Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
SERIKALI imesema inatarajia kutekeleza mradi wa kuimarisha utayari wa Zanzibar kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wenye thamani ya Dola za Kimarekani 500,000 (shilingi bilioni 1.3).
Ilisema fedha zitakazotumika kutekeleza mradi huo ni kutokana na ufadhili kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCF), ambao utaanza mara baada ya tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi kukamilika.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa leo Mei 09, 2026 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Nungwi Mhe. Mdowe Haji Kombo, aliyetaka kujua lini Serikali itajenga ukuta katika Fukwe za Bahari ya Nungwi Kiungani ili kuzuia bahari kuingia katika makazi ya watu.
Kwagilwa alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27 zimetengwa zaidi ya shilingi bilioni 31 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa pande zote mbili za Muungano.
Alisema kuwa kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa Zanzibar yote, maeneo 148 yameathirika ambapo 123 yapo Pemba na 25 yapo Unguja hivyo, kutokana na hali hiyo Serikali ipo katika hatua ya kuanza utekekelezaji wa miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo hayo.
”Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia fedha zilizotengwa, tumeanza kutekeleza miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika halmashauri 11 zilizopo Zanzibar na halmashauri 54 zilizopo Tanzania Bara na hatua itakayofuata ni kubaini gharama za miradi hiyo,” alisema Kwagilwa.
Aidha, alitaja hatua za dharula zilizoanza kuchukuliwa katika maeneo matatu yaliyopo katika Wilaya ya Kati, Unguja yakiwemo ya Cheju, Chwaka na Ubago ambayo yatanufaika na fedha hizo zilizotengwa ni utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni mojawapo ya hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachukua katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, kupitia hatua hizo, Serikali imeendelea kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa fukwe unaosababisha bahari kuingia katika makazi ya wananchi.


