Marekani na Iran zinakaribia kufikia makubaliano ya kusitisha vita katika eneo la Ghuba. Haya ni kwa mujibu wa chanzo kutoka Pakistan kinachohusika na juhudi za upatanishi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, makubaliano hayo yanaweza kujumuisha kusimamishwa kwa mpango wa nyuklia wa Iran kwa muda, kuondolewa kwa vikwazo vyaMarekani na kuruhusu tena usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz.

Habari za uwezekano wa makubaliano hayo zimesababisha bei ya mafuta duniani kushuka kwa zaidi ya asilimia nane, huku masoko ya hisa yakipanda kutokana na matumaini ya kurejea kwa utulivu.

Iwapo makubaliano hayo yatafikiwa, yanatarajiwa kuanzisha kipindi cha siku 30 cha mazungumzo zaidi, yanayolenga kumaliza kabisa mzozo ambao umevuruga usafirishaji wa nishati duniani.

Rais wa Marekani Donald Trump pia ametangaza kusitisha kwa muda operesheni ya kijeshi ya kusindikiza meli katika eneo hilo, akisema kuna hatua iliyopigwa katika mazungumzo.