Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Jumla ya klabu 12 zitashiriki katika mashindano ya wazi ya klabu bingwa ya Taifa yaliyopangwa kufanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) Masaki kwa siku ya Jumamosi na Jumapili.

Klabu hizo ni Taliss-IST, Bluefins, MIS Piranhas, Mwanza, Dar es Salaam Swimming Club, na FK Blue Marlins. Klabu nyingine ni Champion Rise, Braeburn Arusha, Pigec, Lake na klabu mbili kutoka Uganda Flash na Starling.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Chama Cha Kuogolea Tanzania (TSA), Hadija Shebe alisema jana kuwa wanatarajia waogeleaji zaidi ya 200 kushiriki katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Pepsi, Knight Support, IST, Rap &Roll na Delhi Darbaaar DSM Restaurant.

Muogeleaji wa klabu ya Taliss-IST Mohameduwais Abdulatiff akipiga mbizi

Shebe amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha waogeleaji wenye umri kuanzia miaka tisa (9) na wenye miaka 15 na zaidi.

Amesema kuwa kutakuwa na makundi manne, kundi la miaka tisa na 10, 11 mpaka 12, 13-14, na 15 ambapo muogeleaji atakayeibuka wa kwanza atapata pointi 20 ambapo wa pili na tatu watapata pointi 16 na 14 kila mmoja.

“Waogeleaji watakaomaliza katika nafasi ya nne watapata pointi 12 ambapo wa tano, sita, saba, nane, tisa na 10 watazwadiwa pointi 10, 8, 6, 4, 2 na moja. Haya ni mashindano ya TSA na yapo kwenye kalenda ya chama, hivyo waogeleaji wenye vigezo wanatakiwa kushiriki katika mashindano haya,” amesema.

Amesema kuwa jumla ya staili tano za kuogelea zitashindaniwa katika mashindano hayo ambazo ni backstrokes, butterflies, individual medleys, breaststrokes na freestyles.

Mugoeleaji wa klabu ya FK Blue Marlins, Mischa Ngoshani akichapa maji

“Tunawashukuru wadhamini ambao mpaka sasa wamejitokeza kusaidia mashindano haya. Wametupa faraja na moyo wa kuendeleza mchezo huo, bado tunaomba wadhamini wajitokeze kudhamini mashindano haya. Ni mashindano ya kupima vipaji vya waogeaji wetu ambao wataiwakilisha nchi katika mashindano haya,” amesema Shebe.