Mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community, kwa Kiingereza, au SADC kwa kifupi), uliyomalizika Dar es Salaam tarehe 18 Agosti, mwaka huu umeidhinisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya nne ya Jumuiya hiyo. Lugha nyingine rasmi za SADC ni Kiingereza, Kireno, na Kifaransa.

Suala halikuwa kwanini SADC ipitishe uamuzi huo ila ni lini ingefanya hivyo. Ingawa, kwa kiasi kikubwa, ni Tanzania pekee ambako Kiswahili kinatumika zaidi kama lugha rasmi na lugha ya mawasiliano, lugha hiyo inatumika pia kwa viwango tofauti nchini Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Msumbiji, Comoro, Malawi, Somalia, Ethiopia, na Sudan.

Nchi sita kati ya hizo ni nchi wanachama wa SADC. Na hiyo ni mojawapo ya sababu za kuanza kutumika kwenye jumuiya hiyo.

Aidha, mwaka 2018 Afrika Kusini ilipitisha uamuzi wa kuongeza Kiswahili kwenye orodha ya lugha ambazo mwanafunzi anaweza kuchagua kujifunza kuanzia mwaka 2020.

Si rahisi kukadiria idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili. Inakadiriwa wanafikia 150, sehemu kubwa ya hao wakiwa ndani ya jumuiya ya SADC. Kwa hiyo uamuzi wa SADC hauhitaji mjadala mrefu kuujengea hoja: ni uamuzi muafaka ambao ungepaswa kupitishwa siku SADC inaundwa mwaka 1980.

Wakati huo ilikuwa Tanzania pekee, kama mwanachama, iliyokuwa inatumia Kiswahili zaidi ya wanachama wengine, lakini napenda kujenga hoja kuwa, hata wakati ule, matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani ya SADC yasipimwe kwa wingi wa nchi wanachama zilizokuwa zinatumia lugha hiyo, bali yapimwe kwa hadhi ya Kiswahili kama lugha ya Kiafrika.

Tukikipa hadhi hiyo uamuzi mwingine wote unakuwa rahisi zaidi. Jumuiya kama SADC na jumuiya nyingine za aina hiyo kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinaimarisha ushirikiano wa kikanda zikiwa na lengo kuu la kuimarisha nguvu za pamoja za kuleta maendeleo kwa Bara la Afrika na watu wake.

Tunapoimarisha tamaduni zetu, pamoja na kutumia lugha za Kiafrika, tunatambua umuhimu wa tamaduni zetu na tunajenga msingi imara wa Waafrika kujiamini na kusimama kwa majivuno kama raia wengine wa ulimwengu wanaotumia lugha zao. Huwezi kujivunia lugha yako kama unawasiliana kwa lugha za wageni.

Sababu moja ya maana kabisa ya kutumia Kiswahili ni kuwafungulia milango sehemu kubwa ya watu waweze kufuatilia majadiliano na makubaliano ya mikutano ya SADC. Nilihudhuria mdahalo ambapo mmoja wa washiriki alisema kuwa SADC ilifanya utafiti katika miaka ya 1980 kupima uelewa wa wananchi juu ya kazi zake. Raia mmoja wa Zambia alisema kuwa anaifahamu SADC na anafahamu umuhimu wake kwa sababu kila mwaka rais wake anaenda huko na kutoa hotuba. Ufahamu huu ni hafifu sana ukizingatia kuwa jukumu kubwa la SADC ni kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Mazoea ya kutumia lugha ya Kiingereza na lugha nyingine za wakoloni ni mabaki ya moja ya athari za ukoloni. Nakumbuka enzi za ujana niliishi kwa muda mrefu kama mwanafunzi kwenye nchi moja inayotumia Kiingereza na niliporudi Tanzania nilikuwa naota kwa Kiingereza.

Natoa mfano huu kusema kuwa wakati mwingine hatufanyi makusudi kutumia lugha nyingine badala ya kutumia lugha zetu wenyewe. Tumelemazwa na mazoea. Lakini wakati mwingine ni tatizo la kushindwa kuondoa kabisa athari za ukoloni kwenye maisha yetu ya kila siku. Tulikomboa nchi zetu kwa mafanikio kutoka kwenye ukoloni. Tunahitaji kukomboa pia fikra kutoka kwenye ukoloni.

Bado ni kawaida kuona kwamba miongoni mwa watu wawili, yule atakayesimama na kuhutubia hadhira kwa Kiingereza cha lafudhi ya Malkia Elizabeth ataonekana msomi zaidi kuliko yule atakayerudia maneno yale yale kwa Kiswahili chenye lafudhi ya watani zangu.

Tunahitaji kufikia hatua ya kuanza kupima lugha yoyote kama nyenzo tu ya kufikisha ujumbe kwa wanaosikiliza na lugha zote zinapaswa kuwa na hadhi hiyo hiyo alimradi zinazungumzwa na wengi. Kufahamu lugha ya kigeni siyo kipimo cha usomi. Ingekuwa wapo wazungumzaji wa kutosha, hata Kizanaki nacho kingekuwa moja ya lugha ambazo zingetumika SADC.

Kwenye mdahalo niliyougusia nilishuhudia jinsi gani baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walivyopata shida kubwa kuuliza maswali na kujieleza kwa lugha ya Kiingereza. Naamini wangeweza kujieleza vizuri zaidi kwa Kiswahili.

Mara kadhaa nilizua ugomvi wa utani na wahudumu wa hoteli mojawapo ya Dar es Salaam ambako wafanyakazi wameelekezwa kuwasemesha wageni wote kwa lugha ya Kiingereza. Mara zote niliwajibu kwa Kiswahili na kuwashauri ni vyema kumsemesha mgeni kwa Kiswahili kwanza na kama haifahamu lugha, basi ndipo umsemeshe kwa Kiingereza. Niliuliza: “Wewe ukienda Marekani unasemeshwa kwa Kiswahili?”

Ni mifano inayoonyesha unyonge wetu wa kutetea lugha na tamaduni zetu na nguvu kubwa tunayotumia kuimarisha za wengine. Hatua ya SADC ya kutangaza Kiswahili kuwa lugha mojawapo rasmi inatuondoa huko na kutuelekeza kwenye kudumisha lugha na tamaduni zetu na kuondokana na fikra za kikoloni ambazo bado zinatawala maisha yetu.

Maoni: barua.muhunda@gmail.com

684 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!