Vita vinavyoendelea nchini Ethiopia na katika maeneo mengine katika Pemba ya Afrika vinaweza kuathiri harakati za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kujiongezea ushawishi katika eneo hilo.

DJIBOUTI CITY, DJIBOUTI

Wakati dunia ikiwa inahangaika kupambana na janga la Corona, kuna mambo yanaendelea kimyakimya ambayo yanaweza kubadilisha mahusiano na muonekano wa nchi zilizo katika Pembe ya Afrika na hata Afrika Mashariki.

Kinachoendelea katika eneo hilo hakina tofauti sana na jinsi wakoloni walivyokuwa wanagombea maeneo ya kutawala barani Afrika miaka michache iliyopita.

Tofauti ni kuwa wakati mgawanyo huo ulihusisha nchi kukaa pamoja katika Mkutano wa Berlin, hivi sasa kila nchi inajichukulia hatua kivyake kuhakikisha inaimarisha unyayo wake katika eneo hilo. 

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ni moja ya nchi ambazo zimejitanabahisha kuchukua hatua za kuhakikisha inajiimarisha katika eneo hilo.

Tangu kuibuka kwa vuguvugu la Kiarabu mwaka 2011, UAE imejitokeza mstari wa mbele ikijihusisha na masuala kadhaa katika maeneo ambayo yana migogoro kuanzia Misri, Libya hadi Yemen. 

Kwa wastani nchi hiyo ya Ghuba imekuwa ikitumia takriban dola za Marekani bilioni 26 kwa mwaka katika bajeti yake ya ulinzi tangu mwaka 2016, na kiasi hicho kinatarajiwa kuongezeka hadi dola za Marekani bilioni 37.8 ifikapo mwaka 2025, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali.

Kwa kiasi kikubwa ongezeko la bajeti hii ya ulinzi ya UAE linatokana na kujihusisha kwake kwenye migogoro katika eneo la Pembe ya Afrika.

Kukua kwa migogoro na kuongezeka kwa matukio ya vita kumeilazimisha UAE kuongeza idadi ya wanajeshi wake walio nje ya nchi, jambo hilo limewashitua hata majenerali wa jeshi nchini Marekani.

Hadi mwaka jana, jeshi la UAE lilikuwa na kambi imara katika nchi za Eritrea, Djibouti na Somaliland, na kuonyesha jinsi eneo hilo lilivyo muhimu kwa Abu Dhabi. 

UAE inalazimika kulipigania eneo hilo kwa sababu ni mlango wa Bahari Nyekundu, Bahari ya Mediterranean, pia Guba ya Aden. Haya ni maeneo muhimu sana kwa uchumi na usalama wa UAE. 

Pamoja na kulinda masilahi ya kibiashara, kambi za jeshi za UAE katika nchi hizo zinalihakikishia taifa hilo uwezo wa kukabiliana na hatari kabla haijafika nchini mwake. Jambo hilo limeiwezesha UAE kuendelea kufanya biashara na nchi hizo na pia kujitanua hadi maeneo ya Afrika Mashariki wakati huu ambapo inahangaika kukuza mapato yake kutoka katika vyanzo vingine nje ya biashara ya mafuta.

Vita ya mwaka 2015 huko Yemen na kuwekewa vikwazo Qatar mwaka 2017, kumeifanya Abu Dhabi kuchukua hatua zaidi za kujiimarisha katika eneo la Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki. 

Hii ni kwa sababu marafiki zake wa muda mrefu kibiashara walianza kutikiswa, jambo ambalo lilisababisha nchi hiyo nayo iyumbe. Hivyo, lilikuwa ni suala la busara kwa UAE kuanza kujitafutia vyanzo vingine vya biashara kimataifa.

Wakati UAE ikihangaika kulitatua tatizo hilo, nchi za Pembe ya Afrika zikaonekana kuikaribisha kwa mikono miwili lakini mwaka 2017, baada ya kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Misri kwa upande mmoja dhidi ya Qatar, nchi zikalazimika kuanza kuchukua upande wa kuunga mkono.

Somalia

Moja ya nchi zilizojikuta zikiathirika na mgogoro huo wa kidiplomasia ni Somalia. 

Ingawa mgogoro wa Ghuba wa mwaka 2017 unaonekana kama unafikia mwisho, nchi katika eneo la Pembe ya Afrika zimekwisha kuathiriwa sana na mgogoro huo. Somalia imejikuta katika kutoelewana na nchi nyingine nyingi kutokana na mgogoro huo.

Kama zilivyo nchi nyingine za Pembe ya Afrika, Serikali ya Somalia awali iliamua kutoegemea upande wowote katika mgogoro huo. Hata hivyo, UAE, ikaiona Somalia kama inayoiunga mkono Qatar kimyakimya na hilo halikuifurahisha nchi hiyo.

Mwaka 2017, wakati Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo wa Somalia alipoingia madarakani, taarifa zilieleza kuwa Qatar na Uturuki zimesaidia kampeni zake za kisiasa na baadaye taarifa nyingine zikaibuka kuwa hata baadhi ya watu ambao rais huyo aliwateua kushika nafasi nyeti za uwaziri walikuwa na uhusiano wa karibu na Doha na Ankara. Hilo likazidi kuikasirisha Abu Dhabi.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Somalia inaituhumu UAE kwa kuiyumbisha nchi hiyo kwa kuunga mkono na kuvipatia fedha vikundi vya upinzani. 

Tuhuma hizi zilipata msukumo zaidi pale Dubai Ports World, ilipoamua kutoishirikisha Serikali ya Somalia katika mkataba iliyosaini na Jimbo la Somaliland, ambalo limejitangazia uhuru kutoka somalia. 

Mkataba huo ulihusu uendeshaji wa Bandari ya Berbera. DP World pia ikawaleta wawekezaji kutoka Ethiopia na kuwapa hisa katika mradi huo.

Somalia ikatangaza kuwa mkataba huo ni batili na kujaribu kuuzuia kwa kupeleka malalamiko katika Umoja wa Nchi za Kiarabu. Kiongozi wa Somaliland, Muse Bihi Abdi, akasema Serikali ya Farmaajo ilikuwa imetangaza vita kwa kujaribu kuuzuia kataba huo.

Chini ya mkataba huo, Somaliland inatarajia kupata uwekezaji wa hadi dola za Marekani milioni 442, pia kutakuwa na mkataba mwingine wa pembeni na Abu Dhabi kuruhusu majeshi ya UAE kujenga kambi zake katika eneo hilo, jambo ambalo linaweza kuihakikishia nchi hiyo dola za Marekani bilioni moja zaidi.

Sudan

Mwaka 1989, Omar Al-Bashir, aliingia madarakani baada ya kufanya mapinduzi nchini Sudan. Mwaka 1993 akajitangaza kuwa rais na Chama chake cha National Congress kikashika madaraka ya kisiasa.

Chama hicho kinaunga mkono kundi linalotajwa kuwa la kigaidi la Muslim Brotherhood na tangu awali Saudi Arabia na UAE zilikuwa na wasiwasi na utawala wa Sudan.

Hata hivyo, mwaka 2010 serikali ya Al-Bashir ikaanza kulikana kundi hilo ili kuimarisha uhusiano wake na nchi za Ghuba.

Lakini uhusiano wa karibu na Saudi Arabia na UAE hauji hivi hivi. 

Mwaka 2015, Saudi Arabia iliunda muungano ulioingilia vita nchini Yemen. Mwaka 2011, Serikali ya Yemeni iliyokuwa inaongozwa na Ali Abdullah Saleh ikakabiliana na maandamano ya wananchi mitaani na akalazimika kujiuzulu mwaka mmoja baadaye.

Pengo katika uongozi aliloliacha likasababisha baadhi ya maeneo nchini humo kukaliwa na makundi yanayoungwa mkono na kundi la kigaidi la nchini Iran la Houthi. Muungano wa majeshi ulioratibiwa na Saudi Arabia ukadhamiria kulimaliza kundi hilo. Sudan ikajikuta kuwa mshirika muhimu katika vita hiyo.

Mwaka 2018, Omar Al-Bashir akakabiliwa na maandamano ya wananchi na Aprili 2019 jeshi likamlazimisha kuachia madaraka. Jeshi likaunda serikali ya mpito iliyohusisha vikundi vya upinzani kwa lengo la kurejesha demokrasia na hapo UAE ikalazimika kuchukua hatua kulinda masilahi yake dhidi ya mapinduzi hayo.

Hata hivyo, licha ya kuchukua hatua, kuanguka kwa Al-Bashir kunamaanisha kuwa masilahi ya UAE nchini sudan hayawezi kuwa na uhakika na baadhi wanahofia kuwa Emirates inaweza kuvuruga mchakato wa kuirudisha Sudan kuwa nchi ya kidemokrasia kama sehemu ya kulinda masilahi yake.

Ethiopia

Ethiopia inaonekana kama nchi iliyofaidika sana na migogoro inayoendelea katika Pembe ya Afrika, hasa ukizingatia ukaribu wake na UAE. Nchi hiyo ambayo hadi hivi karibuni ilionekana kuwa tulivu, ndiyo ilikuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji.

Februari 2020, UAE ilikubali kuwekeza dola za Marekani milioni 100 kusaidia miradi midogo midogo, midogo na ya kati nchini humo. UAE pia imekubali kujenga bomba la mafuta kati ya Ethiopia na Eritrea.

Lakini Novemba 2020, vita ya wenyewe kwa wenyewe ikaibuka katika Jimbo la Tigray kati ya majeshi ya serikali kuu na majeshi ya jimbo hilo. 

Kiongozi wa wanajeshi hao wa jimbo aliishutumu UAE kulishambulia jimbo hilo kwa kutumia ndege zisizo na rubani kutoka katika kambi yake nchini Eritrea kama sehemu ya kuisaidia serikali kuu.

Ethiopia pia inaweza kuleta sura mpya ya mahusiano yake na nchi za Ghuba katika mgogoro wake na Misri katika mradi wa ujenzi wa bwwa kubwa la umeme katika Mto Nile.

Ujenzi wa mradi huo umeikasirisha Misri, wakati kwa upande mwingine Ethiopia inahitaji umeme huo kujiimarisha kiuchumi.

Ni dhahiri kuwa eneo la Pembe ya Afrika limegeuka kuwa muhimu sana kwa UAE, lakini migogoro inayoendelea inaweza kubadili hali ya mambo wakati wowote.

Vita vinavyoendelea nchini Ethiopia na katika maeneo mengine katika Pemba ya Afrika vinaweza kuathiri harakati za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kujiongezea ushawishi katika eneo hilo.

By Jamhuri