Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amewashauri waandishi wa habari nchini kutumia uhuru ulioongezeka kwa kuwajibika na kuzingatia sheria.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa majadaliano ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 iliyofanyiwa marekebisho mwezi kwa kushirikiana na Muungano wa Haki ya Kupata Habari (CoRI).

Balile amesema kuwa tansia ya habari imepita katika kipindi kigumu cha sheria ngumu kwa kipindi cha miaka sita hivyo ni vyema waandishi wa habari wakanyakazi kwa weledi kutokana na kuongezeka kwa uhuru wa kujieleza.

“Nawaomba waandishi wenzangu tutumie fursa hii vizuri kwani tukifanya tofauti Serikali inaweza kufanya marekebisho na kurejea kule tusikokutaka.

“Ni ukweli usiopingika kuwa uhuru umeanza kuimarika, watu wanazungumza kwa namna wanavyotaka na wengine wamefikia hatua hata kutoa kauli zisizofaa kwa viongozi na hawakamatwi na Polisi kama ilivyokuwa miaka sita iliyopita

“Nawashauri wenzangu tutumie uhuru huu kwa kufanyakazi kwa weledi na kuzingatia sheria zilizopo” amesema Balile.

Amesema wanahabari hawapaswi kuchafua taaluma yao kwa kutofanya kazi kwa weledi au kutumia vibaya uhuru ulioongezeka na kukiuka maadili ya uandishi wa habari.

“Serikali imekiondoa kifungu cha 5(1) kilichokuwa kikimpa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), kugawa matangazo kwenye vyombo vya habari ambapo mwanya huo uliviumiza vyombo vingine vya habari lakini sasa kimeondolewa na mambo yameanza kuwa vizuri,” amesema.

Balile amesema pia imefanya marekebisho katika Kifungu cha 38 (3) kilichokuwa kinazungumzia kashfa kugeuzwa jinai sasa kimewekwa sawasawa tofauti kilivyokuwa awali.

“Kifungu cha 50 (1), 50 (11) kilikuwa kinaruhusu mtu yoyote kudai amekashfiwa na Serikali ingeweza kumfungulia mashtaka aliyemkashifu mwenzake lakini sasa kimeondolewa.

“Pia sasa mitambo iliyotumika kuchapa gazeti lenye taarifa ya kashfa sasa itakuwa salama tofauti na mwanzo ambapo ingeweza kutaifishwa na kuwa sehemu ya washtakiwa” alisema.

Balile amesema kuwa vifungu vilikuwa 22 lakini vilivyokubaliwa na Serikali vilikuwa vinane na wadau wameona ni afadhali ingawa bado kuna vipe gele vingine vinahitaji kufanyiwa marekebisho kwani vinakwamisha utendajikazi wa waandishi wa habari.

Naye Deus Kibamba amesema mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Serikali hayatakuwa na maana kama waandishi wa habari hawatakuwa wabunifu na kujiandaa kwa mabadiliko yatakayotokea.

Kibamba amesema mwandishi wa habari ni kioo cha jamii na jicho hivyo ni lazima wawe imara kusimamia haki zao, kubuni na kutafuta fursa zaidi za maendeleo.

“Wanahabari msiwe watu wa kuripoti tu habari bali muwe sehemu ya kutetea haki zenu, kuwa wabunifu na msione aibu kusimamia mambo yetu pamoja na kuboresha mazingira mliyonayo” amesema.

Pia Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini (Tudarco), Dk Darius Mukiza amesema vyombo vya habari hivi sasa vinapaswa kutafuta njia ya kuboresha mapato yake na kukuza ajira.

Alishauri vifanye shughuli za ushauri wa masuala mbalimbali, utafiti na mafunzo ambazo zitawapatia mapato ya kuwalipa watumishi wao.

“Wafanye makongamano ya kitaifa, utafiti, mafunzo na shughuli mbalimbali zinazohusu taalumu zao kama njia za kujiongezea kipato badala ya kutegemea matangazo kutoka serikalini.

Naye mhariri wa gazeti la Mwananchi, Salehe Mohamed, alisema ni vema waandishi wa habari wakatafuta fursa ya kujielimisha zaidi ili kutenda kazi kwa weledi na ubunifu

“Tujisimamie na kujisemea wenyewe kwenye mambo yanayotuhusu na yanayogusa masilahi ya Taifa bila kuhofia chochote” amesema.

Hata hivyo wahariri walikubaliana kufanyakazi kwa weledi na kuzingatia sheria ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali kufanyia marekebisho vipengele ambavyo bado vimekuwa kikwazo kwa waandishi wa habari iliwepo suala la upataji taarifa kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali.

By Jamhuri