3-Waziri-wa-Ujenzi-John-Magufuli-kush-akitoa-taarifa-kwa-waandishi-wa-habari-hwapo-pichani-leoKamanda-MpingaAjali ya gari iliyoua watu 23 papo hapo na kujeruhi wengine 34, imeongeza maumivu mengine kwa Watanzania ambako sasa takwimu zinaonesha zaidi ya abiria 1,000 wamepoteza maisha.
Ajali iliyotokea usiku wa kuamkia Jumatatu iliyopita ilihusisha basi la Kampuni ya Another G kugongana na lori eneo la Kinyanambo A, Mafinga wilayani Mufindi, ikiwa ni takribani miezi mitatu baada ya ajali nyingine iliyoua watu 50 katika wilaya hiyo.
Basi hilo, lifanyalo safari zake kati ya Iringa na Njombe, lilipata ajali hiyo saa 1:45 usiku wa kuamkia Jumatatu wakati dereva alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana uso kwa uso na lori.


Machi 10 mwaka huu, watu 50 walipoteza maisha kwenye ajali iliyotokea Mafinga, Changarawe, wakati kontena lililokuwa limebebwa na lori lilipochomoka wakati dereva akijaribu kukwepa mashimo barabarani na kuanguka.
Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohamed Mpinga, anasema ajali za barabarani zimegharimu maisha ya watu 969 kati ya Januari mosi na  katikati ya Juni, mwaka huu. Aidha, watu 2,500 wamejeruhiwa katika kipindi hicho, wengine wakipata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali hizo.
Hii ina maana kwamba kwa wastani watu 10 walipoteza maisha katika ajali za barabarani kila siku kati ya Januari na Juni mwaka huu, ilhali waliojeruhiwa ni wastani wa watu 25 katika muda huo.
 Mpinga anasema hadi sasa zimetokea ajali za barabarani 2,240 kati ya Januari na katikati ya Juni.


“Dereva akifanya makosa akikamatwa abiria wanachangia kumlipia faini, jambo ambalo linawapa madereva kiburi wakiamini akifanya makosa abiria wanamsaidia,” anasema Mpinga.
Lakini taarifa za uchunguzi zilizofanywa na gazeti hili zinasema Jeshi la Polisi kitengo cha Mpinga, kimeelezwa kuwa kiburi ndiyo chanzo cha ajali nchini.
Nyaraka ambazo gazeti hili limeziona zinaeleza uzembe ambao unafanywa na vyombo hivyo vya dola kwa kupuuzia mapendekezo ya kitaalamu kuhusiana na kudhibiti ajali nchini.


Barua ya Februari 15, 2010 kutoka kwa Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kwenda kwa aliyekuwa  Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, inabainisha kuwapo baadhi ya watendaji serikalini kutofuatilia badala yake wamekuwa wakitumia amri.
“Mwaka 1996, katika juhudi zetu za kupunguza ajali kama si kutokomeza kabisa katika kikao chetu cha pamoja na wamiliki, tulipendekeza tufunge chombo kinachoonesha mwendokasi wa safari nzima ya basi, yaani ‘to and fro’ (Techograph), hata hivyo ushauri wetu ulipuuzwa na tukaamriwa kufunga vidhibiti mwendo (speed governor).


“Leo ni mwaka wa kumi na nne tangu tufunge hivyo vidhibiti mwendo na takwimu za ajali za barabarani hazioneshi kushuka,” inasema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Taboa,  Mohammed Abdullah.
Hata hivyo, katika barua hiyo wamiliki wa mabasi wanapinga ufungaji wa vidhibiti mwendo kutokana na vyombo hivyo kutumia umeme na kutodumu kwa muda mrefu, wakati uwezo wake wa kudhibiti mwendo kuwa ni ule unaozidi kilometa 80 kwa saa tu.
Barua hiyo inaeleza kuwa wasafirishaji walikuwa na mpango wa kufunga ‘Tracking System’ na ‘Fleet Management System’ teknolojia ya kisasa ambayo ingeweza kufuatilia mwenendo wa mabasi hayo ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.
“Wasiwasi wa wasafirishaji unakuwa pale tunapokuwa na jitihada na nia njema kama hii, tukianza kusema kabla ya watu wote hawakuielewa vizuri na kujitayarisha kuvitumia. Huenda mtu mjanja akapenya na kwa wasimamizi na wakaamua vitu vya ajabu bila kujali usahihi wake kama ilivyokuwa mwaka 1996, tulivyoamua kufunga vifaa vipya vya techograph likaibuka la speed governor badala ya techograph,” inasema.


Inaeleza kuwa ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na wembamba wa barabara zilizopo, matuta yaliyojengwa katika barabara kuu pamoja na utaratibu mbovu wa askari wa Usalama Barabarani kusimamisha magari ghafla huku wakitokea mafichoni.
Inasema kuwa tatizo jingine ni pamoja na tabia ya utoaji wa leseni kwa madereva wasio na ujuzi wa kutosha kwa upande wa usafirishaji wa abiria, hivyo kusababisha ongezeko la ajali nchini pamoja na kugharimu maisha ya watu.
Hivyo, wamelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwafungia leseni madereva, kwa muda, wale watakaopata ajali na watakaporuhusiwa kuendesha magari kutoruhusiwa kusafirisha abiria.


Katika nyaraka ambazo JAMHURI iliziona, Machi 2010 Taboa walitangaza zabuni ya kutafuta mzabuni kwa ajili ya kufungwa kwa ‘Tracking System’ katika mabasi ya abiria ambako kampuni 16 ziliomba hivyo kuingia katika ushindani.
Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa idadi hiyo, kampuni nane kati ya hizo zilionekana kuwa ni feki na baadhi yake zilikuwa zikimilikiwa na baadhi ya vigogo nchini. Baada ya zabuni hiyo kutangazwa, iliteuliwa timu ya wataalamu kufuatilia waombaji ambayo ilikuwa na watu watano: Dk. Jabiri Kuwe Bakari (Mhadhiri-Chuo Kikuu Kishiriki Dar es Salaam), Dk. Mussa Kissaka (Mhadhiri-UDSM), Stanley Mwalembe (Mhadhiri- DIT), Godfrey Nsato (ICT-Meneja SUMATRA) na SSP J. Kahatano.


Kutokana na vigezo vilivyotangazwa, Kampuni ya U-Track Africa Ltd ilishinda zabuni hiyo na kuingia makubaliano ya kufunga vifaa vya kufuatilia mwenendo wa magari katika ofisi za Makao Makuu ya Polisi ambavyo, hata hivyo, havikuweza kutumika kama ilivyotakiwa.
Kutokana na makubaliano hayo ambayo yaliweza kubainisha U-Track kutoa uangalizi wa karibu na matengenezo kwa vifaa hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu, pia gharama za ufungaji wa vifaa vya kufuatilia mwenendo wa mabasi hayo ambavyo viligharimu zaidi ya dola za Marekani 28,200.
Aidha, Mei 11, 2010 yalifanyika makubaliano baina ya TABOA na U-Track Africa Ltd yanayobainisha majukumu ya kampuni hiyo katika kipindi chote cha mkataba kama inavyosomeka sehemu ya mkataba huo.


Katika barua ya Mei 14, 2010, Taboa ilimwandikia IGP ikiitambulisha Kampuni ya U-Track iliyoshinda zabuni hiyo hivyo kutambuliwa na mamlaka hiyo kwa kazi ya kufunga vifaa katika mabasi ya abiria. Pia Mei 31, 2010 Taboa iliwaandikia barua wamiliki wote wa mabasi kuitambulisha kampuni hiyo.
Barua hiyo inasomeka; “Kufuatana na ajali nyingi zinazotokea barabarani kila siku na kuthibitika kuwa vidhibiti mwendo vilivyokuwa vikitumika vilishindwa kufanya kazi iliyokusudiwa, tuliiomba Serikali badala yake ituruhusu kutumia Live Tracking System na ambayo itakuwa na kamera.
“Asiyeweza kulipa mara moja fedha taslimu atalipa taratibu kwa miezi 36. Kwa kipindi cha miezi 36 U-Track watakuwa wako saa 24 kuangalia vifaa hivyo vinafanya kazi ipasavyo,” inasema barua hiyo.
JAMHURI ilipozungumza na uongozi wa Taboa hivi karibuni kuhusiana na nyaraka hizo, uongoni ulikubali kuwapo kwa suala hilo ambalo, hata hivyo, lilishindwa kutekelezeka kutokana na sababu zisizofahamika.


Suala la udhibiti wa ajali za barabarani lingeweza kupunguzwa kama si kuondolewa kabisa kama magari yote ya abiria yangefungwa vifaa hivyo, ambavyo vingesaidia kuweza kufuatiliwa kama ilivyobainishwa katika nyaraka hizo.
Anaeleza kuwa hata gharama za vifaa hivyo zilikuwa dola za Marekani 300, na kila mwisho wa mwezi mmiliki alitakiwa kulipia dola 20 tu, gharama ambazo ni ndogo kuliko zile ya speed governor zilizowahi kufungwa kwa kiasi cha shilingi milioni 1.2.
Anaeleza kuwa miundombinu mingi nchini si rafiki kutokana na kuwa ya kizamani, huku ikiwa si madhubuti kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya magari nchini.


“Ujenzi wa miundombinu ya barabara unafanywa kisiasa, inajengwa chini ya kiwango huku ikiongezewa na mzigo wa matuta makubwa katika barabara kuu, jambo ambalo si sahihi, haiwezekani barabara kuu ikajengwa matuta, hairuhusiwi. Pia hakuna alama za kutosha zinazobainisha kuna nini mbele. Duniani kote highways hakujengwi miji wala shule karibu bali kunajengwa vituo vya mafuta tu, lakini nchini kwetu tuko tufauti,” wanasema Taboa.
Akiongelea madereva, anasema kuwa ili kuepuka ajali nchini ni lazima madereva kutojihusisha na anasa ikiwa ni pamoja na kupata muda wa kupumzika vya kutosha.


“Dereva anasababisha ajali kama gari imeleta matatizo, barabara mbaya, anatembea mwendo hatarishi, ulevi wa aina yoyote akilini pamoja na uchovu, ingawa matuta nayo ni moja ya sababu,” anasema.
Akiongelea suala la uwezo mkubwa wa gea kwa magari ya abiria ya Scania 113-124, anasema kuwa magari hayo si sababu ya ongezeko la ajali nchini, bali kiwango cha mwendo kasi kilichowekwa na mamlaka husika kinasababisha ajali kutokana na madereva wengi kutembea mwendo mkubwa huku wakiwa na shaka ya kukamatwa.


“Katika mambo ya kushangaza nchini ni Serikali kupanga speed 80 tu nchini, lakini mwendo huu hata viongozi wetu wenyewe hawafuati sheria hii, wanatembea zaidi ya 100.Tulishawaambia ni vyema sheria hii ikabadilishwa na kuondokana na mwendo huo unaosababisha madereva kukimbia huku wakiwa na hofu ya kukamatwa, tuliomba kuwekwa speed 100,” anasema.
Anasema kuwa ni kweli mradi huo wa kufunga vifaa hivyo katika mabasi ya abiria ulikuwapo ila kwa sasa Serikali haina fedha.
“Serikali bado inalifanyia kazi suala hilo, kinachosubiriwa ni kupatikana kwa fedha zinazohitajika ambazo ni zaidi ya bilioni 4 ili tuweze kuanza. Na andiko la mradi huo tayari lipo muda mrefu, tatizo ni hizo fedha tu,” anasema Kamanda Mpinga.


Hata hivyo, anafafanua kuwa walikaa na kutafakari kuwa ni vyema mradi huo ukawa chini ya Serikali kuliko kukabidhiwa kwa kampuni moja ya mtu binafsi, hivyo basi mradi huo utatumia kanuni zilezile zinazotumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akizungumza zabuni iliyofanywa na Taboa katika mchakato wa kumpata mzabuni katika mradi huo na kuibuka kwa kampuni hewa, anasema kuwa Taboa walifuata taratibu zote ingawa walikumbana na msururu wa kampuni hewa zilizokuwa zimeomba kutekeleza mradi huo, ambazo ziliweza kubainika mapema na kuondolewa nje ya kampuni shindani.


Alipoulizwa ni taratibu zipi zitatumika kuweza kumpata mzabuni ili kutokumbana na kampuni hewa kama ilivyotokea hapo awali, anaeleza kuwa anaamini ya kuwa kampuni zitakazopatikana katika mradi huo zitafanyiwa uchunguzi wa kutosha hivyo kutokuwa na udanganyifu wa aina yoyote ile.
Akiongea na JAMHURI, Katibu wa Taboa, Enea Mrutu,  anasema kuwa utaratibu wa ufungwaji wa vifaa hivyo uliwasilishwa vibaya kutokana na kutawaliwa na ufisadi, hivyo ulikataliwa na wadau katika mkutano uliofanyika.
“Uliletwa Karimjee tukaukataa kutokana na gharama zake kuwa kubwa mno, mimi ndiye niliyeupinga kwa nguvu zangu zote. Na waziri wakati huo aliunda kamati ambayo ilikaa na kuleta mrejesho mzuri tu, lakini baadaye ikapotea na kufa kifo cha mende,” anasema Mrutu.


Anasema kuwa tangu wakati huo hawajaweza kufuatilia jambo hilo ila Taboa kama watataka kuingiza chombo hicho nchini, wataingiza chombo kisicholipiwa ada ya mwezi kwa nchi nzima, na kuwa iwapo Serikali itataka utaratibu huo kutumika basi wapewe kipaumbele maana wanao uwezo wa kuagiza chombo hicho kwa gharama zao hata kwenda kununua nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kumtafuta mtu wao wenyewe aweze kuwafungia vifaa hivyo.
“Leo hii tunapoongea nimepokea barua ya mtu mmoja ambaye anataka kutufungia car tracking ambaye naona yuko vizuri, amesema atafunga magari 10 bure ambayo yanafanya safari zake njia tofauti tofauti kwa njia zote nchini na madereva wa mabasi hayo kuwekewa bima ya ajali ya kiasi cha Sh. milioni 5 iwapo itotokea,” anasema Mrutu.

 
3579 Total Views 8 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!