo cha matukio haya ya ugaidi yanayoanza kushamiri hapa nchini. Je, ni sisi wenyewe tunataka kumalizana au kuna ajenda ya siri kutoka nje ya nchi yetu? Je, bado tuna marafiki wa kweli wanaotuzunguka? Je, sera zetu za ndani na nje zinaungwa mkono na wote au tuna wapinzani?

 

Ebu tuwaache wachunguzi wa masuala ya usalama wafanye kazi yao barabara na hatimaye ukweli wa jambo hili utabainika.  Lakini rai yangu kwa serikali ni kuihimiza iharakishe uchunguzi wa matukio haya makubwa ili kuwaondolea wananchi hofu. Mathalan, uchunguzi wa bomu lililolipuliwa kanisani bado unaendelea na watu hawajui hatima yake.

 

Sasa tunao mashahidi wa mlipuko uliotokea katika mkutano wa Chadema, nao ni Mbowe na Nape. Mbowe amesema ataupeleka ushahidi kwenye tume huru, hana imani na polisi wetu na vyombo vya usalama kwa ujumla wake. Sasa serikali ikilipuuza suala hili hatutafika mbali.

 

Badala ya kuunda tume, serikali iwabane mashahidi hao waeleze umma wa Watanzania ukweli walionao. Tusifanye mzaha kwa masuala mazito kama haya.

 

Mungu ibariki Tanzania, Mungu tuepushe na hili balaa.

 

0763 400283

[email protected]


Please follow and like us:
Pin Share