Kesi ya Sabaya yapamba moto

ARUSHA

Na Hyasinti Mchau

Kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, inaingia katika wiki ya mwisho ya kusikilizwa mfululizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odera Amuru.

Tayari mashahidi kadhaa wamekwisha kufika mbele ya mahakama hiyo na wiki iliyopita ilikuwa zamu ya Diwani wa Sombetini, Bakari Msangi, kutoa ushahidi.

Mapema mwaka huu JAMHURI liliripoti taarifa ya Sabaya kuvamia duka la mapazia lililopo jijini Arusha, likimnukuu Msangi akidai kuteswa na kundi la vijana wa Sabaya.

Katika kesi inayoendelea sasa ikivuta hisia za wengi, Sabaya na washitakiwa wenzake wanatetewa na mawakili sita wakiongozwa na Wakili Duncan Ohola.

Wiki iliyopita, mawakili hao walijikuta katika wakati mgumu kutokana na ushahidi wa upande wa mashitaka kutolewa kwa ufasaha kuhusu tukio la kuvamiwa kwa duka linalofahamika kama Shaidi Store lililopo Mtaa wa Wapare, Arusha.

Shahidi wa kwanza wa kesi hiyo, Mohamed Hajirin, ameieleza mahakama kuwa siku ya tukio, alikuwa amesafiri kwenda shambani kwake Simanjiro, Manyara; akapata taarifa ya kuvamiwa dukani kwake, aliporudi akalazimika kuihamishia Kenya familia yake, kuhofia misukosuko waliyoipata baada ya Sabaya na kundi lake kuwavamia Februari 9, mwaka huu.

Anasema alipata habari za kuvamiwa dukani kwake na baadaye nyumbani kwake, jambo lililomsikitisha.

Alipoulizwa na mawakili wa Sabaya aliwezaje kwenda Kenya katika kipindi hiki cha ugonjwa wa corona, akajibu hakukuwa na tatizo kwani anamazoea ya kwenda nchini humo.

Shahidi wa pili, Norman Jasin, mjomba wa mwenye duka na muuzaji wa duka hilo, ameieleza mahakama kuwa walipovamiwa Sabaya alidai kuwa duka hilo linajishughulisha na biashara ya kubadili fedha za kigeni kinyume cha taratibu.

Anasema alipigwa vibaya na vijana wa Sabaya bila sababu ya msingi.

“Siku hiyo alikuja dada mmoja akisema anatoka Kenya, anaomba kununua mapazia kwa dola kwa kuwa hana pesa za Kitanzania. Nikamwambia aende benki kubadilisha pesa ndipo aje kununua mapazia,” anadai Jasin.

Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavida, Jasin anadai kuwa dada huyo alirejea tena saa 11 jioni akiwa na dola za Marekani 75, akitaka tena kununua pazia na wakati anazionyesha fedha hizo ndipo Sabaya na wenzake watano walipoingia dukani na kuanzisha madai kwamba duka hilo linabadili fedha za kigeni na baada ya kukataa, akaanza kupigwa.

Sabaya na kundi lake wakamtaka kumpigia simu mmiliki wa duka afike dukani, lakini alipojaribu hakumpata, badala yake akampata Hajarin Saad, naye alipofika dukani akawekwa chini ya ulinzi, akapigishwa magoti na kupigwa.

Anadai kuwa alitishiwa bastola na walinzi wa Sabaya waliofanikiwa kuingia sehemu anayohifadhi fedha; wakachukua kiasi cha fedha walizokuwa wameuza kwa siku hiyo.

Baadaye walikuja kugundua kuwa fedha zilizochukuliwa ni Sh milioni 2.3.

Wakili wa Sabaya akamuuliza alitambuaje kuwa alichokiona ni bunduki? Akajibu kwamba anaitambua kwa sababu amewahi kuona bastola.

Alipoulizwa sababu za mmiliki wa duka kutopokea simu, Jasin, kijana mwenye umri wa miaka 17, akajibu kwamba hawezi kujua sababu. 

Wakili Chavida akamuomba Hakimu Amuru kuingilia kati, akidai kuwa wanachukua muda mrefu kuuliza maswali ya kupoteza muda. Vilevile alidai kuwa swali hilo halina maana, kwani halimhusu aliyepiga simu na kumuomba hakimu kuliondoa.

Wakili Ohola alikubali kuondoa swali hilo na kuendelea na maswali mengine.

Shahidi wa tatu, Ramadhan Ayubu, mteja aliyeingia dukani hapo, anadai mbele ya mahakama kuwa alipoingia alikuta watu ambao hawakuwa wa kawaida na kujikuta akiwekwa chini ya ulinzi na watu hao.

Anadai kuwa kiongozi wa kundi hilo alielekeza atolewe ‘loki’, na mara moja akaanza kupigwa kisha akaporwa Sh 35,000 pamoja na simu yake.

“Niliporuhusiwa kuondoka nikatoka nje, kisha nikarudi kudai simu na fedha zangu. Sabaya akasema ‘huyu bado ana wenge’. Akaamuru nitolewe ‘wenge’. Wakanza kunipiga na kufukuzwa,” anasema Ayubu.

Shahidi wa nne katika kesi hiyo, mtoto wa mwisho wa familia ya mwenye duka, Shahadi Hajarin, anadai kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na mjomba wake kuwa dukani wamekuja maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), kwa hiyo anahitajika, lakini alipofika alimkuta Sabaya, alipomsalimia akaamrishwa kupiga magoti na kuanza kupata kipigo.

Shahadi alisababisha wasikilizaji kuangua kicheko mahakamani baada ya kudai kuwa dukani alikuta msichana amelazwa chini, Sabaya anamuuliza maswali.

“Akamuuliza iwapo jana alifika dukani hapo na kubadilisha dola. Msichana huyo alijibu; ‘ndiyo mkuu’, huku akijifanya kutetemeka,” anadai. 

Malumbano yakaibuka tena pale Wakili Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka, alipotaka kujua wakati akiwa ndani kuna mtu yeyote aliyeingia dukani hapo.

Alipotaka kujibu, Wakili wa Sabaya, Moses Mahuna, aliingilia kati akidai swali hilo halina maana; ndipo Wakili Kweka akaieleza mahakama kuwa mawakili wa upande wa utetezi wanafanya mambo ambayo hayastahili kufanywa na wanasheria; kwamba wanamkwaza.

Akarekebisha swali lake kwa kuhoji kitu gani kiliendelea? Akajibiwa na Shahadi kwamba alikuja Diwani wa Sombetini, Bakari Msangi, akamsalimia Sabaya; ‘Habari yako!’ Sabaya akamjibu; ‘unanisalimia hivyo hujui jina langu? Sema DC ole Sabaya.’

Msangi akarekebisha salamu yake lakini bado akawekwa chini ya ulinzi kwa amri ya Sabaya.

Anasema baada ya Msangi kuingia akashangazwa na kitendo cha msaidizi wa Sabaya kumwita bosi wake ‘Jenerali Sabaya’!

Anadai Msangi alimwambia aache utani huo, lakini Sabaya akatoa amri mabaunsa wake wamuweke stoo, wampe kipigo mpaka wamtoe ngeu.

Shahidi wa tano, Selemani Kassim ameieleza mahakama kuwa yeye ni mfanyabiashara jirani na duka lililovamiwa na Sabaya na kwamba alimwona DC huyo wa zamani akiingia lakini hakujua kinachoendelea ndani ya duka.

Msangi ni shahidi wa sita na akiongozwa na Wakili Chavida, anadai kuwa aliitwa kwa simu baada ya kudaiwa kuwa limevamiwa na Sabaya.

Anasema alipofika alikuta duka limefungwa kwa mlango kuvutwa chini na kubaki sehemu ndogo; akaunyanyua mlango huo na kumkuta Sabaya, kisha akamsalimia lakini sabaya hakumjibu.

“Akawatazama mabaunsa wake na kuwaambia mwelezeni jina langu. Wale walinzi walisema ‘msalimie Jenerali ole Sabaya’. Nikatii. Nilipotaka kumuuliza kuna nini kilichotokea, aliniambia ‘wewe unakuja kuingilia kazi nilizotumwa na Rais kwa kuwatetea hawa?’ akaamuru wanipekue, wakachukua Sh 390,000,” anasema Msangi.

Baada ya kuchukua pesa hizo ndipo Sabaya alipowaamuru mabaunsa ‘wamtoe wenge’, akaanza kupigwa na kulalamika kwanini anataka kuuawa?

Aliieleza mahakama jinsi alivyopigwa hadi alipopelekwa kwenye Hoteli ya Sakina ambapo wakati Sabaya akila raha katika hoteli hiyo, aliiona simu yake ndani ya gari na bunduki mbili nyuma ya gari hilo aliloachwa; akachukua simu na kumpigia mke wake ambaye alifika hotelini hapo na ndicho kilichomsaidia kuachiwa na Sabaya akiwa hoi.

Shahidi huyo ambaye amechukua siku tatu kutoa ushahidi wake, alianza kuhojiwa na wakili wa Sabaya, lakini mahojiano hayo yalikwama baada ya Wakili Mahuna kumuuliza kama aliibiwa pochi katika tukio hilo, msangi akasema hapana.

“Unakumbuka maelezo yako ya Februari 10, mwaka huu siku ya tukio uliyoandika polisi?” anahoji wakili. Msangi akajibu kuwa hakuwahi kusema ameibiwa pochi.

“Ninakuonyesha ulichokiandika. Je, hii si saini yako?” anahoji Wakili Mahuna.

Msangi: Ninasema kama kimeandikwa lakini mimi sijasema nimeibiwa pochi.

Mahuna: Basi tunaomba mahakama hii ipokee kielelezo hicho kama ushahidi.

Hapo ndipo Kweka aliposimama na kuomba mahakama isipokee kielelezo hicho kwani wanasheria wanajua wazi taratibu za kuingiza maelezo yaliyoandikwa polisi yenye mkanganyiko na jinsi ya kuyaingiza mahakamani.

Mahuna aliomba mahakama iliache swali hilo ili kutopoteza muda, lakini Kweka akasema hawakuja mahakamani kufanya siasa au ushabiki wa mpira; kwamba ni lazima kufuata taaluma na anachotakiwa Mahuna ni kukubali amekosea na kulifuta swali hilo ili haki itendeke kila upande.

Mahuna akakubali kukosea lakini akasema kielelezo hicho ni halali; yeye amekosea jinsi ya kuwasilisha.

Hilo lilimfanya Kweka kuanza kutoa vielelezo vingi kama elimu kwa wanasheria, jambo lililosababisha kesi kuahirishwa.