Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, amefariki dunia ghafla Novemba 3, 2025, nyumbani kwake mjini Kahama, mkoani Shinyanga ambapo anatarajia kuzikwa leo.

Mgeja ni mmoja wa wanasiasa waliowahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuacha alama kubwa katika siasa za Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla.

Alijipatia umaarufu mkubwa akiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, nafasi aliyoitumikia kwa miaka kadhaa kabla ya kustaafu, ambapo alijulikana kwa ushawishi, ujasiri na uwazi katika kuzungumzia masuala ya kisiasa na maendeleo.

Baada ya kustaafu uongozi ndani ya CCM, Mgeja aliendelea kushiriki mijadala ya kitaifa na kutoa maoni yake kuhusu masuala ya siasa, utawala bora na mustakabali wa Taifa kupitia taasisi yake ya Tanzania Mzalendo Foundation. Kupitia taasisi hiyo, alihamasisha uzalendo, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti za kisiasa.

Mgeja pia alikuwa akifahamika kwa kutoa maoni yake hadharani kuhusu mwelekeo wa siasa nchini, mara nyingine akitoa ushauri wa wazi kwa viongozi wa vyama vya siasa, jambo lililomfanya kuheshimiwa na wanasiasa wa pande zote.

Katika kipindi cha uhai wake, Mgeja alishiriki kampeni na mikutano mingi ya kisiasa, na mara kadhaa amekuwa miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha demokrasia na ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa Taifa.

Mgeja ameacha historia ya ujasiri, uzalendo na mapenzi makubwa kwa nchi yake.

Mazishi yatafanyika saa saba mchana Novemba 4, 2025 Mjini Kahama.