Jaji Mkuu Mstaafu Augustino RamadhanJaji Augustino Ramadhani amesema endapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watu wasitarajie kuwa “uchungaji” wake utamfanya awe na huruma na wakosaji.
Katika mahojiano maalum na JAMHURI, Jaji Ramadhani amesema atapambana na wala rushwa kama alivyofanya wakati akiwa Jaji.
“Mimi ni Mchungaji ndiyo. Mimi ni mcha Mungu, nimesimamia haki nikiwa jaji kwa sababu Mungu anapenda haki.


“Watu wasitarajie kwa kuwa ni Mchungaji nikiwa rais nitakuwa mpole, kwa hiyo mtu anaweza kula rushwa au kuvuruga mambo halafu nikamtazama tu, hakuna hilo,” amesema.
Ameongeza: “Hata nilipokuwa jaji nimetamka kuwatia hatiani wahalifu. Wengine nimewahukumu kunyongwa hadi kufa nikiwatazama machoni. Adhabu ya kunyonga nimeitamka hivi nikimtazama mshitakiwa.
“Hakuna kitu kizito kama kutamka mtu kunyongwa. Kunyonga ni kitu kizito, lakini nimeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kufuata sheria na haki.


“Sasa ninapoulizwa kuhusu wala rushwa nasema hiyo ni kazi nyepesi kwa sababu kazi ngumu ya kuhukumu kunyonga niliiweza, hii ya wala rushwa naimudu kabisa.”
Anasema alipokuwa akiongoza Mhimili wa Mahakama alipambana na rushwa.
“Nilikuwa Jaji Mkuu wa kwanza kuunda Tume ya Uajiri wa Mahakama kwa ajili ya kushughulikia vyeo na nidhamu. Tulitembea mikoa 18 na huko tuliwaambia wakuu wa wilaya na mikoa kuwa wanao uwezo na madaraka ya nidhamu kwa mahakimu.
“Tuliwahimiza watekeleze sheria kwa vitendo ili kuondokana na kero ya rushwa ambayo kwa kweli ni kero kubwa sana.


“Nikiwa rais, sasa nitakuwa nimepewa rungu kubwa zaidi la kupambana na adui rushwa na uonevu,” amesema.
Jaji Ramadhani amesema ameingia kwenye uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ridhaa yake mwenyewe, na kwamba hakuna shinikizo lolote alilopata kutoka upande au kwa mtu yeyote.
 
Mambo yanayomgusa zaidi
 Jaji Ramadhani amesema pamoja na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM endapo atashinda, mambo muhimu matatu ni kati ya mengi atakayoyapa kipaumbele.
Jambo la kwanza anasema ni Umoja wa Nchi. “Kwa sasa mtaona hatuna ule umoja kama kule nyuma. Umoja wetu umeyumba. Nitahakikisha narejesha misingi ya umoja ili tuendelee kuwa Taifa moja lenye watu wanaoishi kwa kupendana,” anasema.
Pili, anasema kazi yake nyingine itakuwa kurudisha Heshima ya Nchi na Wananchi.


“Kuna wakati ukisema wewe ni Mtanzania, unaona fahari kubwa sana. Watu wa mataifa mengine wanakufurahia kweli kweli. Hili limeyumba kidogo, nitajitahidi kwa dhati kabisa kuimarisha heshima ya Tanzania na Watanzania ili ile heshima tuliyokuwa nayo iendelee,” amesema.
Tatu, anasema anaguswa mno na hali ya umaskini unaowakabili Watanzania. Kwa maana hiyo, anasisitiza suala la kupambana na maadui watatu waliokwishatangazwa tangu mwaka 1961- Ujinga, Maradhi na Umaskini – kuwa ni moja ya kazi zake kubwa atakazozifanya endapo ataingia madarakani.
 
Umaskini wamkera
Jaji Ramadhani anasema Tanzania ni nchi yenye rasilimali nyingi mno, na kwa hiyo hakuna sababu kwa wananchi wake kuendelea kuwa maskini.
“Mungu ametupendelea kwa rasilimali nyingi sana. Rasilimali zote zipo Tanzania. Mungu alitaka Watanzania tuishi maisha mazuri kwa kutumia rasilimali hizi. Tuna rasilimali chungu nzima. Hakuna nchi katika Afrika yenye rasilimali kama sisi. Kinachotakiwa sasa ni determination (uamuzi) wa kuzitumia rasilimali hizo kuondoa umaskini,” anasema.
 
Historia ya Jaji Ramadhani
Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Julai 22, 2007 liliandika wasifu wa Jaji Ramadhani.
Alizaliwa Desemba 28, 1945 Zanzibar mjini akiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wanane. Ni Mkristo wa madhehebu la Anglikana.
Alisoma shule mbalimbali za msingi Mpwapwa mkoani Dodoma. Mwaka 1952-1953 alisoma Town School, Tabora hadi darasa la tatu hadi la nne mwaka 1954-1956 na darasa la sita na saba alisoma Kazel Hill sasa inatwa Shule ya Msingi Itetemia mwaka 1957-1958. Na darasa la nane tu mwaka 1959 akarudi kusoma Mpwapwa.


“Mwaka 1960-1965 nilijiunga na Tabora School kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha sita. Kwa kuwa nilifaulu nilichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966, na nilisoma Shahada yangu ya Sheria na ilipofika Machi 1970 nilihitimu masomo.
“Na mwishoni mwa Machi mwaka huo huo wa 1970 nikajiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Niliingia jeshini kama mwanasheria raia mpaka kipindi cha mafunzo ya kijeshi nikaenda kwenye mafunzo na kisha nikarudi kuitumikia JWTZ.
“Ilipofika mwaka 1971 nikapewa kamisheni kambi ya Mgulani nikawa luteni (nyota mbili). Nikaendelea na jeshi hadi mwaka 1977 nikahamishiwa Brigedi ya Faru, Tabora nikiwa na cheo cha Meja.


“Sasa mwaka 1978 ndiyo mzee Aboud Jumbe Mwinyi, wakati huo akiwa ni Rais akaniita Zanzibar na kuniteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar na kipindi hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva.
“Oktoba 1978 niliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Na ilipofika Machi 1979 nilirudishwa JWTZ na baada ya muda mfupi nikapelekwa kwenye Vita ya Uganda (Vita ya Kagera), nikiwa na cheo cha Luteni Kanali na kwenye vita hiyo nilikuwa naendesha Mahakama za Kijeshi.
“Vita ilipokwisha nikarudi Zanzibar. Januari 8, 1980 nikaapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, wakati huo nikiwa na cheo cha Luteni Kanali. Nikaendelea na Ujaji Mkuu Zanzibar hadi Septemba 1989 alipoapishwa Jaji Mkuu Zanzibar, Hamid Mahamod Hamid.
Hata hivyo, Juni 23, 1989 niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania hadi Julai 2007 nilivyoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.


Nilipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Bara ndiyo sababu ya kuacha Ujaji Mkuu Zanzibar.
“Januari 1993 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na niliendelea na nafasi hiyo hadi Januari 2003. Oktoba 2002 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
“Mwaka 1997 nilistaafu JWTZ nikiwa na cheo cha Brigedia Jenerali, na niliagwa kwa heshima zote za kijeshi japo sikupewa mafao yangu kwa kuwa mafao hayo yameunganishwa kwenye kazi yangu ya ujaji hivyo, mafao yangu yote nikalipwa wakati nilipostaafu kazi ya Ujaji Mkuu.
“Novemba 2001 niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki nafasi ambayo ni ya miaka sita.”


Jaji Ramadhani ana mke na watoto wanne; kati yao wasichana wakiwa wawili. Mtoto wake wa kwanza, Francis, ni mwanasheria; Brigeth ana Shahada ya Uandishi wa Habari; Marina ni Mfamasia, na Mathew naye ni Mfamasia.
Jaji Ramadhani alitawazwa Desemba 28, 2013 kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar.
Katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Ramadhani alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Katika Kanisa la Anglikana anajulikana na kuheshimika kwa umahiri wake kwenye upigaji kinada.

 

By Jamhuri