Tusipotoshe kauli tukaiharibu nchi

Siku ya Ijumaa ya Agosti 9, mwaka huu nilipigiwa simu na marafiki zangu wawili kwa nyakati tofauti na kutoka maeneo tofauti. Simu ya kwanza ilitoka maeneo ya Oysterbay, Dar es Salaam na simu ya pili ilitoka jijini Mwanza kule Usukumani.

Katika simu zote mbili hizi ujumbe ulikuwa mmoja “…Brigedia Jenerali, umesoma gazeti [nalihifadhi] la Jumatano ya Agosti 7?” Niliwajibu wote “…hapana!..” Mmoja akaandika: “Tafadhali jitahidi ulipate, usome padri mmoja wa Kusini huko alivyoandika…” Nilipowajibu kuwa sikuwa na uwezo wa kulipata, mmoja wao aliniahidi kuniletea ili nami nilisome. Hatimaye mmoja wao alifanikiwa kuniletea lile gazeti nami nikalisoma.

Nilisoma kwa makini habari iliyoandikwa na msomi na mwanafalsafa mmoja. Habari yenyewe kuna picha ya Jaji Francis Mutungi, lakini habari yenyewe katika ukurasa ule nilivyosoma mimi, haikuhusiana kabisa na picha ile. Hapo sikuelewa, kwanini iwekwe picha ya jaji yule Msajili wa Vyama vya Siasa? Hakukuwa na uhusiano wowote kati ya picha ile na andiko katika ukurasa ule. Mpaka sasa sielewi mantiki ya picha ile pale. Labda wasomaji wengine walielewa mantiki ya picha pamoja na habari ile.

Kichwa cha habari kinasema: “Ni uongo kusema dini isihusiane na siasa.” Kichwa hiki kimeandikwa kwa herufi nene juu ya ‘background’ nyekundu,  na chini ya maneno yale lipo jina la mwandishi.

Baada ya kusoma nikakumbuka yale maneno ya marafiki zangu walionipigia simu wakisema: “Padri wa kwenu Kusini.” Ni kweli kabisa ninamfahamu mwandishi wa habari ile. Ni padri msomi aliyebobea katika mambo ya falsafa na amepata kuwa jialimu na gombera katika Seminari Kuu ya Peramiho. Ni mwandishi mzuri wa makala katika Gazeti la KIONGOZI. Nasikia siku hizi ni mwalimu katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino – SAUT.

Sasa mtu akisoma kile kichwa cha habari “Ni uongo kusema dini isihusiane na siasa” kisha akaja kusoma maelezo yaliyotolewa, kuna kitu ninaita mchanganyo wa maneno hapo. Haieleweki mwandishi alitaka kutuelewesha nini, maana nielewavyo mimi neno ‘uhusiano’ hapa hapakuwa mahali pake.

Ndipo yanazuka maswali namna hii. Nani katika nchi yetu hii alipata kutoa kauli namna hiyo? Kauli ilitolewa lini na katika mazingira gani? Mwandishi hakutupatia nafasi ili tujue hayo. Si hivyo tu, bali pembeni mwa habari ile kumeandikwa maneno tena kwa wino mwekundu yanayosomeka hivi: “Ukweli ni kwamba wanadini siasa inawahusu na wanasiasa dini inawahusu.” Hapo sasa sijaelewa alikuwa na maana gani.

Loo! Mwandishi naona amejichanganya. Kwanza hakutafsiri maana ya neno ‘uhusiano’ ili sote tukajua anamaanisha nini anaposema: “Ni uongo kusema dini isihusiane na siasa.” Hatukuambiwa uongo huu au kauli hiyo ilitolewa na nani, wapi na lini.

Vinginevyo huo unakuwa ni uvumi tu wala si uhalisia wa kauli kama kweli ilipata kutamkwa. Basi, inakuwa kauli ya kupuuzwa tu. Ieleweke kauli hii ya ‘Ni uongo kusema dini isihusiane na siasa’ ni mashitaka mazito sana yanayotakiwa kuthibitishwa kwa mifano hai.

Nionavyo hapa ni mkanganyo wa maneno, sijui kama kweli habari hii  imepewa kichwa sahihi cha ‘uhusiano’. Kwa tafsiri ya Kamusi ya Kiswahili Sanifu – TUKI, toleo la 3 la 2014, neno uhusiano lina maana ya “Hali ya kuwa na ufungamano; ni sifa ya ujirani mwema.”

Halafu kama neno ambalo mimi ninaamini ndilo lingepaswa kutumika katika habari hii. Neno lenyewe ni ‘mchanganyo’ ambalo kwa Kiswahili sanifu kadiri ya kamusi yetu lina maana ya tendo la kukusanya vitu mbalimbali na kuviweka pamojatendo la kukoroga vitu pamoja.

Kama mawazo yangu yatakuwa sahihi, basi naamini mwandishi wa makala ile hakujua tofauti kati ya maneno mawili hayo labda, ndipo ninasema kwa kuwa mwandishi ni msomi aliyebobea katika falsafa, labda tu nimkumbushe usemi huu wa Kilatini usemao: “Phyilosophia is indistictione” ukimaanisha kuwa falsafa inajikita katika utofautishaji.

Bado naamini kuwa neno uhusiano hapa halikustahili kutumika ila lingetumika neno mchanganyo. Haijapata kutamkwa kauli namna ile na kiongozi yeyote hapa nchini. Viongozi wote wa kidini na wa kisiasa wanashirikiana vilivyo katika nchi hii kutangaza amani na umoja wetu. Wanakuwa na vikao vya mazungumzo kati yao kuhusu mustakabali wa umoja, amani na mshikamano katika nchi yetu.

Kwa kuwa mwandishi hakutufafanulia maana ya neno uhusiano, wala hakutueleza uongo ule umetamkwa na nani, lini na katika mazingira yapi, nafikiri iko haja hapa ya kumkumbusha na pia kujikumbusha sisi sote ile kauli aliyopata kuitamka Baba wa Taifa kwa viongozi wetu wa dini humu nchini – maaskofu kule Tabora na masheikh kule Zanzibar.

Kuna wakati Baba wa Taifa alitoa ufafanuzi mzuri sana kuhusu DINI na SIASA hasa kwa vile alikwishaonja machungu yake wakati anaongoza Chama cha TANU hapa Dar es Salaam.

Baba wa Taifa alilielezea vizuri sana hili na napenda kwa faida ya wasomaji ni mnukuu hapa, hayo aliyoyatamka mara ya mwisho pale Hoteli ya Kilimanjaro mbele ya waandishi wa habari Machi 13, 1995.

Siku ile Mwalimu alitukumbusha hivi:

“…Niliwahi kulizungumza waliponikaribisha masheikh wa Zanzibar, nikafikiri hili niliseme. Niliwahi kulisema kwa maaskofu Tabora. Wakashtuka sana. Lakini, nikajitahidi kuwaelezea wakaelewa, wengine hawakupenda kuelewa. Basi, nikaenda siku moja kwenye Baraza la Idd Zanzibar pale. Masheikh wamekaa. Nikaona nitarudia ile ile hapa. Nikairudia. “NCHI YETU HAINA DINI” (Astakafilahi). Nikaendelea, nchi yetu haina dini, watu wetu wana dini, wengine wanazo dini na wengine hawana…Nikawaeleza masheikh wale taratibu, taratibu kabisa. Nikaendelea, ziko nchi zina dini rasmi, ndiyo dini ya nchi ile.

Waingereza dini yao rasmi ni Uanglikana na mfalme wa Uingereza lazima uwe Mwanglikana. Ndivyo katiba ya nchi. Hiyo ndiyo dini ya nchi na hiyo lazima na ndiyo katiba yao.

Zamani, hata Waziri Mkuu wa Uingereza lazima awe Mwanglikana. Sasa wamebadili. Lakini hata hivyo sijui Mkatoliki, sijui Mhindu wanaweza kuwa waziri mkuu. Wapi! Ndiyo dini rasmi.

Ireland pale dini rasmi ni Ukatoliki na kiongozi wao, kwa mujibu wa sheria nadhani lazima awe Mkatoliki.

Saudi Arabia ni nchi ya dini ya Uislamu. Lakini Uislamu peke yake hautoshi, ila Suni na mfalme lazima awe Suni.

Iran dini yake ni Uislamu, ni nchi ya Kiislamu. Lakini siyo Suni ni Shia. Wengine wanaweza kuruhusiwa, hata wa Suni wanaweza kuruhusiwa.

Pakistan ni Islamu rasmi. Wengine wanaweza kuruhusiwa nadhani Suni, wengine wanajidai pale wanasema ni Waislamu, lakini hapana, siyo kwa hapa, kafanyeni sehemu nyingine! Ndivyo zilivyo nchi huko.

Tanzania nikawaeleza masheikh pale, sivyo ilivyo. Hakuna kwa maana hiyo dini ya Watanzania.

Mimi ni Mkatoliki, lakini dini yangu, si ya Watanzania wala si dini ya serikali wala si dini ya CCM. Nyinyi hapa ni Waislamu safi.

Tukalikazania hilo nadhani likaeleweka. Likawa limeanza kabisa kueleweka. Lakini mambo haya ya msingi yanataka kusimamiwa katika nchi changa. Lazima lisimamiwe. Ukiacha watu wanarudi kule kule kwenye mawazo ya kijinga jinga. (NYUFA: uk. 27-28)

Suala la udini lilianzaje mpaka Mwalimu akaja kulikumbushia? Mwaka 1958 wazee wengi maarufu wa Dar es Salaam waliomsaidia Mwalimu kujenga TANU imara walikuwa ni Waislamu wa hapa hapa Mzizima. Na baadhi yao ndio waliingia katika ile Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU. Kwa vile wazee wale walikuwa waanzilishi, basi ni kawaida kutegemea wengi wao katika ule uchaguzi wa LEGICO (Baraza la Kutunga Sheria) mwaka ule wangepata nafasi ya uongozi.

Kumbe vigezo vilivyotolewa na mkoloni hasa kwa kile kipengele cha elimu isingeliwezekana wazee wa namna ile kuchaguliwa ndipo TANU ikawachagulia wasomi ambao kwa wakati ule na kwa bahati mbaya walikuwa Wakristo.

Hapo ndipo zilianza hisia za udini kusikika. Mwandishi Mohamed Said, katika kitabu chake kiitwacho “The Life and Times of ABDULWAHID SYKES” uk. 245 ameandika hivi: “…He was worried by the turn of events in TANU and the way politics was assuming new dimensions, Sheikh Takadiri was noticing  the encroachment of Christian leadership in TANU, which was going to be voted into the legislative cornea….” (Mohamed Said uk. 245).