KMC FC kuwafuata Ruvu Shooting na wachezaji 22

Kikosi cha wachezaji 22,viongozi pamoja na benchi la ufundi kitaondoka jijini Dar es Salaam leo kuelekea mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa siku ya Jumapili Februali tano katika uwanja wa Jamuhuri mkoani humo.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni itaondoka leo ikiwa imeshafanya maandalizi yake ya mwisho na kwamba wachezaji wote wapo tayari kukipiga katika uwanja huo ambao wapinzani Ruvu Shooting wanautumia kwa sasa.

KMC FC chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana inakwenda kwenye mchezo huo ikifahamu kuwa utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kwamba kila mmoja anahitaji matokeo hasa ukizingatia Ligi inakwenda ukingoni kwa sasa.

Aidha KMC FC katika safari hiyo itawakosa wachezaji muhimu wa nne kutokana na sababu za majeraha ambao ni Waziri Junior Shentembo, Daruweshi Saliboko, Awesu Ally Awesu pamoja na Matheo Anton.

” Tunakwenda kwenye mchezo mgumu tukiwa ugenini, tunafahamu umuhimu wa mchezo huo kwasababu tunahitaji matokeo mazuri na hata Ruvu Shooting nao wanayahitaji pia, hivyo kikubwa tunakwenda kupambana hadi dakika ya mwisho.

Ukiangalia kwenye mchezo wa mwisho KMC FC tulipoteza dhidi ya Namungo , matokeo ambayo yalimuumiza kila mmoja wetu, hivyo tunawaahidi mashabiki zetu kuwa pamoja na ugumu wa michezo tunayokutana nayo bado tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri.

KMC FC inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa imeshacheza jumla ya michezo 21 na hivyo kukusanya alama 23, huku ikishika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara.