Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Utabiri wa hali ya hewa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), umeonesha kuendelea kupanda kwa kiwango cha joto kwa miezi mitatu ya Januari, Februari na Machi 2025 pamoja na ukame.
Mamlaka za Hali ya Hewa katika nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zimeonesha mwaka 2025 kiwango cha joto katika mataifa hayo kimepanda kwa nyuzi joto mbili tofauti na kipindi kilichopita.
Hali hiyo imesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo hayo, hali inayoashiria kutokea kwa ukame.
Kwa kawaida, vipindi vya jua la utosi katika mataifa karibu yote ya Afrika Mashariki hufikia kilele mwishoni mwa Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea Kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea Kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ya mwanzoni mwa Februari 2025 ilisema jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine.
Kwa mujibu wa TMA, kipindi cha Februari 2025, hali ya ongezeko la joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo, ikielezwa hadi Februari 11, 2025, kituo cha hali ya hewa cha Mlingano mkoani Tanga, kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzijoto 36.0 sentigredi Februari 5, ikiwa ni ongezeko la nyuzijoto 2.1 sentigredi ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa Februari.

TMA nchini inasema kituo cha hali ya hewa kilichopo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam, kiliripoti kiwango cha juu cha nyuzijoto 35.0 sentigredi Februari Mosi, 2025 (ongezeko la nyuzi joto 2.2 sentigredi).
Inasema vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza Februari 2025 hususani maeneo ambayo msimu wa mvua za vuli umeisha.
Kama TMA ilivyokiri kuwa ongezeko hilo halikuwa kwa Tanzania pekee ni wazi hatua zinapaswa kuchukuliwa kwani taarifa zinaonesha wastani wa ongezeko la joto la dunia mwaka 2023 ulifikia nyuzi joto 1.40 za sentigredi na kuufanya kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia.
Hali hiyo inaelezwa ilichangiwa na uwepo wa El Nino ambayo ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la kati la Kitropiki kwenye Bahari ya Pasifiki na mabadiliko ya tabianchi.
Kutokana na hali hiyo, hata tathmini ya hali ya hewa msimu huu nchini Kenya inaonesha viwango vya mvua vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi na vinakadiriwa kuwa vya chini huku joto likipanda na kuwa juu kwa wastani wa nyuzi joto 35.
Tunaona viwango vya joto visivyo vya kawaida ikilinganishwa na misimu kadhaa iliyopita. Hii inaashiria hali ambayo si nzuri kwa eneo lote la Afrika Mashariki.
Kikubwa kinachotakiwa ni kwa wataalamu wa hali ya hewa katika mataifa hayo kushauri namna wananchi katika EAC wanavyopaswa kuishi na joto hilo.
Tunazishauri mamlaka zinazohusika kutoa elimu kwa wananchi kukinga afya zao na pia kushauri aina ya mazao ya kulima yanayohimili ukame kama mihogo, mtama, kunde, mbaazi na
mengineyo.